Social Icons

Pages

Tuesday, May 26, 2015

PROFESA KITILA MKUMBO: CHAMA CHA ACT-WAZALENDO

Profesa Kitila Mkumbo
WASIFU Umri: 44 Elimu: Shahada ya Sayansi ya Elimu (BSC Education), Shahada ya Uzamili (M.A) Saikolojia na Shahada ya Uzamivu (PhD) Saikolojia. Kazi: Profesa Mshiriki Shule ya Elimu (Duce).
Historia yake
Profesa Kitila Mkumbo ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mwanaharakati wa masuala ya kisiasa. Alizaliwa Juni 21, 1971 katika Kijiji cha Mgela wilayani Iramba, Singida. (Atatimiza miaka 44 Juni 2015). Profesa Mkumbo hakuwa na bahati ya kulelewa na wazazi, hivyo alisomeshwa kwa misaada ya ndugu na wasamaria wema.
Alisoma katika Shule ya Msingi Mgela iliyoko wilaya ya Iramba kati ya mwaka 1981-1987 kisha akajiunga Shule ya Sekondari Mwenge (Singida) na kusoma kidato cha kwanza hadi cha tano mwaka 1988-1991 na elimu ya Juu ya Sekondari akaipata pale Shule ya Sekondari Pugu kati ya mwaka 1992-1994 akijikita katika mchepuo wa PCB (Fizikia, Kemia na Bailojia).
Baada ya kuhitimu kidato cha sita alifanya kazi ya kuvua samaki katika Bwawa la Mtera huko Iringa kwa sababu ya kuwa na hali mbaya ya kiuchumi na baadaye alipata nafasi ya kwenda kujiunga na mafunzo ya polisi kwenye Chuo cha Polisi (CCP) Moshi kwa muda wa miezi miwili lakini alikatisha mafunzo baada ya kuchaguliwa kujiunga Chuo Kikuu.
Profesa Mkumbo alihitimu shahada yake ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1999 akisomea Sayansi ya Elimu na kupata daraja la kwanza, akaanza kazi hapo hapo Chuo Kikuu kama Ofisa Utawala, aliifanya kazi hiyo kwa miaka minne (1999 – 2003) na wakati anafanya kazi aliendelea kusoma shahada ya uzamili (M.A) akibobea katika Saikolojia, alihitimu shahada hiyo mwaka 2002.
Mkumbo ni mmoja wa wanafunzi waliofanya vizuri katika shahada ya uzamili na baada ya kufundisha Chuo Kikuu kwa miaka michache alipewa udahili katika Chuo Kikuu cha Southampton kilichoko nchini Uingereza ambako alitunukiwa shahada ya uzamivu akibobea pia katika saikolojia, hii ilikuwa ni mwaka 2008.
Mwaka 2010 hadi 2012 amekuwa Makamu Mwenyekiti wa Udasa (Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) na Mwenyekiti wa Udasa Oktoba 2014 hadi sasa.
Pia amekuwa mkuu wa Idara ya Elimu ya Saikolojia na masomo ya Mtaala katika UDSM 2009 – 2012, Mhadhiri Mwandamizi kuanzia 2011 – 2014,
 Mkuu wa Kitivo cha Elimu Duce na hatimaye Profesa Mshiriki kuanzia Julai 2014.
Mkumbo alianza siasa kama mwanachama wa CCM, baadaye alijiunga Chadema kawa mshauri muhimu wa chama hicho, pia akiwa mjumbe wa Kamati Kuu. Mwaka jana (2014), Profesa Mkumbo alitangaza kukihama chama chake cha zamani na kujiunga na chama kipya, ACT – Wazalendo, akiwa na rafiki yake wa siku nyingi, Zitto Kabwe. Hata katika chama hiki kipya yeye amekuwa mshauri mkuu. Watu nilioongea nao kutoka ndani ya ACT wanasisitiza kuwa Mkumbo ana mchango mkubwa na unaoonekana anapokuwa katika taasisi yoyote ile.
Profesa Mkumbo amekwishafanya tafiti zaidi ya 18 na zimechapishwa katika majarida ya kitaaluma ya kimataifa, amekwishaandika vitabu takribani vitatu, ameoa na ana watoto watatu.

Mbio za ubunge              
Profesa Mkumbo hakuwahi kugombea ubunge katika jimbo lolote hapa Tanzania, muda wake mwingi amejikita katika masuala ya kitaaluma na ushauri wa mikakati ya kisiasa. Japokuwa alipokuwa mwanachama hai wa Chadema alifanya harakati nyingi katika jimbo la Iramba (jimbo linaloongozwa na Mwigulu Nchemba wa CCM) na amewahi kuingia kwenye misukosuko mingi na hata kufunguliwa kesi ya kisiasa kwa sababu ya harakati zake.
Mtu yeyote yule anatambua kuwa harakati zile za Mkumbo jimboni Iramba (ambazo sina hakika kama amezisitisha kutokana kuhamia ACT) lazima zilikuwa na nia ya kugombea ubunge kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu au labda miaka mingine mitano ijayo. Ninachoamini ni kuwa, Mkumbo nadhani anajiandaa kuwa mbunge miaka ya mbele na huwenda bado ndoto hizo ziko kwenye damu yake.

Mbio za urais
Profesa Mkumbo hajatangaza nia ya kutaka urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ila sehemu kubwa ya wanachama wa ACT nilioongea nao walimtaja kama mmoja wa wanachama wa ACT wenye sifa zote muhimu za kuwa Rais wa nchi ikiwa chama hicho kitaamua kuweka mgombea urais katika uchaguzi wa Oktoba mwaka huu.
Nilipomuuliza yeye mwenyewe aliniambia kuwa ana mipango ya muda mrefu sana ya kisiasa na kwamba ataitekeleza kwa kadri alivyoipanga bila kufuata mipango na matakwa ya watoa maoni juu yake. Kwa hiyo, Profesa Mkumbo naye anachambuliwa kwa sababu ana sifa, vigezo na uwezo wa kuwa rais wa nchi, hata kama yeye mwenyewe hana mipango hiyo maana hatujui nini huwatokea viongozi mbalimbali na wakaweza kubadilisha mipango yao muda wowote mbele ya safari.

Nguvu zake
Sifa na nguvu ya kwanza ya Profesa Mkumbo ni kuwa kijana na msomi mahiri. Pamoja na kuwa wasomi wengi wanapewa madaraka na wanavurunda kama vile hawakwenda shule, bado mataifa yote duniani hayakwepi wala kukimbia dhana ya kuongozwa na watu walioelimika maana kuna wasomi wengi tu ambao ni waadilifu katika kazi zao, mmoja wao ni Profesa Mkumbo.
Ukiniuliza, mmoja kati ya wasomi wanaojua majukumu yao na wanayasimamia sana, nitakwambia Profesa Mkumbo ni mmoja wao. Nguvu na sifa vina maana kubwa sana kwa mtu ambaye anafikiri au anafikiriwa kuwa rais wa nchi.
Lakini jambo la pili, yeye ni mwanademokrasia thabiti na anayependa demokrasia iwe katika vitendo. Msomi huyu ni mmoja wa watu wanaoamini katika kujenga hoja na wanaopenda hoja zishindanishwe na zijadiliwe kwa uwazi na kisha hoja yenye mashiko ndiyo ipitishwe.
Ukitembelea ukurasa wake wa “Facebook” utaona watu wanaandika jambo lolote na humuoni akigombana nao, anapingwa waziwazi na wakati mwingine anatukanwa lakini anaacha uhuru wa wanaompinga na kumtukana uendelee. (Mimi binafsi nimekuwa sipendi mtu anitukane au anidhalilishe kwenye mitandao, napenda kupingwa kwa hoja na si kutukanwa na nakumbuka kila aliyenitukana niliishia kumuondoa miongoni mwa marafiki).
Jambo la tatu ambalo ni nguvu na sifa ya Profesa Mkumbo ni kubahatika kuwa kiongozi kila alipokaa, kusoma, kufanya kazi n.k. Amebahatika kuwa kiongozi tangu akiwa mdogo, nidhamu na kuwajali wenzake viliwavuta watu waliomzunguka kumtumia yeye awe mwakilishi wao. Amekuwa “kiranja” tokea akiwa Shule ya Msingi, Sekondari na Sekondari ya Juu. Uwezo huu wa kiuongozi uliendelea hata alipokuwa Chuo Kikuu (UDSM) kwani alichaguliwa kuwa Rais wa Serikali ya Wanafunzi (Daruso) kati ya mwaka 1998 – 1999.
Watu nilioongea nao kuhusu uongozi wa Mkumbo alipokuwa Daruso wameniambia alikuwa na karama za kipekee. Mmoja ambaye hivi sasa ni kiongozi mkubwa CCM na aliwahi kumpinga Mkumbo walipokuwa Chuo Kikuu, amenieleza kuwa Mkumbo alikuwa na ushawishi mkubwa kila akisimama mbele ya wanafunzi  na mmoja wa marais wa Daruso waliovuka vikwazo vya kupinduliwa.

Udhaifu wake
Moja ya mambo ambayo nayatazama kama udhaifu mkubwa wa Profesa Mkumbo ni uthubutu unaopita kiasi. Binadamu waliofanikiwa huthubutu kufanya mambo kadha wa kwadha lakini uthubutu kwa kiwango kisicholeta madhara kulingana na mahali walipo. Jambo hili halifanywi na Mkumbo na mara kadhaa amethubutu kufanya mambo yaliyowagutusha wenzie.
Mathalani, alipokuwa mwanachama wa Chadema alikiri kuhusika katika kuandaa waraka uliopewa jina maarufu la “waraka wa mapinduzi ndani ya Chadema”. Waraka ule ulikuwa ni moja ya mikakati ya msomi huyu kumpigia chapuo rafiki yake wa siku nyingi “Zitto Kabwe” ili ajiandae kuongoza chama hicho kupitia kwenye uchaguzi uliokuwa ukifuata. Waraka wa Kitila na wenzake ulitafsiriwa kama njama za mapinduzi ndani ya chama, usaliti na “kitu kisichofaa”.
Uthubutu huu wa Kitila ungewezekana sana kama angekuwa anafanya kazi katika vyama vikubwa mno duniani, siyo hapa Afrika Mashariki, tena nchini Tanzania. Lazima tukubali kuwa vyama vya kiafrika vimejijenga katika mifumo migumu sana kuingilika kidemokrasia na mara nyingi vina shida kwenye eneo hilo, ndiyo maana nilishtushwa na kujua kwamba Kitila amekubali kuhusika na waraka ule wakati anatambua kuwa yuko Afrika ambako demokrasia inapiganiwa kwa matakwa ya walioko madarakani kwa wakati husika.
Kwa siasa za Afrika, hata huko ACT ambako Kitila ni mwanachama leo hii, ukijaribu kuandaa waraka kama ule wa Chadema, nako anaweza kuonekana kama msaliti, mfanya mapinduzi, mhaini n.k. Ndiyo maana nasisitiza kuwa uthubutu huu unaopitiliza ni tatizo kubwa sana kwake na kwa watu waliomzunguka na tamaduni zao. Hata akiwa rais wa nchi atazungukwa na watu mbalimbali, aliowakuta na watakaomkuta, atakuwa na jukumu la kufanya mambo kwa uthubutu wa viwango vinavyokubalika ndani ya taasisi aliyomo kuliko “kuthubutu kulikovuka mipaka” ambako kunatazamwa kama uhaini kwa tamadani na demokrasia ya Afrika.
Lakini kuthubutu huku kulikopitiliza ndiko pia kumemfanya Mkumbo mara kadhaa atofautiane sana na menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwenye mambo kadha wa kadha. Ubishi na kutokukubali mambo kirahisi au kutokukubaliana na mazingira na tamaduni za mahali ulipo, ni mambo ambayo yanamgharimu sana na nayatazama kama udhaifu utakaoendelea kutishia ustawi wake kisiasa.

Nini kinaweza kumfanya asipitishwe
Moja ya masuala yanayoweza kumfanya Profesa Mkumbo apitishwe na ACT kugombea urais wa Tanzania ni kwa sababu ya “umashuhuri”. Umaarufu wa Mkumbo umetokana na nafasi na fursa ya kuonekana mara kwa mara katika shughuli za kitaifa za Chadema (wakati akiwa mwanachama), pia  yeye ni mmoja wa Watanzania waliowahi kushiriki katika mijadala mingi ya kitaifa na ambayo imekuwa ikioneshwa moja kwa moja katika vyombo vya habari kwa hisani ya Udasa na vyombo binafsi.
Sehemu kubwa ya Watanzania wanaofuatilia habari wanaweza kuwa wanamfahamu Mkumbo kwa namna moja au nyingine. Kwa sababu ACT ni chama kipya na kinahitaji kujikuza na kwenda juu kisiasa, nadhani kitahitaji mtu wa namna yake ambaye akipelekwa kwa wananchi, hawatauliza huyu ni nani, katokea wapi n.k.
Lakini pia, Mkumbo anaweza kupitishwa na ACT kugombea urais kwa sababu ya uzoefu wake wa kumudu mazingira magumu na majukumu mengi, achilia mbali uwezo wake mkubwa wa kujenga hoja majukwaani. Mkumbo amemudu mambo mengi tangu akiwa chuo kikuu, kwa mfano kumudu kuongoza Daruso na kisha akapata daraja la kwanza katika shahada yake siyo jambo dogo. Mimi nimekuwa kiongozi wa Daruso na sikudhani kama kiongozi wa Daruso anaweza kupata “First Class”, Uongozi ule ni kushughulikia matatizo ya wanafunzi kila kukicha huku vikao vya menejimenti vya chuo vinavyoamua masuala ya wanafunzi vikiendelea kila kona na unapaswa kuwapo kote huko. Pia kuongoza Udasa, Duce, na timu za kiushauri katika mipango na mikakati ya Chadema na baadaye ACT. Mtu anayemudu majukumu mengi namna hii ndani ya ACT anaweza kuwa Profesa Kitila pekee na huenda chama hicho kikahitaji mgombea urais anayemudu kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja.

Nini kinaweza kumwangusha?
Ikiwa ACT itakuwa na mwanachama mwingine ambaye ana sifa kumshinda Profesa Kitila (si kwa maana ya elimu tu), anaweza kabisa kupewa nafasi hii ya kugombea urais na Mkumbo akasaidia katika masuala mengine ya mikakati. Hii ndiyo sababu pekee ambayo inaweza kuzorotesha ndoto ambayo Mkumbo anaotewa, kwamba ana sifa, uwezo na vigezo vya kuongoza Tanzania.

Mipango mingine iwapo hatachaguliwa
Mipango mitatu hivi inaweza kufuatwa na Profesa Mkumbo ikiwa hatapewa kazi ya kupeperusha bendera ya ACT kwenye urais mwaka huu:
Mpango wa kwanza ni kuendelea kuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu, kazi ambayo anaifanya hadi sasa kwani yeye ni mmoja wa wataalamu wachache waliobobea na wenye uwezo mkubwa katika eneo la Elimu ya Saikolojia hapa nchini.
Mpango wa pili ni kuendelea kusaidia vitengo vya upangaji mikakati ndani ya chama kipya cha ACT Wazalendo ambacho naamini kwa uchanga wake kinahitaji wapanga mikakati wazoefu ili kukifanya kisidumae na labda kufa.
Na mpango wa tatu ni kuendeleza mchango wa ukuzaji wa fikra katika jamii ya Watanzania ambayo ina matatizo makubwa katika kufanya siasa za kuvumiliana na kukubali changamoto mpya.

Hitimisho
Safari ya kisiasa ya Profesa Mkumbo inaweza kuathiriwa na ukuaji au uzorotaji wa Chadema na Ukawa. Kwa sababu ni mwanachama wa ACT na kwa kusema ukweli, ukuaji wa ACT kwa kiasi kikubwa utategemea sana na uzorotaji wa Chadema, ndiyo kusema kuwa ukuaji wa Chadema kwa kasi yoyote unaweza kuathiri safari ya kisiasa ya ACT na Prof Kitila mwenyewe.
Kwa mfano, hata kama ikitokea Profesa Mkumbo akagombea urais wa Tanzania, ikiwa mgombea wa Ukawa atakuwa na nguvu kubwa kwa wananchi, Mkumbo na ACT hawatakuwa na fursa nzuri tena, labda mpaka uchaguzi mwingine.
Pamoja na yote hayo, namtakia kila la heri “rafiki yangu” Profesa Kitila Mkumbo katika kufikia safari yake kisiasa na kiu ya mabadiliko ya Tanzania afikiriayo.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: