Rais Jakaya Kikwete amesema umoja wa Vijana wa Chama
Cha Mapinduzi (UVCCM) umegeuka jukwaa la watu wanaotaka kugombea urais
kwa kuwa makuwadi na mawakala wa kuhonga fedha vijana wenzao badala ya
kufanya mijadala ya kukijenga chama.
Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, alitoa kauli hiyo
jana wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Kwanza wa shirikisho la wanafunzi
wa vyuo vya elimu ya juu, mjini hapa. Alisema vijana wa chama hicho wanatakiwa kuwa wapiganaji,
wapambanaji na wanaharakati katika katika kukiimarisha chama kutokana na
hatma ya CCM ipo mikononi mwa vijana wake.
“Kupata wanachama vijana kitupa fursa ya mtazamo mpya wa
kimaendeleo kwa chama chetu na ninaamini kupitia shirikisho hili
tutakijenga na kukiimarisha chama…Maana kule umoja wa vijana bwana
umegeuka jukwaa la watu wanaotaka kugombea urais,” alisema Rais Kikwete.
Alisema badala ya umoja huo kukaa na kuzungumza mambo ya mstakabali
wa chama na Taifa, lakini viongozi wa vijana ndio wanachukua fedha kwa
wazee na kuwagawia vijana. “Vijana hamuwezi kugeuka makuwadi na mawakala wa kuhonga wenzenu,
ikiwa kwa namna hii watakuwa wametoka kabisa kwenye mstari maana katika
kikao cha NEC nilimuita Sixtus (Katibu wa UVCCM) na wenzake nikamwambia
huko mnakoenda siko, rudini huku…sisi tunategemea miaka 30 ijayo Rais
atoke miongoni mwenu ni lazima tufanye kazi ya kuwaandaa vijana ili wawe
viongozi wazuri,” alisema na kuongeza:
“Unaposema umoja wa vijana, utakuta viongozi wale wanasafirishwa
kwasindikiza wazee wanaotaka urais, haiwezekani nyie vijana mkahusishwa
na ugawaji rushwa, zamani enzi zetu hoja za vijana zilikuwa zina nguvu,
lakini sasa hivi hoja za vijana sio tishio tena kwa mtu yoyote.”
Alisema kwa sasa hawatoi hoja za kukijenga chama na kuwataka kurudi nyuma na kurudisha misingi ya uanzishwaji wa umoja huo. Rais Kikwete alisema anaamini shirikisho hilo litakipa uhai chama
kwa kutoa mawazo ya kujenga matumaini mbele ya safari kwa kutambua
mahitaji ya wananchi katika jamii na kuyasemea.
“Haiwezekani ukawa na viongozi wa vijana ambao wanafanyakazi ya
kugawa hela ya wazee kwa vijana wenzao, jambo ambalo halifai kwani umoja
huu hauwezi ukawa jukwaa la kampeni kwa wanaotafuta urais,” alisema
Rais Kikwete.
Akizungumzia kuhusiana na shirikisho hilo, Rais Kikwete alisema
jukumu lao kuu ni kutafutia chama wanachama, marafiki,na kuungwa mkono
na wanafunzi wa elimu ya juu na wanafunzi wengine na pia kuwa kiungo
muhimu kati ya CCM na wanafunzi hao.
Aidha, alisema shirikisho hilo linawajibu wa kuwa chombo cha
uwakilishi wa maslahi ya wanafunzi na kuwa wepesi kuyatambua mambo yenye
maslahi kwa wanafunzi na kuyasemea. “Muwe tumaini na kimbilio la wanafunzi kwa kutatua changamoto na
kuzisemea kwa chama na serikali badala ya kuacha mambo yakaharibika na
kuamsha migogoro, shirikisho hili ni tanuru la kupiga viongozi wa
baadaye ni lazima muwe na mipango mathubuti,” alisema.
Aliwataka kuchagua viongozi wazuri, waaminifu, waadilifu, wabunifu
na wachapa kazi katika shirikisho lao ambao watakuwa na uwezo wa kujenga
hoja. Hata hivyo, alisema wawe wepesi kukubaliana na matokeo ya uchaguzi
ambao wanaufanya katika shirikisho hilo kwani hata yeye mwaka 1995 kura
za urais hazikutosha, lakini hakukata tamaa.
“Chama kinasema jitokezeni kugombea, nasubiri hiyo Juni 3
watajitokeza wangapi, maana ninavyosikia ni wengi wapo zaidi ya 20
wanaotaka urais, lazima tushirikiane kujenga chama chetu na shirikisho,
mimi nilijaribu mwaka 1995 kugombea urais, lakini kura hazikutosha na
sikumnunia Mzee Mkapa,” alisema Rais Kikwete.
Akimkaribisha mgeni rasmi mlezi wa shirikisho hilo, January
Makamba, alisema shirikisho hilo lina matawi 137 katika mikoa mbalimbali
nchini na kuzitaja changamoto zinazowakabili vijana hao ni mikopo ya
wanafunzi, ushirikishwaji katika kampeni na suala la ajira na kumuomba
Rais Kikwete kuyatafutia ufumbuzi.
Shirikisho hilo pia litafanya uchaguzi wa ngazi mbalimbali za
uongozi ikiwamo nafasi ya uenyekiti, makamu mwenyekiti, wajumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec), katibu wa uchumi na fedha, katibu wa
siasa na uenezi na Katibu wa uhamasishaji.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment