Rais Jakaya Kikwete jana aliwaaga mabalozi wa
Tanzania nchi za nje, huku akiwaeleza kuwa viashiria vya matukio ya
ugaidi, ambayo yamekwishasababisha baadhi ya watu kuuawa na wengine
kujeruhiwa katika maeneo tofauti ya Tanzania Bara na Zanzibar,
vinaviweka vyombo vya ulinzi na usalama katika tahadhari wakati wote
nchini.
Alisema hayo wakati akifungua mkutano wa siku tatu wa mabalozi hao,
wenye kaulimbiu: “Diplomasia ya Tanzania kuelekea Dira ya Taifa 2025”,
jijini Dar es Salaam jana. Alisema tayari Tanzania imekwishakuwa muathirika wa ugaidi na
kwamba, viashiria vya tatizo hilo ni baadhi ya matukio yaliyokwishatokea
na kusababisha athari kubwa kwa watu nchini.
Baadhi ya matukio hayo aliyataja kuwa ni pamoja na lile la milipuko
ya mabomu katika Ubalozi wa Marekani, jijini Dar es Salaam Agosti 7,
1998, ambalo liliua watu 11 na wengine 85 kujeruhiwa na la mlipuko wa
bomu uliotokea katika Parokia ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi Olasiti,
jijini Arusha, Mei 5, mwaka juzi na kuua watu watatu na wengine kadhaa
kujeruhiwa.
Aliyataja matukio mengine kuwa ni ya bomu lililorushwa katika
mkutano wa Chadema wa kuhitimisha kampeni za uchaguzi za udiwani wa kata
nne za Jimbo la Arusha Mjini Juni, 15, mwaka juzi, lililoua watu watatu
na wengine zaidi ya 70 kujeruhiwa.
“Matukio ya ugaidi yanaviweka vyombo vya ulinzi na usalama katika
tahadhari wakati wote, maana hujui litatokea wakati gani. Sasa lipo
vuguvugu nchini. Lakini pia kuna uhusiano na mitandao ya kigaidi
duniani, hivyo na sisi tuko kwenye matishio,” alisema Rais Kikwete.
Aliwataka mabalozi kuendelea kutengeneza marafiki duniani na
kuangalia namna watakavyokabiliana na changamoto za utandawazi na
kuwasaidia Watanzania wanaowekeza nje ya nchi.
Pia aliwataka mabalozi kuleta habari nchini zenye tija kwa sababu
nafasi waliyonayo ni muhimu na kuwataka watambue kuwa Watanzania
wanategemea namna gani wanashiriki kwenye vituo vyao vya kazi kupanua
fursa za kiuchumi nchini.
“Nimeingia nchi ikiwa haina maadui na nafurahi naondoka nchi yetu
ikiwa haina maadui,” alisema Rais Kikwete kabla ya kuwaaga mabalozi hao
kwa kuwaambia. “Huu ni mkutano wangu wa mwisho…Mimi ndio namaliza hivi.”
Pia aliwataka mabalozi kushiriki katika jitihada za kuzishawishi
nchi za China na Marekani zifikie makubaliano kwenye mkutano
unaotarajiwa kufanyika jijini Paris, nchini Ufaransa, ya kupunguza
umwagaji wa hewa ukaa kuepusha hatari ya uharibifu wa mazingira.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment