Waziri Mkuu wa zamani ambaye pia ni Mbunge wa
Monduli, Edward Lowassa, amesema kuwa kumekuwa na tabia ya watu
kuombeana mabaya na mojawapo ni kuzushiana magonjwa na amependekeza kuwa
wakati umefika kwa Chama Cha Mapinuzi (CCM) kupima afya za wagombea
wake wa urais ili kujua ukweli nani mgonjwa.Kadhalika, amesema kuwa yeye ni mzima wa afya na yuko tayari kwa
chochote katika mchakato wa mapambano ya kuwaletea wananchi maendeleo. Lowassa aliyasema hayo jana nyumbani kwake mjini Dodoma alipokuwa
anajibu maswali mbalimbali ya wahariri ambayo yalihusu mambo mbalimbali
yanayomhusu, lakini siyo masuala ya sera na maono yake kuhusu uongozi wa
nchi kwa kuwa hotuba yake anayoitarajia kuitoa Jumamosi ijayo mjini
Arusha, ndiyo itaweka wazi maono yake kuhusu uongozi wa nchi.
“Leo hii hata nikikimbia kilomita 100 watasema Lowassa ni mgonjwa.
Pale Dar es Salama nilifaya mazoezi na watu wale Albino km tano.
Wakasema Lowassa amechoka sana amepata stroke amekimbizwa Ujerumani….
Huu ni uongo mtupu. Naomba tu kusema kuwa afya ni neema kutoka kwa
Mungu,” alisisitiza na kuongeza: “Twendeni tukapime afya zetu nami nitakuwa wa kwanza kupima tujue
nani mgonjwa. Mengine nimewa-challenge kwenye speech yangu sitaki
kuyasema hapa.”
RICHMOND
Akijibu swali kuhusu kadhia ya mkataba wa Richmond ambao ndio kiini
cha kujiuzulu nafasi ya uwaziri mkuu Februari mwaka 2008, Lowassa
alisema jambo hilo linajulikana na limekwisha kuandikwa sana. Hata hivyo, alisema kadhia hiyo ajenda haikuwa mkataba wa Richmond ila uwaziri mkuu.
Lowassa alisema awali alitaka kuvunja mkataba wa Richmond kama
ambavyo alifanya kwenye mkataba wa City Water chini ya utawala wa Rais
Benjamin Mkapa akiwa waziri wa maji na mifugo, serikali ikashitakiwa,
lakini walishinda kesi kwa kuwa walifanya jambo kwa mujibu wa sheria na
serikali ililipwa fedha nyingi.
Alisisiziza kuwa nia yake ilikuwa kuuvunja mkataba, serikali
ilishirikishwa, lakini mamlaka ya kufikia uamuzi huo hayakuwa yake
ingawa kila kitu kilikuwa kinajulikana wazi. Lowassa alisema hakuna senti moja ya serikali ililipwa Richmond na
kutaka aliyekuwa Waziri wa Fedha wakati huo, Zakia Meghji, aulizwe kama
kuna senti ya serikali ililipwa Richmond.
Alikumbusha kuwa hata Rais Jakaya Kikwete alimweleza wazi
aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati huo, Dk. Ibrahim Msabaha,
kutokulipa Richmond fedha za umma kwa kuwa ilikuwa imeonekena kuwa haina
uwezo wa kutekeleza mkataba wa kuzalisha umeme hadi kampuni hiyo
itakapotekeleza kwa ukamilifu makubaliano yaliyokuwa kwenye mkataba
husika.
Lowassa alisema kuwa aliwaita wataalam serikalini akiwamo
Mwanasheria Mkuu wa serikali na kuwambia kwamba kuna habari zimeandikwa
kwenye gazeti la The Guardian kwamba Richmond hawana uwezo wa fedha
kutekeleza mkataba wake. “Niliwaambia be careful. Nikaweka kwenye maandishi kwa Mwanasheria
mkuu. Kwa wale makatibu wakuu kulikuwa na timu ya serikali ya kujadili
chini ya Katibu Mkuu wa nafikiri Gray (Mgonja)… maamuzi yalichukuliwa na
mnajua yaliyotokea,” alisema.
Aliwataka wananchi kujifunza kutokana na yaliyotokea kwa Richmond
kwamba wakubwa wawili, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hilary
Clinton na Rais Barack Obama wa Marekani walifika Tanzania na
kuihakikishia serikali kwamba mitambo ya Richmond/Dowans ilikuwa ni
mizuri na salama na yenye uwezo wa kuzalisha umeme.
Alikumbusha kuwa kama isingelikuwa ni ubishi wa kisiasa jinsi
suala la Richmond lilivyoshughulikiwa, leo Tanzania isingekuwa kwenye
wakati mgumu kama ilivyo sasa kwani umeigharimu nchi Sh. bilioni 120
baada ya kushindwa kesi katika mahakama ya usuluhishi wa biashara huko
Paris, Ufaransa.
AKUBALIANA NA MBOWE
Alisema suala la serikali kuingia katika madeni hayo pia
liliibuliwa bungeni na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,
Freeman Mbowe, kwamba serikali imeshindwa kesi kule Ufaransa ambayo
iliamua na majaji Wazungu na sasa itatakiwa kulipa Dowans Sh. bilioni
120 kwa sababu tu ya ubishi wa kisiasa.
Akiwasilisha hotuba ya Kambi ya Upinzani Bungeni Mei 12, mwaka huu
aliitaka serikali isimame na isema sasa ni nani walihusika katika
kadhia ya Richmond ambayo ni matokeo ya minyukano ya kisiasa ndani ya
CCM ambayo sasa yameliingiza taifa katika hasara ya Sh. bilioni 120
baada ya kushindwa kesi huko Ufaransa.
Mbowe alisema katika mlolongo wa kushindwa kusimamia nchi,
kuendekeza makundi na vita vya kisiasa ndani ya CCM na serikali yake kwa
gharama ya Taifa, sasa linadaiwa Sh. bilioni 120 baada ya kushindwa
kwenye kesi ya Dowans/Richmond katika Mahakama ya Kimataifa ya
Usuluhishi (ICC) huko Paris.
“Serikali haijataka kuliweka jambo hili wazi na ni dhahiri kuna siri kubwa inayosababisha jambo hili kuwa la usiri mkubwa. Huko mbele ya safari jambo hili litaligharimu Taifa mabilioni haya
ya fedha ambayo yangeweza kuepukika kama ukweli, uwazi na haki
vingetawala mchakato mzima wa kashfa ya Richmond. Serikali isimame sasa
na ilieleze Taifa ni nani anasema kweli, ni nani alilidanganya Bunge na
ni nani analindwa na serikali katika kashfa hii?” alisema Mbowe.
UTAJIRI WAKE
Akizungumzia madai kwamba ana utajiri mkubwa, Lowassa alisema ana
ng’ombe kati ya 800 na 1,000 na nyumba chache. Ila kama kuna mwenye
kutaka kujua kila anachomiliki taarifa hizo zipo kwenye fomu yake ya
kutangaza mali na madeni inayowasilishwa kwa Tume Sekretariati ya
Maadili ya Viongozi wa Umma.
Hata hivyo, alisema: “Ninauchukia sana umasikini, ninapenda
utajiri. Napenda Watanzania wachukie umasikini. Ninautafuta uongozi wa
nchi hii ili kuwasaidia wananchi kuachana na umasikini siyo
kuukumbatia,” alisema.
Alitoa angalizo kuwa anatamani nchi hii iwe na watu wenye uwezo
wengi kama Reginald Mengi (Mwenyekiti Mtendaji wa IPP), Said Bakhressa
(Mmiliki wa AZAM), Nazir Karamagi, ili kusaidia kuondoa umasikini
nchini. Alisisitiza kuwa hana tatizo lolote na utajiri ambao umepatikana
kwa njia halali, ingawa kuna watu wanawaonea wenzao wivu kwamba
wamefanikiwa wakati wao walipata fursa, lakini kazi yao ni kuendekeza
ulevi na wanawake.
Alitaka wanasiasa waache kuwadanganya watu kwamba umasikini ni kitu kizuri. Akizungumzia madai kwamba amekuwa anatoa fedha nyingi katika
harambee mbalimbali anazoendesha nchini, Lowassa alisema kwamba hana
fedha ila ana marafiki.
Alisisitiza fedha zinazopatikana katika harambee zinachangwa na
marafiki wake mbalimbali na yeye kazi yake ni kuongoza harambee hizo
ambazo kwa maoni yake zimesaidia sana maendeleo katika jamii.
Aliwashauri wabunge wainge mfao huo kwa kufanya harambee mbalimbali
vijijini ili kusiadia kuchangia maendeleo ya jamii. Alikumbusha kuwa
shule za kata zilijengwa kwa harambee.
ELIMU
Lowassa alisema elimu ya Tanzania imevurugwa sana na juhudi kubwa
ni lazima zichukuliwe kurekebisha hali hiyo. Aliitaja elimu kuwa ndiyo
mkombozi wa matatizo mengine makubwa ya taifa kama ukosefu wa ajira kwa
vijana. Alisisitiza msimamo wake kuwa sera inapashwa kuwa elimu kwanza na
siyo kilimo kwanza, kwa kuwa ni kupitia elimu kilimo kinaweza kuboreshwa
na kuleta tija.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment