Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki.
Kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) ya Mkoa wa Dar es
Salaam, imekubali mapendekezo ya kuongeza majimbo ya uchaguzi katika
mkoa huo kutoka saba ya awali hadi kufikia 13.Kikao kilichofikia makubaliano hayo kilifikiwa licha ya mvutano
kutoka kwa wabunge wa upinzani ambao walipinga mapendekezo ya
kuongezeka kwa majimbo hayo. Kwa upande wa Halmsahuri ya Temeke, majimbo mapya yaliyopendekezwa
kuongezeka ni Mbagala, na Kijichi na kufikia jumla ya majimbo manne kwa
kujumuisha majimbo ya sasa ya Kigamboni na Temeke.
Akifungua kikao hicho Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck
Sadiki, (pichani), alisema wamefanya mapendekezo hayo ili kuwasilisha
kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ambayo ratiba yake inataka mwisho wa
kuwasilisha mapendekezo hayo kuwa Mei 31, mwaka huu.
Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, Halmashauri ya Kinondoni majimbo
mapya yaliyopendekezwa kuongezeka ni Kibamba na Bunju na hivyo kufikia
majimbo matano ukiongeza na ya zamani ya Ubungo, Kawe na Kinondoni.
Katika Halmashauri ya Ilala, jimbo moja ndilo lilipendekezwa
kuongezeka na kufikia jumla ya majimbo manne pamoja na ya zamani ya
Segerea, Ilala na Ukonga.
Pamoja na Kamati kukubali mapendekezo hayo, Wabunge wa Upinzani
hawakukubaliana na maamuzi hayo na kusema kwamba wanapanga kupeleka
maombi mbadala kwa Nec ya kutokubaliana na utaratibu huo ndani ya mwezi
huu.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alitoa wito kwa Watanzania na wadau
wengine wasiokubaliana na utaratibu huo wa kuongeza majimbo, kupeleka
mapendekezo yao mbadala kwa Tume ili wakati inafanya maamuzi ifanye kwa
kuzingatia matakwa ya Watanzania.
“Sioni sababu ya kuongeza majimbo kwa kuwa kama Serikali ingekuwa
na nia ya kuleta maendeleo ingeongeza Halmashauri na si majimbo,
wanataka kutumia mwanya wa kuongeza majimbo ili kutatua mgogoro uliopo
ndani ya Chama Cha Mapindizi (CCM) wa kugombania majimbo kwa hiyo
wanajua wakiongeza kila mmoja atakuwa amepata,” alisema Mnyika na
kuongeza:
“Watu walikuwa wanakataa muundo wa serikali tatu kwa sababu ya
gharama, lakini eti hivi sasa wanataka tena kuongeza majimbo ambayo
yataongeza gharama kubwa zaidi, haya ni mambo ya ajabu sana.”
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, alisema ni vema tume ikagawa majimbo
hayo kwa kuzingatia kama upo uwezo wa kuyamudu majimbo hayo na sio
kuangalia tu wingi wa watu na kuanza kugawa bila kutafakari na kupima
uwezo wake.
Kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa mwaka
huu, Mbagala itakuwa na kata 10, watu 738,504, Kigamboni Kata 9, watu
375, 881, Temeke Kata 7, watu 346, 425 na Kijichi kata 6, watu
362,146.
Ubungo itakuwa na kata 7, watu 454,536, Kibamba kata tano, watu 343,
876, Bunju kata sita, watu 332, 576, Kawe kata nane, watu 443, 729 na
Kinondoni Kata nane, watu 342, 138, Ilala ina Kata 10, watu 157,315,
Segerea kata 13, watu 657,634 na Ukonga kata 12, watu 503, 175.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment