Mtoto wa Baba wa Taifa, Charles Makongoro Nyerere
amevunja ukimya juu ya uvumi ulioenea kwamba yeye ni miongoni mwa watu
wanaotarajiwa kuchukua fomu ya kugombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu ujao
kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kusema hata yeye anajisikia na
yuko tayari kiafya, kiakili na ana nguvu ya kulitumikia Taifa kwenye
nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa nchi.Hata hivyo, Makongoro alisema kuwa dhamira hiyo ataiweka wazi kwa
kuzungumza na wandishi wa habari siku mbili au tatu kabla ya tarehe
iliyopangwa na CCM ya kuanza kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa na chama
hicho kugombea nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi wa mwaka huu.
Makongoro aliyasema hayo juzi jijini Mbeya wakati akipokea kwa
niaba ya familia ya Baba wa Taifa, Tuzo ya Uongozi uliotukuka na
Uzalendo ambayo ilitolewa na viongozi wa dini za Kiislamu na Kikikristo
mkoani Mbeya kwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere kwa lengo
la kutambua mchango wake kwa Taifa la Tanzania.
Makongoro alilazimika kulisema hilo, baada ya watu mbalimbali
waliokuwa wakizungumzia wasifu wa Hayati Baba wa Taifa kila mara kugusia
uvumi unaomhusisha na kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.
“Kwa kuwa kuna maneno yanapita na mimi nimeyasikia, na kwa kuwa
nanyi mmenitaka niseme ninachoweza kuwaeleza hata mimi najisikia na niko
tayari kulitumikia taifa katika nafasi hiyo (urais), nimesikia CCM
wametangaza ratiba ya kuchukua fomu, hivyo ninachoweza kuwathibitishia
ni kwamba siku mbili au tatu kabla ya tarehe iliyopangwa na CCM kuanza
kuchukua fomu nitazungumza na waandishi wa habari kuelezea uamuzi wangu
juu ya suala hilo,” alisema Makongoro.
CCM tayari imetangaza ratiba na utaratibu kwa wale wanaotaka kuomba
kuteuliwa na chama hicho kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, na
tarehe ya kuanza kuchukua fomu za kugombea nafasi hizo itakuwa Juni 3,
mwaka huu.
Aidha, alisema wiki ya kwanza ya kuanza kuchukua fomu za kugombea
urais kupitia CCM, atakuwa mjini Dodoma kwa ajili ya ama kuwashuhudia
wale wanaochukua fomu hizo au yeye mwenyewe kuchukua fomu.
Kwa kauli hiyo, Ni dhahiri kwamba mtoto huyo wa Baba wa Taifa
ameingia rasmi kwenye orodha ya makada wa CCM walioonyesha nia ya kutaka
kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini anachelea tu
kukiuka kanuni na taratibu za Chama chake cha CCM kama atatangaza uamuzi
wake mapema.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment