Msemaji mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Cecilia Paresso.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imeikosoa serikali
kwa kukosa mikakati endelevu ya kukabaliana na tatizo la ukosefu wa
ajira nchini.
Aidha, Kambi hiyo imeilaumu serikali kwa kuwapa wananchi matumaini
yasiyo na matokeo chanya juu ya suala la utengenezaji wa ajira nchini na
hivyo kulifanya tatizo hilo kuwa wimbo uliozoeleka ndani ya masikio ya
Watanzania.
Akisoma hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ya Wizara ya
Kazi na Ajira, kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha
2015/2016, Msemaji mkuu wa kambi hiyo, Cecilia Paresso, alisema ni
jambo la aibu kwa nchi iliyojaliwa utajiri mkubwa wa maliasili na
rasilimali kukosa ajira.
“Serikali imeshindwa kuzianisha sera, sheria, mikakati na mipango
mbalimbali ambayo kwa pamoja ingeweza kutatua matatizo sugu ya ukosefu
wa ajira nchini,” alisema.
Alisema ni serikali ndiyo iliyoua falsafa ya kujitegemea ambayo Baba wa Taifa alipigania kwa ajili ya Watanzania wote. Alisema Serikali ya Ukawa itakapoingia madarakani imekusudia
kudhibiti na kuondoa changamoto hizo za ajira kwa kuhakikisha wananchi
wanatengenezewa ajira za kutosha na wanaishi na kufanyakazi kwa amani na
utulivu na kuondoa umaskini.
Paresso, alisema ni ukweli usiopingika kwamba “soko la ajira”
Tanzania limefurika wanaotafuta kazi, lakini si kweli kwamba watu wote
wanaotafuta wanasifa stahiki kwa kila kazi. Akizungumzia kuhusu ukuaji uchumi nchini, alisema kiwango cha
asilimia saba ya ukuaji hakiakisi maendeleo halisi ya watu kwenye kaya
zao.
“Hivi sasa maisha yako juu. Bei ya bidhaa na huduma mbalimbali za jamii, ziko juu. Kwa kifupi hali ya maisha ni ngumu,” alisema.
Aidha, alisema Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa tatizo kubwa la
viongozi wa serikali ni kuona kuwa “wizara inapaswa kufa kivyake” bila
kutambua na kuona pia jitihada zinazotakiwa kuchukuliwa ili kuwepo na
mfumo unaounganisha wizara, idara, wala za serikali, uongozi wa sekta
binafsi kufanya kwa umoja, utakaoweza kusaidia kujenga uwezo wa uelewa
wa jinsi gani ajira zinaweza kutengenezwa katika nchi.
Kuhusu kima cha chini cha mshahara, Kambi hiyo ilisema inashangaza
serikali kujigamba kuwa imepandisha kima cha chini cha mshahara kutoka
sh. 240,000 hadi Sh. 265,000.
MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII
Kambi hiyo ilisema katika kipindi cha miaka mitano imekuwa
ikishauri kuunganishwa kwa mifuko yote ya hifadhi ya jamii na kubaki
chini ya usimamizi wa Wizara ya Kazi na Ajira lengo likiwa ni
kuiraisishia Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi za Jamii katika
kutekeleza Sheria moja na kuunda vifungu sawa vya kisheria
vitakavyosimamia utekelezaji na uendeshaji wa mifuko hiyo.
Katika taarifa ya Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kuhusu
utekelezaji wa Bajeti ya wizara hiyo, Mjumbe wa Kamati hiyo, Dk. Maua
Daftari, akisoma bungeni, alisema Kamati hiyo inahoji kuhusu ushauri
ulitoa mwaka wa fedha 2014/2015 kuhusu uanzishwaji wa mfuko wa pensheni
kwa wazee, migogoro ya wafanyakazi, ukuzaji wa ajira kwa vijana,
ufuatiliaji wa masuala yanayohusu usalama na afya mahali pa kazi (OSHA)
na uanzishwaji wa idara/kurugenzi ya hifadhi ya jamii.
MGOGORO WA WAFANYAKAZI SEKTA YA MADINI
Kamati hiyo ilisema suala la migogoro ya muda mrefu katika sekta ya madini ni miongoni mwa migogoro inayoisumbua taifa.
MGOGORO WA WAFANYAKAZI WA MABASI YA ABIRIA
Ilisema katika kipindi cha mwezi Machi na Aprili, mwaka huu,
kumekuwa na migomo ya madereva wa mabasi ya abiria ambayo imeleta athari
kubwa kwa kusababisha kazi nyingi za uzalishaji kusimama. “Sababu ya migomo hii ni pamoja na madereva kutokuwa na mikataba ya
ajira, mpango wa serikali wa kuwataka madereva kwenda sule kila
wanapotaka kujaza maombi ya leseni mpya na madereva kulalamikia serikali
kushindwa kutatua kero zao za ajira,” alisema Dk. Maua.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment