Nyota ya Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa
Monduli (CCM), Edward Lowassa, imeendelea kung’aa baada ya Taasisi ya
Samunge Social Sciences Research Center (SSSRC), kufanya utafiti na
kubaini kuwa kiongozi huyo ni chaguo la kwanza kwa wananchi.Utafiti huo uliofanywa miaka miwili kuanzia 2013 hadi 2015,
unaonyesha Lowassa anaongoza kwa asilimia 20.7 dhidi ya wagombea 31. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,
Mtafiti Mkuu wa SSSRC, George Nyaronga, alisema utafiti huo waliufanya
kwa kutumia madodoso pamoja na mahojiano kwenye mikoa 18.
Utafiti huo na asilimia walizopata wanasiasa wengine kwenye mabano
ni Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema, Dk.
Willbrod Slaa asilimia 11.7; Waziri wa Ujenzi, John Magufuli (7.6);
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe (7);
Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January
Makamba (4.8); Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim
Lipumba (4.2) na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe 3.4 sawa na
Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (2.4) na Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia (1.2). Alisema pia utafiti huo ulionyesha kuwa Lowassa pekee ndiye
anayekubalika na wapiga kura wengi, karibia idadi sawa ya jinsia zote
mbili, wanaume 50 na wanawake 49.
Kwa ujumla, Lowassa na vinara wengine 10 wanaotajwa kuwania urais
walipata asilimia 67.2, huku asilimia zilizobaki (32.8) zikitwaliwa na
wagombea wengine 10 kati ya 20 waliohusishwa katika utafiti huo. Aidha, Nyaronga alisema hawakuwa na dodoso linaloorodhesha majina
ya wanaopendekezwa kuwa Rais ila majina yalitajwa na wajaza madodoso
wenyewe kisha wao wakajaza majina kwenye SSSRC.
Kwa mujibu wa dodoso lenye kichwa cha habari cha katika tafiti
kuhusu uchaguzi wa mwaka 2015, takwimu zinaonyesha kuwa Watanzania
wanamtaka mtu mwenye kufanya maamuzi magumu. Alisema kwa maoni ya wengi waliohojiwa na kujaza dodoso,
wanaonyesha kuwa Lowassa anakubalika zaidi na kwamba ulifanywa katika
mikoa 18 ya Bara na Visiwani, watu 1,000 walijaza dodoso na 6,000
walifanyawa mahojiano. Alisema utafiti huo uliofanywa kwenye mikoa ya Dar es Salaam,
Zanzibar, Morogoro, Singida, Shinyanga, Mwanza, Mara, Mbeya, Katavi,
Kigoma, Tabora, Arusha, Moshi, Iringa, Njombe, Songea, Lindi na Mtwara.
Nyaronga alisema baadhi ya mambo ambayo tafiti hiyo ilikuwa
ikitafuta majibu ni masuala yanayohusu changamoto kwa Tanzania kwa sasa,
sifa za kiongozi anayehitajika kukabiliana na changamoto hizo,
mapendekezo ya jina la Rais atakayesimamia vizuri changamoto hizo, chama
chenye uwezo wa kutupatia rais ajaye kwa mujibu wa katiba ya mwaka 1977
na kama Watanzania watapiga kura.
VYAMA VYA SIASA
Alisema utafiti huo umebaini CCM ina asilimia 53.5 ya kutoa Rais , Chadema yenye asilimia 34.2. Alisema vijana wa miaka kati ya 18-25 ambao ni sawa na asilimia 46
wanamtaka Lowassa kuwa Rais, ikifuatiwa na vijana wa miaka 26-30, na
vijana wa kati ya miaka 30-35.
Aliongeza kuwa CCM kina wanachama wengi wenye umri mdogo
ikilinganishwa na vyama vingine vya siasa Tanzania na Chadema ndicho
kinachofuatia kwa kupendwa na umri wa miaka kati ya 18 -25. Mtafiti huyo alisema CCM inapendwa zaidi na watu wenye aina
mbalimbali za elimu kuanzia shahada ina watu 144, sekondari ina watu 84
na hata katika elimu ya msingi ina watu 18, ikifuatiwa na Chadema.
Alizitaja changamoto kuu 16 zilizopo Tanzania kwa sasa kama
zilivyoorodheshwa na wananchi ambapo wanamtaka Rais ajaye azishugulikie
ni elimu, afya, viwanda, ajira, kilimo, miundombinu hafifu, kukosekana
kwa utawala bora, uchumi hafifu, nishati, migogoro ya ardhi, mikataba
mibovu.
Nyingine ni ukwepaji kodi, rushwa, ufisadi, ubinafsi na kutokuwa na uzalendo. “Katika tafiti hii tumegundua kuwa Lowassa anaongoza katika kila
nyanja kama Rais pendekezwa kuwa Rais wa Tanzania 2015, ukiangalia
jinsia zote wa kiume na wa kike wanamtaka Lowassa kuwa Rais,” alifafanua
na kuongeza:
“Tafiti hii inaipa chama dira na mwelekeo wa kujua kwamba ni
Mtanzania gani ndani ya chama anayehitajika na Watanzania, chama
kikishajua hilo hakifanyi kosa kumwacha mtu huyo anayehitajika na
Watanzania ili kwanza kukiokoa chama kupoteza dola lakini pia kukilinda
kiweze kubaki madarakani.”
Aliasema chama mbadala wa CCM ni Chadema, takwimu zinaonyesha kuwa,
iwapo Lowassa hatapeperusha bendera ya CCM 2015, basi anayetakwa na
wananchi kuwa Rais mbadala ni Dk. Willibrod Slaa. Alisema Machi 2015, taasisi isiyo ya kiserikali ya Positive
Thinkers Tanzania ripoti yake ya utafiti ilioji watu 3,298 na Lowassa
alipata watu 752 katika mikoa 13 Tanzania Bara na Mwenyekiti wa Taasisi
hiyo,Tibatizibwa Yabutinga, alielezea kuwa Lowassa ni mwanasiasa
anayekubalika sana kuwa rais ajaye 2015.
Alisema katika ripoti hiyo ili orodhesha matokeo yake kuwa Lowassa
alipata asilimia 22.8, Slaa 19.5 asilimia , Nchemba 10.6, Profesa
Lipumba 8.9, John Magufuli 6.8 , Kabwe 6.7, Membe 5.9, Pinda 3.2 ,
makamba 1.6, Mwandosya 1.2.
Alisema Twaweza sauti za Wananchi, Nov.2014 Imegundua kuwa katika
watu 1,445 walioshiriki utafiti ni kuwa wengi wao walisema kuwa
changamoto kuu ni Uchumi, elimu na afya na wanasiasa wengi hawatimizi
ahadi zao.
Twaweza pia wametoa tafiti kuwa CCM bado kinapendwa na Watanzania
kwa asilimia 51 kwa nafasi ya urais, asilimia 46 kwa nafasi ya ubunge na
kwa asilimia 47 kwa nafasi za udiwani ikifuatiwa na Chadema.
Alisema ripoti hiyo ya Twaweza pia inatoa ripoti kuwa vijana chini
ya miaka 34, watu chini ya miaka 50 na wazee zaidi ya miaka 50 kwa
pamoja wengi wana sapoti kubwa kwa chama cha mapinduzi, na katika nafasi
ya urais 2015, ripoti ya Twaweza inasema kuwa ndani ya CCM, kura za
wagombea urais kwa tiketi ya CCM ni Lowassa anaongoza kwa asilimia 17,
Pinda asilimia 14, Magufuli asilimia tano, Samuel Sitta asilimia tano,
Membe asilimia saba.
Alisema ripoti hiyo ya Twaweza pia iliweka wazi kuwa iwapo uchaguzi
utafanywa , basi CCM itaongoza kwa asilimia 47, Ukawa kwa asilimia 28 na
kama mtu atasimama binafsi, basi atapata asilimia 19.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment