Maduka ya Kariakoo, Dar es Salaam yakiwa yamefungwa jana ikiwa ni
mwendelezo wa mgomo wa wafanyabiashara katika maeneo mbalimbali nchini.
Kamati ya
Maadili ya Amani na Haki za Binadamu ya madhehebu ya dini nchini
imemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuzungumza na wafanyabiashara na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kutatua mgogoro uliopo baina yao.
Kauli hiyo imekuja baada ya wafanyabiashara katika
eneo la Kariakoo kugoma kufungua maduka yao wakilalamikia ujio wa
mashine za Kielektroniki za Kutolea Risiti (EFD).
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Askofu William
Mwamalanga alisema jana kuwa wamegundua mgogoro huo una lengo la
kuhujumu maendeleo ya Watanzania.
“Kufunga biashara kwa siku tano ni jambo ambalo halikubaliki katika nchi inayojitutumua kujitegemea,” alisema Askofu Mwamalanga.
Katika tamko hilo, maaskofu na masheikh walimtaka
Waziri Pinda kuwawajibisha baadhi ya watendaji wa Serikali wanaodaiwa
kutumia madaraka yao kukuza mgogoro huo.
“Viongozi wa dini ili tujenge nyumba za ibada,
hospitali, shule na miradi ya maji kwa jamii tunahitaji biashara,”
alisema Askofu Mwamalanga.
Katika hatua nyingine
Mjumbe wa kamati ya kitaifa ya kushughulikia vikwazo vya kibiashara visivyo vya forodha, Jimmy Mwalukelo alisema mgogoro huo unazorotesha uchumi.
“Kosa walilofanya TRA ni kupeleka mashine moja kwa
moja kwa wafanyabiashara bila kutupa elimu mawakala wao ambao ndiyo
tunaowapelekea wateja wetu.
“Mteja akitaka kwenda kulipa kodi ni lazima muhasibu amfanyie hesabu ndiyo aende kulipa kodi za ndani,” alisema Mwalukelo.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment