Mwenyekiti wake, Jaji mstaafu Damian Lubuva.
Siku moja baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kutangaza ratiba ya mchakato wa uteuzi wa wagombea wake kwa ajili ya
uchaguzi mkuu wa mwaka huu, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imetangaza
rasmi ratiba ya Uchaguzi Mkuu.
Tume hiyo imetangaza uchaguzi huo utafanyika Oktoba 25, mwaka huu na kampeni zitaanza Agosti 22 hadi Oktoba 24, mwaka huu. Taarifa ya Tume iliyosainiwa na Mwenyekiti wake, Jaji mstaafu
Damian Lubuva, jana ilieleza kuwa uteuzi wa wagombea wa nafasi za
udiwani, ubunge na urais, utafanyika Agosti 21, mwaka huu.
Jaji Lubuva alisema Nec inawataarifu wananchi kwamba ratiba hiyo
imetolewa kutokana na mamlaka iliyopewa kupitia vifungu vya Sheria ya
Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343. Alitaja vifungu hivyo kuwa ni vya 35 B (1), (3) (a), 37(1) (a) na 46(1).
Akizungumza na NIPASHE kufafanua juu ya wagombea kuchukua fomu,
Jaji Lubuva alisema baada ya uteuzi, siku inayofuata Agosti 22, mwaka
huu, wagombea wataanza kuchukua fomu hizo. Kuhusiana na masuala ya pingamizi, Jaji Lubuva alisema mambo hayo
yote yatapaswa kufanyika ndani ya siku zisizozidi 90 kabla ya uchaguzi
mkuu.
“Sisi tumetangaza ili Watanzania wafahamu kitu gani kinaendelea,
lakini kuhusiana na uchukuaji wa fomu na pingamizi, kwa mujibu wa
sheria, hayo yote yanatakiwa kufanyika ndani ya siku zisizozidi 90 kabla
ya uchaguzi,” alisema Jaji Lubuva.
Nec imetangaza ratiba ya uchaguzi mkuu wakati wadau hususani vyama
vya siasa vikionyesha wasiwasi kwamba itakuwa vigumu kufanyika kutokana
na maandalizi duni hususani kasi ndogo ya uandikishaji wa wapigakura
katika daftari la kudumu la wapigakura kwa kutumia mfumo wa
kielektroniki wa Biometric Voters Registration (BVR).
Viongozi kadhaa wa upinzani wamekuwa wakisema kuwa sababu za Nec
kuahirisha kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa iliyopangwa kufanyika
Aprili 30, mwaka huu za kutokamilika kwa daftari la wapigakura ndizo
zitakazotumika kuahirisha uchaguzi mkuu wa Oktoba.
Hata hivyo, Nec imekuwa ikisisitiza kuwa uchaguzi mkuu
hautaahirishwa na kwamba itahakikisha daftari linakamilika mwishoni mwa
Julai, mwaka huu. Vyama vya siasa ambavyo vimeshatangaza na vingine kuanza mchakato
wa kupata wagombea katika uchaguzi mkuu wa Oktoba ni Chama cha Wananchi
(Cuf), Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) na NCCR-Mageuzi.
MBUNGE AIBUA UTATA BVR
Wakati Nec ikitangaza mchakato wa uchaguzi mkuu, Mbunge wa Mbeya
Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu Sugu, amewataka wananchi
wakatae kuondolewa kwa vifaa vya kuandikisha BVR kit kwenye vituo kabla
watu wote hawajaandikishwa.
Akichangia jana jioni mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya
Jamii, Jinsia na Watoto na Wizara ya Kazi na Ajira ya 2015/2016, alisema
siku saba zilizotolewa na Nec kuandikisha wananchi hazitoshi na kuna
uwezekano idadi kubwa wasiandikishwe.
Mbilinyi ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo, alisema kutokana na BVR kuonyesha udhaifu katika
kuandikisha wapiga kura, wamekubaliana na wananchi wa Mbeya kuwa hakuna
kuruhusu mashine za BVR kuondolewa kwenye vituo kabla ya wananchi wote
hawajaandikishwa.
“Nazungumza kama Waziri Kivuli wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, sisi Mbeya tumekubaliana wananchi wakomae, hakuna kuruhusu BVR
zitolewe hata baada ya siku saba kwisha na mikoa mingine muige mfano huo
hadi watu wote waandikishwe,” alisema.
Alisema bado kuna foleni kubwa ya wananchi mfano katika Jiji la
Mbeya ambao wanasubiri kuandikishwa na maeneo mengine wanalamika
kujipikia chakula wakiwa vituoni ili waandikishwe, lakini BVR zinachukua
muda mrefu kuandikisha mtu mmoja,” alisema.
“Serikali ya CCM mmechoka, mmewachosha hata wananchi, kazi yenu ni
kuwasema Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) kwa sababu ya kuungana,
mbona nyie mmeungana na ACT hatusemi, endeleeni kusema, lakini viongozi
wa Ukawa wanaendelea kuchapa kazi, Profesa Lipumba yupo Lindi, Dk. Slaa
yupo Kawe, CCM mwisho wenu ni Oktoba,” alisema.
Naye Mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema), David Silinde,
akizungumza na NIPASHE nje ya ukumbi wa Bunge alisema hali ni mbaya na
kwamba kuna idadi kubwa ya wananchi hawataandikishwa na siku saba
hazitoshi. Silinde alisema kutokana na hali hiyo, amejipanga kwenda kumuona
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kumweleza kwamba siku saba zilizotolewa na
Nec hazitoshi.
“Nilikuwa jimboni kwangu nimekuja leo hapa Dodoma, siku saba za
uandikishaji zimekwisha leo (jana) jimboni kwangu na bado watu wengi
hawajaandikishwa, tulipendekeza siku 14 serikali ikakataa, sasa matokeo
yake ni haya,” alisema.
Mbunge wa Mbarali (CCM), Dickson Kilufi, alisema alikuwa jimboni
kwake na kuwa wananchi wengi hawajaandikishwa na siku saba zimekwisha.
Kilufi alisema kutokana na hali ilivyo, serikali inabidi iweke
utaratibu mwingine utakaowezesha wananchi wote kuandikishwa, vinginevyo
wananchi watakosa haki ya kupiga kura kutokana na kutoandikishwa.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment