Social Icons

Pages

Tuesday, May 26, 2015

PETER MZIRAY, RAIS MTENDAJI APPT-MAENDELEO

Mwenyekiti wa APPT-Maendeleo, Peter Mziray akihutubia kwenye moja ya mikutano ya hadhara ya chama hicho jijini Dar es Salaam.
Historia yake
Peter Mziray ni Rais Mtendaji wa Chama cha APPT Maendeleo, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa na kitaaluma ni mtaalamu wa mifugo na uchumi wa kilimo.
Mziray alizaliwa Oktoba 10, 1959 katika Kijiji cha Kankokoro, Kata ya Kihurio, Wilaya ya Same, Mkoa wa Kilimanjaro. (atafikisha miaka 56 Oktoba).
Alianza elimu ya msingi wilayani Same katika Shule ya Jitengeni kati ya mwaka 1966 – 1972 kisha akaendelea na sekondari mkoani Dar es Salaam katika Shule ya Pugu kwa kidato cha I hadi IV kati ya mwaka 1973 – 1976. Masomo ya juu ya sekondari (kidato cha V na VI) aliyapata katika Shule ya Sekondari Mkwawa mkoani Iringa kati ya mwaka 1977 – 1978.
Baada ya kumaliza kidato cha sita, Mziray alihudhuria mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kwa mujibu wa sheria kwenye Kambi za Bulombora, Kigoma na Buhemba mkoani Mara kati ya mwaka 1979 – 1980.
Alijiunga na Benki ya NBC, Tawi la Barabara ya Boma, mjini Moshi na kufanya kazi ya ukarani kati ya mwaka 1981 – 1983. Mwaka 1981 – 1983 aliajiriwa katika kiwanda cha kusindika ngozi ya ng’ombe, mbuzi na kondoo kilichokuwa jijini Mwanza akiwa na cheo cha msimamizi wa uzalishaji.
Mwaka 1983, Mziray alikwenda Urusi kuanza masomo ya kitaalamu katika Chuo Kikuu cha Lumumba kilichoko Moscow. Alisomea Shahada ya Ufugaji wa Wanyama (Animal Husbandry), alipohitimu aliendelea na Shahada ya Uzamili katika fani hiyohiyo na kuhitimu mwaka 1989 na kuwa mtaalamu wa mifugo aliyebobea.
Alipokuwa Urusi aliongoza chama cha wanafunzi Watanzania walioko Urusi akiwa katibu (kilikuwa na wanachama zaidi ya 600), alifanya kazi kubwa ya kutatua matatizo ya wanafunzi huko ughaibuni, akishirikiana kwa karibu na Ubalozi wa Tanzania, Moscow (USSR).
Mziray alirejea nchini na kuajiriwa na Wizara ya Kilimo na Mifugo mwaka huohuo 1989. Mwaka 1991 alikwenda Uingereza kwa masomo ya muda mfupi katika Chuo Kikuu cha Bradford ambako alitunukiwa Cheti cha Mipango ya Miradi ya Kilimo. Wakati huohuo, alianza kusomea masuala ya uchumi wa kilimo kwa ngazi ya stashahada katika Chuo Kikuu cha Reading kuanzia mwaka 1992 hadi alipohitimu mwaka 1993 na kuunganisha tena Shahada ya Uzamili ya Uchumi wa Kilimo/Mifugo ambayo aliikamilisha mwaka 1994.
Aliporejea nchini mwaka 1994, aliendelea kutoa mchango wake kwa nchi yetu akishiriki kubuni na kuanzisha miradi mbalimbali ya kilimo na ufugaji ambayo ilipitishwa na wizara, kuwatembelea wakulima na wafugaji ili kutoa ushauri na kufanya machapisho mbalimbali juu ya kilimo na mifugo hadi alipoamua kustaafu rasmi mwaka 2000.
Mziray amebobea vizuri katika lugha tatu za kimataifa: Kiswahili, Kiingereza na Kirusi na amemuoa Harumi na wana watoto na familia yenye furaha.

Mbio za ubunge
Alianza mbio za ubunge mwaka 1995, alifanya hivyo kupitia NCCR – Mageuzi lakini akashindwa kupenya katika kura za maoni za ndani ya chama hicho katika Jimbo la Same Mashariki. Alirejea kazini na kuendelea na utumishi kwa sababu sheria ilikuwa inaruhusu hali hiyo.
NCCR ilipovurugika na baadhi ya wanachama wake na viongozi kujiondoa na kwenda TLP, Mziray naye alikuwa mmoja wao na mwaka 2000 akapata nafasi ya kuwania ubunge wa Jimbo la Same Mashariki kupitia TLP, aliamua kuacha kazi wizarani na kwenda jimboni ambako alipambana na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Daniel Yona. Mziray hakufanikiwa kushinda ubunge mwaka huo.
Baadaye mwaka 2001 aliomba ridhaa ya TLP ili apitishwe na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki. Alikuwa miongoni mwa Watanzania waliojieleza bungeni kuomba nafasi hiyo lakini hakufanikiwa kuchaguliwa kwa sababu chama chake kilikuwa na wabunge wachache hivyo kikakosa uungwaji mkono kwa sababu nafasi za ubunge ule huchukuliwa kwa kiasi kikubwa na wabunge kutoka vyama vyenye wabunge wengi.
Baada ya kuona mambo hayaendi ndani ya TLP, Mziray alishirikiana na wenzake kadhaa kuasisi chama kipya, kikiitwa PPT – Maendeleo (Sasa kinaitwa APPT Maendeleo) na mwaka 2005 akagombea ubunge wa Same Mashariki kwa tiketi ya PPT.
Mziray alifanikiwa kumtikisa Anne Kilango Malecela wa CCM kiasi ambacho wengi walidhani angeshinda. Matokeo yalipotangazwa, Mziray alipata kura 11,665 (asilimia 34) akiachwa kwa kadri na Kilango ambaye alipata takriban mara mbili ya ushindi wa Mziray. Kura 20,333 (asilimia 60.4).
Mbio za urais
Alianza mbio za urais mwaka 2010 baada ya kupitishwa na chama chake APPT Maendeleo. Wakati anagombea urais, watu wengi hawakuwa wanamfahamu vizuri na ilidhaniwa kuwa anapoteza muda lakini matokeo yalipotangazwa, aliibuka kwenye nafasi ya nne akipata asilimia 1.15 (kura 96,933).
Mwaka huo pia chama chake kilipata madiwani watatu na mmoja wa viti maalumu kutoka mikoa ya Mara na Kilimanjaro na kikaingia kwenye orodha ya vyama vya siasa vichanga vinavyopata ruzuku.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu 2015, Mziray anaonyesha kila dalili kuwa ataingia kwenye kinyang’anyiro kwa mara nyingine ili kupandisha kura zake lakini pia katika malengo ya kuzidi kukiimarisha chama chake.

Nguvu yake
Mziray ni mtu wa umri wa kawaida na hata ukitizama mambo yake yanaendana na umri huo. Ana sifa zote za kuitwa kijana imara hata kama anakaribia miaka 60 na mara nyingi ukimkuta katika mikutano mbalimbali utamuona akibadilishana mawazo na kuwapa vijana changamoto. Kuwa karibu na vijana ni sifa muhimu kwa mtu anayetaka kuwa Rais.
Jambo la pili linalomuongezea nguvu mwanasiasa huyu ni weledi wake kitaaluma. Mziray ni msomi mwenye shahada tatu (mbili zikiwa za uzamili), stashahada ya juu moja na stashahada ya kawaida moja. Viwango hivi vya elimu alivyopitia kutoka vyuo vinavyoheshimika duniani vinamfanya kuwa mmoja wa Watanzania wachache wenye weledi mpana na ambao wanahitaji kupigwa msasa katika maeneo mengine, ila si kwenye elimu.
Jambo la tatu linalompa Mziray nguvu ni ushawishi wake kwa vyama vingine vya siasa (hususan vyama vipya, vidogo au vinavyojiimarisha hivi sasa) kupitia katika Baraza la Vyama vya Siasa. Alichaguliwa kushika wadhifa wa mwenyekiti wa Baraza hilo kwa mara ya pili mwaka 2014. Ana mwanya mzuri wa kupenyeza ajenda muhimu na hakika hii ni nafasi ya pekee kwa mwanasiasa ambaye yuko mbioni kusaka madaraka makubwa ya nchi.

Udhaifu wake
Moja ya udhaifu wake mkubwa umekuwa namna anavyotumia nafasi anazopewa kujijenga na kusahau kuwa kuna watu waliompa kwa malengo maalumu.
Mathalan, akiwa Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa haikutegemewa kuwa angesimama kwenye Bunge Maalumu la Katiba na kuanza kuwaponda wabunge wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) walipoamua kuondoka bungeni. Alinukuliwa akisisitiza kuwa hao walioondoka hawajapunguza kitu kwa sababu yeye akiwa mwenyekiti wa baraza la vyama na msemaji wa baraza hilo bado yumo katika Bunge.
Udhaifu huu wa Mziray unaendana na ile sifa ya ukigeugeu kwa sababu awali, alionekana pia kuunga mkono hoja za Ukawa, kabla ya kuamua kugeuka na kuunga mkono hoja za CCM. Kama Mziray asipojitathmini, jambo hili linamharibia rekodi yake njema na haliwezi kufutika kirahisi.
Lakini kubwa kuliko yote ni kwamba, yeye ni mmoja wa wanasiasa wakubwa kutoka vyama vya upinzani, walioshiriki katika hatua zote za Bunge Maalumu la Katiba na kuzalisha katiba ambayo madhehebu ya kidini, mashirika ya kiraia na vyama vikubwa vya upinzani vinailalamikia kuwa imesaliti matakwa na mahitaji ya kikatiba ya Watanzania. Kwa ile dhana ya siasa za vyama vya upinzani vinavyowapigania wananchi wa chini ili sauti zao zisikike, huenda Mziray anaweza kupwaya katika dhana hiyo.
Katika eneo la udhaifu pia, namtazama Mziray kama kiongozi wa vyama vya siasa aliyeshindwa kabisa kutengeneza, umoja, mshikamano na ustawi wa vyama (hususani vyama vya upinzani), ili kuvijengea misingi ya kujiandaa kushika dola kirahisi muda mfupi ujao. Nadhani anahitaji kujitathmini pia kwenye eneo hili, kuona kama anavitendea haki vyama anavyoviongoza kupitia Baraza la Vyama vya Siasa.
Ukienda katika Baraza la Vyama vya Siasa utaona bado kuna mgawanyiko mkubwa, kuna vyama vya siasa vyenye wabunge na vina sauti zao, kuna vyama vya siasa vidogo vyenye misimamo ya kiupinzani na kuna vingine vinaunga mkono ajenda za CCM waziwazi.
Haya yote yanafanyika chini ya uongozi wake na kuendelea kwake kunafifisha ukuaji wa demokrasia na kama tukimpima katika mizani ya namna hii, tunaweza kumhukumu kwa udhaifu wa kushindwa kuunganisha walau ajenda chache ambazo vyama vyote vinaweza kukubali kuzipigania.

Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Mambo kama matatu hivi ndiyo yanayoweza kukifanya Chama cha APPT Maendeleo kimpitishe na kumtangaza Mziray kuwa mgombea wake wa urais:
Jambo la kwanza ni kwamba ndiye mwenye uwezo wa kipekee katika chama chake. Kwa wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa katika nchi, unapotaja APPT Maendeleo unamzungumzia Mziray. Hajajenga watu wengine kuwa na jina kubwa kama lake katika ulingo wa siasa na hivyo fursa ya kupitishwa kugombea urais imo mikononi mwake.
Lakini sababu ya pili itakayomfanya apitishwe na chama chake ni kwa kuwa aligombea urais mwaka 2010. Fursa ile ilimfanya ajitambulishe kwa jamii pana ya Watanzania na kukitambulisha chama chake, kwa hivyo APPT inaweza kuwa bado ina nafasi ya kumtumia tena kukipaisha chama hicho kama alivyojaribu mwaka 2010.
Mwisho, naona anaweza kuvuka kizingiti na kuteuliwa kugombea urais kupitia chama chake kwa sababu ana uzoefu mkubwa wa masuala ya kimataifa (amesoma nje ya nchi shahada zake zote) lakini pia amepata fursa ya kufanya kazi serikalini na hata kuzunguka nchi mara nyingi akishiriki katika siasa. Nadhani hakuna mwana APPT mwingine aliyeifanya kazi hii kama Mziray.

Nini kinaweza kumwangusha?
Jambo moja kubwa ninaloliona linaweza kumwangusha Mziray kwenye mchujo ni ikiwa atapatika mpinzani thabiti ndani ya chama chake. Hadi sasa sioni kama APPT Maendeleo ina mpinzani thabiti kabisa wa kushindana naye ndani ya chama hicho.
Lakini kwa kuweka akiba ya maneno, huenda kina wanachama wengine wazoefu na wenye sifa zinazokaribiana na zake lakini ambao hawajajitangaza. Muda ukifika tutajua na wakijitokeza watu wa namna hiyo, sitasita kusema kuwa anaweza kuangushwa.

Asipochaguliwa (Mpango B)
Kama Mziray hatachaguliwa kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia APPT Maendeleo, namuona akijikita tena jimboni Same Mashariki kuusaka ubunge kwa mara ya tatu.
Ikumbukwe kuwa, Mziray ana nguvu kubwa na ushawishi pale Same Mashariki na nathubutu kusema kuwa kama katika chaguzi za hivi karibuni angekuwa mgombea wa moja ya vyama vya upinzani vyenye nguvu kubwa zaidi, huenda leo angekuwa bungeni mjini Dodoma.
Lakini pili, kama hatapitishwa kuusaka urais, kiongozi huyu anaweza kabisa kurudi vijijini na kuhamasisha masuala ya kilimo na ufugaji. Tukumbuke kuwa nchi yetu inategemea kilimo kwa kiasi kikubwa kiuchumi. Wakulima vijijini wana hali mbaya na bado wanalima kwa teknolojia za zamani. Watu kama Mziray ni wachache sana hapa Tanzania (kwa elimu ya kilimo na mifugo). Anaweza hata kuwa na mchango mkubwa zaidi kwa Taifa kuliko hata kuwa katika siasa.

Hitimisho
Mziray anakabiliwa na changamoto kubwa zaidi kisiasa mwaka huu kama ataamua kugombea urais. Tayari karata za kiuchaguzi zinaelekea kuipa nafasi nzuri zaidi Ukawa kuwa mshindani mwenye nguvu kupita kiasi dhidi ya CCM. Jambo hili linaweza kuwa si rafiki kwa vyama vinavyojiimarisha kama APPT na kwa wanasiasa ambao wanajijenga kupitia vyama hivyo, kama Mziray.
Kama Mziray ataendelea kufanya siasa nje ya Ukawa kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, huenda chama chake kikaporomoka au njia bora ya yeye kuendelea kujiimarisha kisiasa inaweza kuwa ni kujiunga na vyama vingine vidogo ambavyo hata hivyo vina mielekeo ya kuja kusaidiana na CCM ili kupambana na Ukawa. Ni vigumu kutabiri hali ya mambo itakavyokuwa lakini pamoja na yote hayo, namtakia Mziray safari salama na kila la heri katika mipango yake ya kisiasa huku tuendako.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: