Siasa ni dhana pana inayoakisi utaratibu na mwenendo wa jumla wa maisha ya mwanadamu katika jamii inayomzunguka.
Siasa huamua aina ya uongozi wa nchi husika kutegemea matakwa ya watawala. Ziko nchi zinazoongozwa kifalme na kisultani na
nyingine huongozwa kwa utawala wa kiimla. Kadhalika, kuna nchi
zinazoongozwa kijeshi na zipo ambazo huongozwa kwa misingi ya dini
rasmi. Nchi nyingine huongozwa kidemokrasia.
Ifahamike kwamba mfumo wa siasa katika nchi yoyote
duniani huongozwa na mapambano ya kimatabaka, huku tabaka la chini
likipigania kujikwamua na wakati huohuo, tabaka tawala likiimarisha
mbinu za kuendelea kutawala. Kwa lugha nyingine, siyo kila chama cha siasa
kinaweza kuwa na lengo la dhati la ukombozi na wala siyo kila serikali
na mamlaka za kisheria zinaweza kuwa na nia ya kuleta ustawi wa watu
wake.
Hoja hiyo ndiyo inayonisukuma kuupima mchango na wajibu wa vyama vya upinzani barani Afrika, ikiwamo Tanzania.
Tulipopata uhuru mwaka 1961, Tanganyika ilikuwa nchi ya vyama vingi vya siasa kwa mujibu wa Katiba.
Vyama vilivyokuwapo wakati huo ni Tanganyika
African National Union (Tanu), United Tanganyika (UTP), African National
Congress (ANC) na All Muslim National Union of Tanganyika (AMNUT).
Baada ya uhuru (1962), vyama vingine vinne
vilivyosajiliwa ni People’s Convention (PCP), People’s Democratic (PDP),
Nationalist Enterprise na African Independence Movement.
Vyote hivi vilifanya kazi kubwa ya kukuza demokrasia na ustawi wa nchi.
Hata hivyo, Tanu iliaminiwa zaidi kwa sababu ya sera zake zilizolenga kuleta uhuru wa kweli na ujenzi wa misingi ya Taifa. Hata hivyo, baadaye kwa sababu ya uchanga wa Taifa
letu, ikaonekana ni vyema kisheria kibaki chama kimoja cha siasa ili
kisimamie jukumu la ujenzi wa nchi na utaifa.
Hiyo ndiyo siri kubwa ya Watanzania kutokuwa na udini, ukabila, chuki au ubaguzi wa aina yoyote.
Mfumo wa demokrasia ya vyama vingi ulirejeshwa tena mwaka 1992 kwa Sheria namba 5 ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992.
Kimsingi vyama vya upinzani vimekuwa vikifanya
kazi nzuri ya kuimarisha demokrasia nchini; muda wote vimekuwa
vikiisimamia, kuikosoa, kuishauri Serikali ya CCM na kuirudisha kwenye
mstari pale inapokwenda kombo.
Kwa kiwango kikubwa, vyama hivi vimeleta mwamko mkubwa kwa wananchi katika ushiriki wa masuala ya siasa na elimu ya uraia. Zaidi ya hayo vyama vya upinzani vimekuwa
vikifanya kazi nzuri ya kuibua tuhuma na kashfa mbalimbali dhidi ya
baadhi ya viongozi na watendaji wa Serikali.
Baadhi ya kashfa hizo ni wizi na matumizi mabaya
ya madaraka, urasimu na umangimeza, mikataba mibovu, rushwa na upendeleo
katika ajira na utoaji wa zabuni. Nyingine ni kiburi cha fedha na ulevi wa madaraka na kauli za ovyo zinazotolewa na baadhi ya watendaji na viongozi wa Serikali.
Mchango huo wa vyama vya upinzani umeizindua
Serikali ya CCM na kuchukua hatua za kujiimarisha zikiwamo za
kuwawajibisha watendaji na viongozi wazembe na wanaokiuka miiko ya
uongozi. Pamoja na kazi hiyo nzuri, vyama vya upinzani,
bado vina udhaifu mkubwa. Vingi havina sera zaidi ya wimbo wa kutaka
kuing’oa CCM madarakani. Baadhi havina ofisi wala mtandao nchi nzima.
Pia, demokrasia ndani ya vyama hivyo imeminywa.
Katika chaguzi zote tangu 1995 karibu sura za wagombea urais na
uenyekiti ndani ya vyama hivyo ni zilezile. Mara nyingi wanasiasa wapya wa upinzani wanapotaka
kugombea nyadhifa za juu ndani ya vyama hivyo huitwa wasaliti na kupata
misukosuko mikubwa.
Uzoefu unaonyesha kwamba vyama hivyo vingi
huibuka ghafla wakati wa chaguzi na kutoweka tena baada ya shughuli
hiyo kumalizika. Havina benki ya viongozi na makada kama ilivyo CCM. Mara nyingi
vyama vya upinzani husubiri CCM watibuane ndipo vipate wagombea
wanaokihama chama hicho tawala.
Mtazamo wangu ni kwamba vyama vya upinzani vimetoa mchango wenye tija kwa maendeleo ya Taifa letu.
Hata hivyo, wito wangu ni kwamba vyama vya
upinzani viache kupinga kila jambo, badala yake visifie pia mazuri
yanayofanywa na Serikali ya CCM.
Upinzani ni kutoa changamoto ambayo ni dhana inayojumuisha kukosoa na pia kusifia inapobidi.
Kwa upande mwingine, CCM isivione vyama vya
upinzani kama maadui, bali wavione kuwa ni wadau muhimu wa maendeleo ya
uchumi na kijamii pamoja na ustawi wa demokrasia.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment