Wadau wa Taasisi za Mwasilianao nchini wakisikiliza mada kwenye mkutano
wa kutoa elimu kwa ajili ya wadau hao kujiandaa kwa biashara ya wazi ya
masafa ya mawasiliano ifikapo Oktoba mwakani. Mkutano huo ulifanyika Dar
es Salaam jana.
Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA), imeanza kutoa elimu kwa wadau wa
mawasiliano nchini ili kujiandaa kwa biashara ya wazi ya masafa ya
mawasiliano ifikapo Oktoba, mwakani. Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma
alisema mamlaka hiyo itaanza kuuza masafa hayo kwa wadau wake ambao ni
kampuni za simu za mkononi, redio na televisheni.
Alisema lengo la kufanya hivyo ni kutaka
kukabiliana na changamoto ya mahitaji ya masafa ya mawasiliano, ambayo
kwa sasa ni kidogo ikilinganishwa na mahitaji.
Profesa Nkoma alisema wadau hao watakuwa na fursa
ya kulipia masafa hayo kwa kuzingatia vigezo vitakavyowekwa na TCRA
vinavyochagizwa na mabadiliko ya tenkolojia mpya ya mawasiliano.
“Faida za kufanya mnada kwa uwazi na haki ni
kutaka kuepuka malalamiko ya wadau, kila mdau anahitaji kupata masafa
lakini yapo kidogo, masafa hayo yanaanzia 694MH mpaka 862MH. Kila mmoja
atapata kwa kuzingatia vigezo, lakini kabla ya kufikia hatua ya mnada
huo, leo (jana) tutatoa elimu juu ya ugawaji na vigezo ili wavifahamu
pamoja na mambo mengine,” alisema Profesa Nkoma.
Kwa upande wake, Mhandisi Masafa kutoka mamlaka
hiyo, Victor Kweka alisema mbali na faida hizo, nyingine ni kupunguza
matumizi ya kuwa na minara mingi ya kampuni za simu katika eneo lenye
umbali mfupi.
“Yote haya ni kutokana na mabadiliko ya teknolojia kukua zaidi kutoka analojia kwenda dijitali,” alisema Kweka. “Masafa hayo yatasaidia kuongeza kasi ya kufika
mbali zaidi na kwa urahisi ukilinganisha na ilivyo sasa, kampuni
zinatumia minara mingi na wakati mwingine wananchi huilalamikia.”
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment