Social Icons

Pages

Wednesday, May 27, 2015

WAPINZANI WALIA NA BRELA BENGENI

David Kafulila 
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imelia na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) kuwa imekataa kutoa majina ya wamiliki wa Kampuni ya Simba Trust Ltd inayomiliki asilimia 50 ya hisa za Kampuni ya PAP iliyohusika katika sakata la ukwapuaji wa fedha zaidi ya Sh300 bilioni  kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow.
Hayo yamo katika hotuba ya msemaji mkuu wa kambi hiyo wa Wizara ya Viwanda na Biashara kuhusu bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2015/16, David Kafulila, iliyosomwa  bungeni jana kwa niaba yake na Rajab Mbarouk Mohamed.
“Kukataa kutoa majina hayo inaunganishwa na dhana kwamba wamiliki wa  kampuni hiyo ni viongozi waandamizi wa Serikali ya CCM,” alisema Mohamed. “Hivyo, Watanzania waelewe kuwa uhusiano uliopo kati ya Simba Trust na PAP ni kaburi la CCM ifikapo Oktoba,” alisisitiza.
Alisema wakati umma unataka kuelewa wamiliki wa kampuni hiyo iliyohusika na ukwapuaji wa fedha za escrow, Brela imegoma kutoa majina ya wamiliki wa kampuni hiyo ya Simba Trust.
Aliitaka Serikali kueleza ni kwa nini taasisi hiyo ya umma bado inakataa kutaja majina ya wamiliki hao.

Ubinafsishaji wa viwanda
Alisema Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara,  Dk  Abdlallah Kigoda hakupewa wizara hiyo kwa bahati mbaya, bali ni mkakati rasmi uliopangwa kwa sababu alikuwa muhusika mkuu katika mchakato mzima wa ubinafsishaji wa viwanda vyetu.
“…Sasa ni muda mwafaka kwake kuhakikisha anarekebisha makosa aliyoyafanya pamoja na Serikali ya CCM,” alisema Mohamed. Pia, alimtaka Waziri huyo kulitaarifu Bunge ni viwanda vingapi hadi sasa vilikiuka masharti ya mkataba wa mauzo ambayo Serikali imechukua hatua.

General Tyre
Akijibu hoja za wabunge, Dk Kigoda alisema wizara yake ikishirikiana na wadau mbalimbal ikiwamo Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Msajili wa Hazina, Ubalozi wa Tanzania nchini Ujerumani na Shirika la Maendeleo Nchini (NDC), imeweza kufikia makubaliano na mbia Mwekezaji wa Kiwanda cha Matairi cha General Tyre (GTEA) kilichopo Arusha.
“Makubaliano yaliyofikiwa ni kwamba, Serikali itanunua  hisa asilimia 26 zilizozokuwa zikimilikiwa na Continental AG ya Ujerumani katika kiwanda hicho kwa Dola za Marekani milioni moja na hivyo kuifanya imiliki kiwanda hicho kwa asilimia 100,” alisema Dk Kigoda.
Alisema baada ya hatua hiyo,  NDC, inatarajiwa kuanza ukarabati wa mitambo na kufanya majaribio ya uzalishaji wa matairi na wakati huo huo ikitafuta wabia wenye uzoefu wa uzalishaji wa matairi ya magari.
“Ufufuaji wa kiwanda hicho ni hatua nzuri katika kuongeza ajira kwa vijana wetu na hususan wale wa Jiji la Arusha,”alisema Dk Kigoda.
Akisoma taarifa ya Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara kuhusu bajeti ya wizara hiyo, Makamu Mwenyekiti, Dunstun Kitandula aliitaka Serikali kuongeza jitihada za kukifufua kiwanda hicho.
“Kwa kuwa kiwanda hiki kimekuwa na mgogoro wa muda mrefu, Serikali ifanye jitihada za makusudi kukamilisha utaratibu wa ununuzi wa hisa,”alisema

Michango ya wabunge
Wakichangia mjadala wa bajeti hizo mbili zilizopitishwa jana, Mbunge wa Chalinze (CCM), Ridhwani Kikwete alisema; “Maendeleo ya nchi hutegemea zaidi viwanda na hata China wameweza kufanikiwa kubadilisha uchumi wa watu wa hali ya chini kwa kufungua viwanda vidogo vinavyosaidia kusukuma mbele gurudumu la maendeleo na kutoa ajira.”
Alisema haoni kama kuna juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kuhakikisha nchi inakuwa na viwanda vya aina hiyo. “Vijana wanamaliza Veta (Vyuo vya ufundi), lakini hatuoni nguvu au mpango mkakati wa kuwasaidia waweze kujiajiri wenyewe. Wizara ingetueleza watawasaidiaje,” alisema.
Mbunge wa Solwa (CCM), Ahmed Salum aliitaka Serikali kupunguza urasimu katika utaratibu wa uwekezaji na uanzishwaji wa viwanda nchini. “Kukiwa na viwanda vingi nchini ndivyo tutakavyofanikiwa kukuza uchumi wetu na serikali itapata uwanja mpana wa kutoza kodi,” alisema.
Salum aliungwa mkono na mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Lucy Owenya aliyehoji sababu za viwanda kutelekezwa, huku akitaka kujua sababu za kutofufuliwa kwa kiwanda cha General Tyre cha jijini Arusha.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Esther Midimu aliitaka Wizara ya Mawasiliano kutoa ufafanuzi kuhusu ‘wizi’ unaofanywa na kampuni za simu. “Inakuwaje mtu unanunua muda wa maongezi au kifurushi cha mtandao cha mwezi mzima lakini kinakwisha ndani ya wiki tu?”
Alisema hata watumiaji wa mitandao hiyo ya simu hukatwa Sh400 kila mwezi kwa nyimbo ambazo hawakuomba, hali inayoashiria kuwa kuna wizi wa wazi unaofanywa na kampuni hizo.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: