Wananchi wa vijiji vinane katika Wilaya ya Sengerema
mkoani Mwanza, wamemkumbusha Rais Jakaya Kikwete, kuhusu
ahadi aliyowapa ya kuwajengea barabara ya lami yenye urefu wa zaidi ya
kilomita 40 ili kupunguza msongamano wa magari yanayotumia kivuko cha
Kigongo – Busisi kwenda mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani.
Wakizungumza baada ya kuzinduliwa kwa kivuko kipya cha Mv Super
Samar, wananchi hao wa vijiji vya Kamanga, Nyamazugo, Nkungule,
Nyakahako, Kasomeko, Katunguru, Nyamililo na Ibondo, walisema Rais
Kikwete anapaswa kutimiza ahadi yake kabla hajaondoka madarakani.
William Nkandi mkazi wa Kamanda, alisema kuzinduliwa kwa kivuko
hicho kipya kitakachotoa huduma za usafiri wa majini kati ya Jiji la
Mwanza na Sengerema kupitia kivuko cha Kamanga, kitasaidia ufupisho wa
safari iwapo Rais Kikwete atatimiza ahadi yake aliyoitoa mwaka 2010.
Naye Dk. Fortunatus Masha, mkazi wa Kamanga, alisema ili kuwasaidia
wananchi wa vijiji hivyo na ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni za
uchaguzi mkuu 2010, inampasa Rais Kikwete kutimiza ahadi ya ujenzi wa
barabara ya lami kabla hajaondoka madarakani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni ya Mv Samar, Salum Ally,
alisema kivuko hicho kina uwezo wa kubeba abiria 250 na magari madogo
yasiyopungua 50 ama makubwa 24, hivyo kuwasaidia wananchi wa vijiji
hivyo.
Ally alisema kivuko hicho tayari kilifanyiwa ukaguzi na maofisa wa
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi kavu na Majini (Sumatra) na kuona
kina uwezo wa kuchukua abiria na mizigo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kivuko hicho, Ofisa Mfawidhi wa
Sumatra Mkoa wa Mwanza, Michael Rogers, alisema kivuko hicho kitachangia
kukuza uchumi wa wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa pamoja na kutoa ajira
kwa vijana.
Kivuko hicho kilichojengwa na kampuni ya Songoro Marine, kimegharimu kwa gharama ya Sh. milioni 900.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment