Dk Emmanuel Makaidi
WASIFU
Umri: Miaka 74
Elimu: Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Howard, Marekani
Kazi: Mwenyekiti wa Chama cha NLD.
Historia yake
Dk Emmanuel Makaidi ni Mwenyekiti wa Taifa wa
Chama cha NLD na ni mhandisi aliyebobea. Alizaliwa Aprili 10, 1941 huko
wilayani Masasi mkoani Mtwara. Baba yake mzazi alikuwa ni katekista wa
Kanisa la Anglikana.
Alianza elimu katika Shule ya Msingi Namalenga
wilayani Masasi kati ya mwaka 1948 – 1952, mwaka 1953 – 1954 alisoma
katika Shule ya Kati (Middle school) iitwayo Luatala hukohuko Masasi.
Baadaye alijiunga na Shule ya Sekondari ya Chuo cha Mtakatifu Joseph na
kusoma kidato cha kwanza hadi cha nne kati ya mwaka 1953 hadi 1956.
Makaidi alisoma darasa la 13 na 14 (kidato cha
tano na sita) katika Shule ya Sekondari Luhule, Uganda kati ya mwaka
1957 – 1958. Alipelekwa Uganda si kwa sababu ya kipato cha baba yake, la
hasha, alisaidiwa na Askofu wa Anglikana baada ya kuona anafaulu
mitihani yake kwa alama za juu sana.
Makaidi aliendelea kufadhiliwa na askofu huyo
ambaye alimuunganisha na mashirika mengine na kumtafutia chuo Afrika ya
Kusini. Akapelekwa Chuo Kikuu cha Witwatersrand na kuhitimu Shahada ya
Uendeshaji na Usimamizi kati ya mwaka 1958 – 1960.
Baada ya kuhitimu vizuri pale Witts, aliendelea
kupata ufadhili wa masomo ya shahada ya uzamili, mara hii alielekea
Marekani na kusoma masuala ya Menejimenti na Utawala kwa ngazi ya
uzamili kati ya mwaka 1960 – 1962. Alisoma pia katika Chuo Kikuu cha
Howard kilichoko jijini Washington, Marekani.
Baada ya kurejea nchini akiwa mhitimu wa M.A,
Makaidi alianza kazi serikalini mwaka 1966 hadi mwaka 1973 akiwa
mchambuzi kazi mkuu, katika kitengo cha Utumishi.
Kati ya mwaka 1974 na 1975 (miaka miwili). Alirudi
tena Marekani na kusoma Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Sayansi ya
Siasa katika Chuo Kikuu cha Howard akipata kuwa karibu na mmoja wa
maprofesa nguli duniani, Wamba Dia Wamba. Makaidi ameniambia kuwa hata
tabia ya kuandika vitabu na kutunga mambo ya ubunifu, alifundishwa na
profesa huyu mahiri.
Aliporejea nchini kwa mara ya pili mwaka 1976
aliendelea na kazi yake pale Utumishi hadi mwaka 1985 alipopewa kazi
nyingine kubwa zaidi, akawa Mkurugenzi wa Miundo na Mishahara kwenye
kamati iliyokuwa inashughulikia mashirika ya umma nchini.
Wakati anaendelea na kazi utumishi, alipata fursa
nyingine ya kusomea stashahada ya Kuchakata Taarifa za Kielektoniki
katika Chuo Kikuu cha Trinity, Ireland. Alikwenda huko na kuhitimu mwaka
huohuo 1977.
Kabla hajafanya kazi katika kamati maalum ya
kusimamia mashirika ya umma akapandishwa cheo na kuwa Naibu Katibu Mkuu
Wizara ya Kazi na Ustawi wa Jamii na mwaka huohuo 1985 akafukuzwa kazi.
Kisa cha Makaidi kufukuzwa kazi serikalini, tena
akiwa na wadhifa huo ilikuwa ni kwa sababu ya kuandika kitabu cha
Kiingereza chenye jina “mwanasiasa mwenye roho ya shetani”. Serikali
ikamzonga vilivyo, ikamtuhumu kuwa kitabu kile kinamtukana Mwalimu
Julius Nyerere. Mwisho wa siku “kazi ikaota mbawa”.
Mbio za ubunge
Mbio za urais
Nguvu yake
Udhaifu wake
Nini kimemfanya apitishwe NLD?
Bahati nzuri, mwaka huohuo 1985 akaajiriwa na Shirika la Finwork
Directory kuwa Mkurugenzi Mtendaji, kazi aliyoifanya hadi mwaka 1991.
Kuanzia mwaka 1992 hadi hivi leo, Dk Makaidi
hajajishughulisha tena na kazi za serikalini wala mashirika binafsi.
Amejiajiri akiwa na kampuni kadhaa zilizoajiri Watanzania wa vipato vya
kawaida, lakini pia ameendelea kutoa ushauri wa kitaalamu kwa kampuni za
ndani na nje ya nchi huku akiongoza chama cha NLD akiwa Mwenyekiti. Dk Makaidi ni mwandishi mzuri wa vitabu, ameshaandika zaidi ya 10. Amemuoa Modesta Ponela na wana watoto wanane.
Mbio za ubunge
Dk Makaidi alijitosa katika mbio za ubunge kwa
mara ya kwanza mwaka 2010 katika Jimbo la Masasi, Mtwara akipambana na
Mariam Kasembe wa CCM (aliyeibuka mshindi wa jumla kwa asilimia 63.7) na
Clara Mwatuka wa CUF (aliyepata asilimia 15.2). Katika uchaguzi huo Dk
Makaidi alishika nafasi ya tatu kwa kupata kura 5,384 sawa na asilimia
11.7 ya kura zote zilizopigwa.
Januari 2014, Dk Makaidi alikuwa mmoja wa
Watanzania walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa wajumbe wa Bunge
Maalumu la Katiba ambalo liliendeleza mchakato wa kikatiba, ulioanzishwa
na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Mbio za urais
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Dk Makaidi
alipitishwa na chama chake, NLD, kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania. Ni mmoja wa wagombea waliofika katika maeneo kadhaa ya nchi
kuomba kura pamoja na kuwa chama chake hakikuwa na nguvu kubwa ya
kisiasa na hata uchumi. Kwenye uchaguzi ule ambao mshindi alikuwa
Kikwete, Dk Makaidi alipata asilimia 0.19 ya kura zote zilizopigwa na
kushika nafasi ya saba kati ya wagombea 10 waliokuwa wanashindana.
Katika mbio za urais za mwaka huu, NLD tayari
kimeshampitisha tena kuwa mgombea wake na kinasubiri tu ridhaa ya Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuona kama ndiye atakayepewa nafasi hiyo
au la.
Makubaliano ya ndani ya Ukawa ya namna ya kumpata
mgombea urais wake, hayajawekwa wazi hadi hivi sasa japokuwa vyama
vinavyounda umoja huo vinaweza kukiachia chama kimoja kiteue mgombea
urais au vinaweza kushindanisha wagombea wa vyama vyote na kumchukua
mmoja wa jumla ambaye anaweza tena kukabidhiwa kwa chama chake cha awali
ili agombee.
Sheria za Tanzania kwa sasa haziruhusu vyama
kuungana kabla ya uchaguzi na jambo hilo lina maana kuwa mgombea mmoja
atakayeteuliwa na umoja huo, atagombea kupitia katika chama chake
kilichosajiliwa na viongozi wa vyama vingine watakuwa na jukumu la
kuhamasisha wanachama wao wampigie kura mgombea wa chama hicho kwenye
uchaguzi.
Nguvu yake
Jambo la kwanza linalombeba Dk Makaidi ni elimu. Yeye ni mmoja
wa Watanzania wachache waliosoma na kufikia ngazi ya shahada ya uzamivu.
Amenijulisha kwamba amesoma kwa shida tangu alipokuwa kijana mdogo na
hata alipokuwa kazini, lakini aliweka juhudi kubwa. Elimu ya ngazi
aliyonayo ni bora kwa mtu anayetaka kuongoza nchi.
Lakini jambo la pili, yeye ni kati ya
wajasiriamali waliothubutu kuanzisha shughuli za kujiingizia kipato na
kuajiri Watanzania wengine huku akiendelea na kazi ya kuwatetea wananchi
kupitia siasa. Dhana ya ujasiriamali inakua duniani hivi sasa na mtu
yeyote mwenye uzoefu mkubwa na sekta ya soko huria, anafahamu matatizo
ya wananchi wa chini kwa karibu na sifa hii ina umuhimu wake katika
kuongoza Taifa lililojaa walalahoi na watu wa chini.
Tatu, Dk Makaidi hajawahi kuwa mwanachama wa Tanu
wala CCM. Ameniambia kuwa tangu zamani alikuwa anakiona chama
kinachoongoza dola kwa jicho baya, hakuamini kama siku moja kingelikuja
kulibadilisha Taifa hili na kwa hivyo aliweka msimamo wa kutojiunga
nacho. Anasema yeye ni mmoja wa Watanzania wachache ambao wanaweza
kujipiga kifuani hadharani na kutamba kuwa kwa umri wake hakuwahi kuwa
mwanachama wa CCM.
Lakini sifa na nguvu ya nne ya Dk Makaidi ni
msimamo. Kiongozi huyu ni mmoja wa wanasiasa wanaotoka kwenye vyama
vinavyokua au kujiimarisha, akiwa na msimamo thabiti katika masuala ya
msingi. Si mtu wa kuyumbishwa na fedha au ukuu, si mtu wa kutumika au
kutumiwa, anasimamia ajenda anazozijua na kuziamini.
Katika Bunge Maalumu la Katiba, Dk Makaidi ni
mmoja wa viongozi waliounda Ukawa walioamua kuondoka. Hakujali kupoteza
mamilioni ya fedha za posho, alishikilia msimamo na kuzitosa fedha.
Alisimamia misingi ya kusaka katiba bora aliyokuwa anaiamini na tokea
hapo amekuwa moja ya mihimili mikubwa ya Ukawa.
Ni wanasiasa au viongozi wangapi wa vyama visivyo
na wabunge kama yeye walioweza kuondoka Dodoma na kuacha posho kwa ajili
ya kupigania masilahi mapana ya Taifa? Ndiyo maana Makaidi anakuwa
mmoja wa Watanzania ambao wana vigezo na sifa za kuwa kiongozi mkubwa
zaidi.
Udhaifu wake
Moja ya jambo ninalolitizama kama udhaifu wa Dk
Makaidi ni kutoweza kukikuza chama chake kupata wabunge. NLD ni moja
kati ya vyama visivyo na wabunge na yeye ndiye mwenyekiti wake. Pamoja
na ile dhana kuwa vyama vyenye wabunge vina nguvu kubwa ya rasilimali
fedha na watu nyakati za uchaguzi, hiyo haiondoi ukweli kuwa hata
vyenyewe kuna wakati havikuwahi kuwa na wabunge lakini vilipambana hadi
kuanza kupata wabunge. Kutofanikiwa kukikuza chama chake kuwa katika
ngazi ya juu ya ushindani wa kisiasa, kunaweza kutafsiriwa kama
“kushindwa kupenya” vizingiti vya siasa za vyama kabla hajakabidhiwa
majukumu makubwa ya nchi.
Lakini pili, naona kama Dk Makaidi ana udhaifu
katika eneo la kutoa taarifa kwa umma na labda kupitia katika vyombo vya
habari. Hivi karibuni alipohojiwa na juu ya hatua ya chama kimoja
ambacho kinaunda Ukawa kuanza kura za maoni za ndani ilhali makubaliano
ambayo hayajakamilika, Dk Makaidi alitoa kauli zinazoashiria namna
ambavyo hakuwa anaridhishwa na hatua ile.
Kwa mtizamo wangu, yale ni masuala ambayo
angepaswa kuzungumza na viongozi wenzake wa Ukawa au kuwasiliana na
viongozi wa chama kile kilichoanza kura za maoni na kujua namna ya
kuwasiliana na waandishi. Moja ya mambo ambayo mkuu yeyote wa nchi
anapaswa kujifunza na kuyashikilia ni anatoa habari zipi, kwa nani, kwa
nini na zitaleta madhara gani. Japokuwa hili ni jambo la mtu kujifunza
zaidi, lakini kwa kiongozi ambaye anatajwa kuwa na sifa za kuwa rais, ni
upungufu mkubwa.
Nini kimemfanya apitishwe NLD?
Moja ya mambo yaliyofanya NLD impitishe kuwa
mgombea urais wake ambaye ataomba kibali cha Ukawa kupeperusha bendera
ya umoja huo ni kwa sababu ni mwanasiasa maarufu kuliko mwingine yeyote
ndani ya chama chake. Ningeshangaa kama NLD wangefikiria kumpeleka
mwanachama mwingine ambaye hana uzoefu wa kisiasa au asiyefahamika kama
ilivyo Dk Makaidi.
Nini kinaweza kumwangusha?
Asipopitishwa (Mpango B)
Lakini pili, nadhani amepitishwa kwa sababu ya uzoefu wake
katika kufanya kazi serikalini. Amekuwa mtumishi wa Serikali kwa zaidi
ya miongo mitatu. Huu ni muda mrefu katika shughuli za utumishi wa umma.
Lakini pia amekuwa mfanyakazi wa ngazi ya juu katika sekta binafsi na
hivyo anajua changamoto za ndani ya Serikali na katika sekta binafsi.
Tatu, naona amepitishwa kwa sababu yeye ni mmoja
wa waasisi wa Ukawa. Isingekuwa jambo la busara kwa chama chake
kumpitisha mgombea ambaye hafahamu vizuri misingi ya uanzishwaji wa
umoja huo, malengo na dira yake kwani ingekuwa kazi rahisi kuangushwa na
wagombea wengine wenye wasifu mkubwa kumshinda. Faida ya kufahamu Ukawa
ni muhimu kwa ajili ya kulinda masilahi ya chama kinachokua kama NLD.
Nini kinaweza kumwangusha?
Mambo mawili makubwa yanaweza kumwangusha katika mchujo wa ndani ya Ukawa, maana ameshapita ule wa ndani ya chama chake.
Moja ni ikiwa umoja huo utaamua moja kwa moja kuwa
nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia umoja huo
igombewe na moja ya chama kinachounda umoja huo na kisicho NLD,
‘automatically’ atakuwa amekosa fursa hiyo muhimu.
Lakini jambo la pili linaloweza kumwangusha kwenye
mchujo ni ikiwa wagombea wa Ukawa watapambanishwa bila kuangaliwa
wanatoka chama gani. Huenda jambo hili likamwangusha kwa sababu ndani ya
Ukawa kuna viongozi wenye sifa nyingi zaidi, uzoefu mkubwa zaidi wa
kitaifa na kimataifa na wakiwa miongoni mwa Watanzania mashuhuri
kumpita.
Mwisho, jambo linaloweza kumkwamisha, ni ikiwa
mgombea wa Ukawa atapaswa kutoka Zanzibar. Kwa sababu yeye ni Mtanzania
mwenye asili ya Bara, hii ni sababu isiyo na majadiliano na inaweza pia
kukiathiri chama chake kwa sababu hata huko Zanzibar nimeambiwa kina
wanachama wa kawaida wasio na sifa kubwa kama za kwake.
Asipopitishwa (Mpango B)
Dk Makaidi atakuwa na mipango kama minne ikiwa hatapitishwa kugombea urais kupitia Ukawa:
Jambo la kwanza atakalofanya linaweza kuwa ni
kugombea ubunge katika Jimbo la Masasi ambalo aligombea mwaka 2010. Dk
Makaidi ni mwanasiasa mwenye uwezo mkubwa na tuliona uthubutu wake,
uwezo wa kujenga hoja na kufanya utafiti kama alivyouonyesha katiba
Bunge Maalumu la Katiba, naamini akiwa mbunge anaweza kuwa na mchango
mkubwa zaidi kwa Taifa.
Lakini jambo la pili, kwa sababu kiongozi huyu ni
mjasiriamali wa muda mrefu na mtu mwenye uzoefu na sekta ya umma na ile
binafsi, anaweza kuendelea na ujasiriamali wa juu zaidi akiajiri vijana
wa Kitanzania wengi zaidi kwa kuangalia mahitaji ya sekta ya umma na
wananchi kwa ujumla na kuona namna wanavyoweza kupata huduma za ubunifu.
Jambo la tatu analoweza kufanya ni kutoa ushauri
na kufundisha. Kwa sababu ana shahada ya uzamivu, natambua kuwa kuna
vyuo vingi vipya vimeanzishwa hivi karibuni lakini vikiwa havina walimu
wa kutosha. Kama anafikia vigezo, anaweza kuungana navyo na kuendelea
kuwasaidia vijana kitaaluma. Lakini kwa kuunganisha, anaweza pia
kuendelea na kazi za kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wajasiriamali
wanaokua na wale wanaojifunza, bila kusahau kampuni za ndani na nje.
Hitimisho
Hitimisho
Rais wa Afrika ya Kusini, Jacob Zuma hana hata
shahada moja ya chuo kikuu na elimu yake haieleweki hadi leo, uzoefu wa
kisiasa peke yake umemtosha kuongoza Taifa kubwa kabisa Afrika. Dk
Makaidi ana uzoefu wa kisiasa ndani ya nchi na ni msomi, naamini anao
uwezo mkubwa lakini itampasa azidi kujipanga hata akikosa tiketi ya
urais kwa Ukawa.
Lakini pia, chama chake kimepata fursa muhimu ya
kuwamo katika muungano wa vyama vya siasa vitatu vyenye wabunge na
ambavyo unaweza kusema ndivyo vyenye nguvu hapa Tanzania, ukiachilia
mbali CCM. Kuwamo kwenye muungano na vyama hivi ni fursa pekee kwake
kisiasa, lakini pia kwa chama chake.
Ni matumaini yangu kuwa baada ya Uchaguzi Mkuu, Dk
Makaidi atakuwa mwanasiasa mwenye taswira ya juu zaidi, lakini pia
chama chake walau kitakuwa na wawakilishi huku na kule.
Binafsi nampongeza kwa kuendelea kuwa mwana
mabadiliko lakini zaidi ya yote kwa safari yake ya kisiasa ambayo
naamini bado haijafika mwisho.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment