Mratibu wa Ulingo, Dk. Ave Maria Semakafu.
Asasi ya Kiraia yenye wanachama wanawake kutoka
vyama vya siasa (Ulingo) kwa kushirikiana na asasi kadhaa, wameandaa
mafunzo kwa wanawake watangaza nia na wagombea wa nafasi za uongozi
tofauti katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu.
Asasi hizo ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Mtandao
wa Jinsia Tanzania(TGNP) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake
Tanzania (Tamwa) Zanzibar. Mafunzo hayo yatatolewa nchi nzima kwa zaidi ya wanawake 2,300
watakowania na kugombea nafasi za udiwani, ubunge na urais, yatakuwa
katika awamu mbili, ya kwanza itaanza Juni Mosi hadi 5 na awamu ya pili
ni Juni 22 hadi Juni 27, mwaka huu.
Baada ya hapo watawapa sapoti wanawake watakaojitokeza kugombea. Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mratibu wa Ulingo, Dk.
Ave Maria Semakafu, (pichani) wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwahamasisha, kuwajengea uwezo,
kuwatia moyo na ujasiri wanawake hao, ili waweze kujiandaa na
kukabiliana na hali ya unyanyapaa na ukandamizaji kutoka katika vyama
ambavyo havina demokrasia.
Alisema ulingo ilifanya utafiti baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka
2010 na kugundua kwamba watangaza nia na wagombea wanawake wamekuwa
wakikatishwa tamaa na kunyanyapaliwa na vyama na kupewa kauli ya
kutouzika.
Miongoni mwa mambo waliyoyapitia ni Sheria ya Vyama vya Siasa ya
mwaka 1992, katiba za vyama vya siasa na mifumo ya uteuzi wa wagombea
wa viti maalum katika vyama vya siasa.
”Aprili mwaka huu Ulingo tulianza uratibu wa kuandikisha wanawake
watangaze nia watakaowania nafasi za udiwani, ubunge na urais. Mwaka
2010 tuligundua unyanyapaaji mkubwa dhidi ya wanawake ambao walikuwa
wanakubalika na wananchi, lakini vyama vya siasa kwa kukosa demokrasia
waliwaondoa kwa madai hawauziki,” alisema Dk. Semakafu.
Alisema demokrasia katika vyama vya siasa kuanzia ngazi ya chini
hadi Taifa haipo na kusababisha wanawake kuathirika na mfumo dume,
kitendo kinachosababisha jamii kukosa viongozi wanaokubalika na wenye
vigezo.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment