Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga.
Kituo cha Televisheni cha ITV na Radio One kwa
kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani pamoja na
Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom, kimezindua kampeni ya kuhamasisha
kupunguza ajali za barabarani.
Kampeni hiyo ilizinduliwa jana katika Kituo Kikuu cha Mabasi
yaendayo mikoani cha Ubungo (UBT), jijini Dar es Salaam na kushirikisha
madereva na wadau mbalimbali. Tukio hilo lilikwenda sambamba na ubandikaji wa stika katika mabasi
ya mikoani lililofanywa na wafanyakazi wa ITV, Radio One na wa Vodacom
wakiongozwa na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa ITV Radio One, Mkurugenzi wa
Radio One, Deogratius Rweyunga, alisema kaulimbiu ya kampeni hiyo ni
`Zuia ajali sasa, toa taarifa mapema.' Rweyunga alifafanua kuwa kampeni
hiyo ni muhimu kwa kuwa inalenga kupunguza ajali za barabarani kwa
kiwango kikubwa.
Alisema pamoja na kwamba miundombinu inaweza kuwa sababu ya ajali
za barabarani, lakini pia ukiukwaji wa sheria za barabarani unaofanywa
na madereva umekuwa chanzo kikubwa cha ajali hizo. Alisema kupitia kampeni hiyo wanaamini itasaidia kupunguza ajali kama si kumaliza kabisa.
Aliongeza kuwa wanategemea zaidi ushiriki wa wananchi na abiria
wenyewe katika kutoa taarifa kwa kupiga simu namba 0800 757575 ambayo ni
bure, pale wanapoona madereva wanakiuka sheria za barabarani.
Rweyunga alisema dereva atakayeripotiwa kukiuka sheria za
barabarani atapigwa picha yeye na gari lake na kurushwa moja kwa moja na
vituo vya ITV Radio One pamoja na Capital Radio na kukamatwa mara
moja.
“Kampeni hii ni tofauti na nyingine zilizopita, hii itahusisha
abiria kwa asilimia 100, abiria atapaswa kutembea na namba hizo na
atapiga simu mara moja pale tu anapoona dereva anakiuka sheria za
barabarani, tunaomba ushirikiano katika hili,” alisema Rweyunga. Mkuu wa
Mawasiliano na Uhusiano wa Vodacom, Rosalynn Moria, alisema ni jukumu
la kila Mtanzania kuhakikisha kuwa anachangia katika kupunguza ajali
nchini.
Moria alisema wamejizatiti kuunga mkono jitihada za kupunguza ajali
nchini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Kwa upande wake, Kamanda
Mpinga alizishukuru kampuni hizo kwa mchango wake na kuviomba vyombo
vingine vya habari pamoja na kampuni mbalimbali za simu kuunga mkono
jitihada hizo. Alisema anaamini kupitia kampeni hiyo, ajali za
barabarani zitapungua kwa kiwango kikubwa na kuwaomba wananachi kutoa
ushirikiano kufanikisha kampeni hiyo.
Aliongeza kuwa matukio ya ajali nchini yatapungua iwapo watumiaji
wa barabara hususani madereva, watazingatia kanuni za usalama barabarani
pamoja na wananchi kutoa taarifa za ukiukwaji wa kanuni na sheria za
barabarani.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment