Social Icons

Pages

Wednesday, May 27, 2015

UANDIKISHAJI BVR WAZUA HOFU RATIBA YA UCHAGUZI

Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR- Mageuzi), David Kafulila.
Wadau mbalimbali hususani vyama vya siasa wamesema ratiba ya uchaguzi mkuu iliyotangazwa juzi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) haitekelezeki ikiwa uandikishaji utaendelea kwa kusuasua na kuwanyima fursa wananchi wengi kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura (DKWK).Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR- Mageuzi), David Kafulila, alisema changamoto iliyopo ni uandikishaji kwenda sawa na ratiba iliyotolewa na kwamba inahitajika nguvu ya ziada kuhakikisha mchakato unafanikiwa.
“Ratiba haitekelezeki iwapo wengi watakosa fursa ya kujiandikisha katika DKWK, nguvu kubwa ielekezwe namna gani watu wataandikishwa wote, jimboni kwangu watu wanaamka saa nane usiku kwenda kupanga foleni haijulikani muda gani wataandikishwa, wameajiri watu dhaifu, mashine moja inaandikisha watu 50 kwa siku, kuna kila dalili za kushindwa kufanikisha,” alisema.
Kuhusu kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa, Kafulila alisema inavyoonekana kuna msimamo wa chini kwa chini wa serikali kwa kuwa wanajua kura hiyo haitawezekana kufanyika mwaka huu.
 
JOHN MNYIKA
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, alisema kutangazwa kwa ratiba hiyo ni ishara kuwa uchaguzi mkuu utafanyika na hilo limefanikiwa kutokana na shinikizo la viongozi wa kuu wa vyama vya siasa kushinikiza Nec itangaze ratiba.
“Kihistoria kipindi kama hiki katika chaguzi zilizopita ratiba inatolewa mapema, lakini safari hii kulikuwa na giza na dalili zilikuwa zinaonyesha kuna mipango ya kusogeza mbele uchaguzi,” alisema.
Alisema ratiba hiyo ni ishara kuwa kura ya maoni haitafanyika kabla ya uchaguzi mkuu wala haitafanyika pamoja na uchaguzi mkuu.
Mnyika alisema pamoja na ratiba hiyo, lakini kuna uwezekano wa kufika karibu na uchaguzi na Nec ikatoa sababu za maandalizi hafifu kama ilivyotokea kwenye kura ya maoni ambayo ilitangazwa kufanyika Aprili 30, mwaka huu, lakini ikasitishwa muda mfupi kabla ya terehe hiyo.
“Dalili haziashirii maandalizi yako sawa sawa, tume haijapewa fedha za kufanya uchaguzi, wametoa ratiba kutokana na shinikizo, kwa sasa tunaelekeza nguvu katika kushinikiza maandalizi ya kutosha,” alisema.
 
PROFESA BAREGU
Kwa upande wake, msomi aliyebobea katika taaluma ya sayansi ya siasa, Prof. Mwesiga Baregu, alisema ratiba inayopaswa kutoka kwa sasa ni kueleza uandikishaji wapiga kura kwa ngazi ya kijiji, mtaa, kata, wilaya na mkoa ili kurahisisha watu kupanga ratiba zao kwa ajili ya kujiandikisha.
“Kwa sasa kinachoonekana ni kuwa Nec imeshaona kura ya maoni katika muda uliopo haitawezekana na sijui kwa nini haitoi tamko ambalo limejaa, inatoa vipande vipande,” alisema.
 Prof. Baregu alisema hali hiyo inaonyesha kuwa uwezo wa Nec wa kukamilisha daftari haina uhakika nao, na kwamba kwa ratiba iliyotolewa sasa wameruka hatua muhimu ya kuweka wazi ratiba ya Daftari la Wapigakura ikiwa ni pamoja na uhakiki wa daftari ili watu wajiandae kisaikolojia.
“Inaonyesha Nec imefanya hivyo kuridhisha vyama vya upinzani, bado haijajibu suala la uandikishaji wa kijiji, kata na maeneo ili kila mtu ajipange kutekeleza wajibu wake wa kikatiba, ili mtu apange safari lini aondoke, ratiba ya jumla haiwezi kuwasaidia wananchi,” alisema Prof. Baregu na kuongeza:
“Bado staili ya kazi ya tume haijaeleweka kabisa, kidogo wanajitahidi kuridhisha kwa kutangaza ratiba ya uchaguzi ambao hauwezi kufanikiwa bila daftari, kura ya maoni imeahirishwa, lakini msimamo wa viongozi ulikuwa uko pale pale, lakini hadi sasa hawajawaomba radhi Watanzania.”
 
LUGOLE WA CUF
Afisa Uchaguzi wa Chama cha Wananchi (CUF), Abdulrahman Lugole, alisema ratiba hiyo haitelekezeki kwa kuwa uandikishaji wa wapiga kura haujafanyika kwa usahihi kwa kuwa maeneo ambayo uandikishaji umemalizika kuna wananchi wengi hawajaandikishwa.
“Mikoa ya Lindi, Mtwara, Iringa na Ruvuma undikishaji umefanyika ilimradi, mfano eneo la Nachingwea wananchi wameandikishwa bila kuchukuliwa alama za vidole, jambo ambalo linaonyesha kuwa siku ya kupiga kura itakuwa ngumu, hakuna utaratibu wa kutoa nafasi ya kutathmini uandikishaji kabla ya kwenda maeneo mengine,” alibainisha.
Lugone alisema mikoa ya Pwani na Tanga uandikishaji umepangwa kufanyika kipindi cha mfungo wa Ramadhani na kwa hali ya misururu mirefu ni wazi kuwa watu watakata tamaa na kuendeleza ibada.
“Tunachokiona ni kuburuza watu, Nec inalazimisha mambo kama ilivyofanya kwenye kura ya maoni, daftari halieleweki kwa sasa, inaonyesha hawakujipanga tangu mwanzoni kwa kuwa serikali haikuwa na nia ya kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika mwaka huu, kwa kuwa walijua Katiba inayopendekezwa itapitishwa na hivyo kutakuwa na kipindi cha mpito,” alisema.
 
KHAMIS WA ACT WAZALENDO
Msemaji wa Chama cha ACT Wazalendo, Abdallah Khamis, alisema ratiba ni ngumu kwa kuwa uandikishaji haujakamilika na haijulikani lini utakamilika, huku utekelezaji wa ratiba uchaguzi mkuu ukitegemea kukamilika kwa Daftari la Kudumu la Wapigakura.
 
MAELEZO YA JAJI LUBUVA
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Nec, Jaji Mstaafu Damian Lubuva, alisema ratiba hiyo imewekwa wazi ili wananchi wajue siku ya uchukuaji fomu, uteuzi, kampeni na tarehe ya uchaguzi mkuu.
“Ndani ya Nec kutakuwa na mambo mengine yanaendelea kama mchakato na mengine, tunawataka wadau wazingatie ratiba, muda wa kampeni ni siku 60 na usizidi siku 90,” alisema.
Kuhusu Kura ya maoni, alisema nguvu kubwa imeelekezwa katika uandikishaji wa wapiga kura na kwamba itaamuliwa na itatangazwa kwa kadri wanavyojiridhisha na uboreshaji wa daftari na wataangalia hali itakavyokuwa na kwamba kwa sasa watashauriana na ofisi ya Waziri Mkuu.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Nec juzi, uteuzi wa wagombea ni Agosti 21, Agosti 22 ni Kampeni, Oktoba 24 kufunga kampeni na Oktoba 25, mwaka huu ni uchaguzi mkuu. 

CHANZO: NIPASHE

No comments: