Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya
Habari Tanzania (MOAT), Dk. Reginald Mengi (wa pili kushoto) akizungumza
katika mkutano wa wamiliki wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam
jana juu ya Muswada wa Vyombo vya Habari. Wengine ni wajumbe wa MOAT,
Rostam Aziz wa New Habari 2006 Ltd (kushoto), Wakili wa Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu, Godfrey Mpandimizi (wa pili kulia) na
Samuel Nyalla kutoka Sahara Media Group.Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania kupitia
chombo chao cha Moat wameunda kamati maalumu itakayokutana na ya Bunge
ya Huduma za Jamii kushinikiza miswada miwili ya habari isijadiliwe
kwenye Bunge la Bajeti linaloendelea mjini Dodoma.
Miswada hiyo ni wa Haki ya Kupata Taarifa na ule wa Huduma za
Vyombo vya Habari, ambayo pamoja na mambo mengine inapendekeza kiwango
cha elimu kwa mwanahabari kiwe kuanzia shahada. Inapendekeza pia adhabu ya kifungo cha miaka mitano jela kwa yeyote
atakayekiuka sheria ya tasnia hiyo, huku vyombo vya habari vya binafsi
vikitakiwa kujiunga na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) saa 2: 00.
usiku kila siku kwa ajili ya taarifa ya habari.
Moat walifikia maamuzi hayo katika mkutano wao uliofanyika jana
jijini Dar es Salaam, baada ya kuitathmini miswada hiyo na namna
itakavyominya uhuru wa vyombo vya habari na wananchi katika kutoa na
kupata habari kutoka vyanzo tofauti iwapo itapitishwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited (MCL),
Francis Nanai, alisema kamati hiyo yenye wajumbe watatu itaenda kukutana
na kamati ya bunge kuishauri miswada hiyo isiingizwe bungeni kujadiliwa
kutokana na upungufu huo.
Alitaka maprofesa, wanasheria wakiwamo mahakimu na mawakili kuijadili miswada hiyo kwanza. Mwenyekiti wa Moat, Dk. Reginald Mengi, alisema miswada hiyo inaua
ndoto ya vijana, tasnia ya habari na kwenda kinyume cha katiba ambayo
inaeleza haki ya kila Mtanzania kupata taarifa.
Aliitaka serikali kutokuwa sehemu ya kuvunja katiba ya nchi kwa
kupitisha miswada hiyo ambayo vipengele vyake vinalenga kuangamiza
tasnia hiyo nchini. Alisema vyombo vya habari ndivyo vilivyoipaisha Tanzania hadi
kujiunga na Mpango wa Kuongoza Serikali kwa Uwazi na Uwajibikaji (OGP).
“Nchi yetu imejipatia sifa nyingi kupitia vyombo vya habari ndiyo
maana ipo hata katika OGP, hii ni kupitia vyombo vya habari. Sisi
tunaheshimu haki ya wananchi kupata habari,” alisema Dk. Mengi. Aliongeza: “Muswada huu hauwezekani, ni mbovu, utatupa matatizo
kipindi cha uchaguzi. Huwezi kuwa na uchaguzi huru ikiwa wananchi
watakosa habari. Hakuna amani bila uhuru na haki. Amani ni hazina ya
nchi yetu, kundi fulani lisitupore amani yetu. Serikali na vyombo vya
habari vishirikiane.”
Alishangazwa na wanasiasa kwani vyombo vya habari ndivyo
vilivyowawezesha wakati wakisaka madaraka lakini baada ya kufanikiwa
wamesahau walikotoka.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hali Halisi Publishers Ltd, Saed Kubenea,
alisema miswada hiyo haipaswi kujadiliwa bungeni wakati huu bali isubiri
Rais ajaye kutokana na jinsi inavyokinzana na katiba, ibara ya 18
inayoeleza haki ya raia kutoa maoni na kupata taarifa.
Alisema baada ya waandishi kutendewa ubaya kama vile kung’olewa
meno na kucha, kinachofuatia sasa kinalenga kuwapeleka gerezani kwa
kuletwa kwa miswada hiyo.
Mkurugenzi wa kituo cha redio cha Sport FM cha Dodoma, Abdallah
Majura, alisema Moat wameukataa muswada huo kwamba haufai na kuhoji
iwapo kutakuwapo na mgawanyo wa mapato pindi vyombo vingine vya habari
vikitakiwa kujiunga na TBC wakati wa taarifa ya habari.
Miswada hiyo pia inakataza mtu kumiliki vyombo vingi vya habari na
faini ya Sh. milioni 20 au kifungo kisichopungua miaka mitano au adhabu
zote mbili kwa pamoja kwa mshitakiwa atakayethibitishwa na mahakama
kutenda kosa.
Pia bodi ya kusajili na kumfuta mwandishi wa habari itakuwa na
uwezo wa kumsimamisha mwanahabari asifanye kazi yake tena, hivyo
kutengeneza mpenyo wa kuwashughulikia waandishi wanaoikosoa serikali.
Akifungua mkutano wa OGP, jijini Dar es Salaam, wiki iliyopita,
Rais Jakaya Kikwete aliahidi kuisaini miswada hiyo kwa imani kwamba,
wabunge wataijadili vyema ili aisaini kabla ya kumalizika kwa Bunge hilo
na kuondoka kwake madarakani.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment