Social Icons

Pages

Wednesday, April 01, 2015

GWAJIMA ATOKA HOSPITALI, AACHIWA KWA DHAMANA

Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima akilalamika kwa maumivu alipokuwa akisaidiwa kuingia kwenye gari la Polisi  wakati akitolewa Hospitali ya TMJ na kupelekwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay Dar es Salaam, jana.
Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ameruhusiwa kutoka hospitalini alikokuwa amelazwa na baadaye kuachiwa na polisi kwa dhamana isiyokuwa na masharti.
Gwajima aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya TMJ alichukuliwa Kituo cha Polisi Oysterbay kwa kuwa jana ndiyo tarehe aliyokuwa ameitwa kuendelea na mahojiano baada ya kupoteza fahamu akiwa katika mahojiano ya awali.
Dk Fortunatus Mazigo aliyekuwa akimtibu Gwajima, alisema anaendelea vizuri hivyo angepewa kibali cha muda kutoka kwa sababu afya yake haikuwa imeimarika kwani hata kusimama ilikuwa ni lazima apate msaada.
Muda mfupi kabla ya kuruhusiwa lilifika gari la polisi aina ya Land Cruiser hospitalini hapo likiwa na askari wanne wenye bunduki na baada ya muda, likifuatiwa na gari jingine dogo la polisi aina  ya MG6 Turbo.
Polisi walioshuka kwenye gari ndogo walikwenda wodini alipokuwa amelazwa Askofu Gwajima na baada ya muda walirudi naye katika lifti.
Akiwa amevaa suti ya rangi ya kijivu na shati jekundu, Gwajima akiwa kwenye kiti cha magurudumu kilichopelekwa hospitalini na wasaidizi wake, akionekana mwenye maumivu aliingizwa katika gari hilo dogo na kupelekwa Kituo cha Polisi Oysterbay.
Alipofika katika mlango wa chumba cha Mkuu wa Upelelezi wa Kituo hicho, Salum Ngalama, ofisa huyo aliamuru Gwajima apewe dhamana na kesho aende Kituo Kikuu cha Polisi.
Baada ya kukamilisha taratibu, aliachiwa na baadaye aliwaambia waandishi wa habari kuwa ifike mahali viongozi wa dini waheshimiane na wanapokosolewa waache malumbano yasiyo kuwa na sababu.
Alisema katika jamii iliyostaarabika kuelekezana na kukemeana pale mmoja anapokosea ni kawaida na iwapo itafikia hatua hiyo hakuna haja ya mwingine kupiga kelele badala yake ayafanyie kazi aliyoelekezwa.
“Viongozi wa dini tuheshimiane, tusiwe wakali tunapokemewa na kuleta malumbano yasiyo ya msingi,” alisema Gwajima na kuelekea nyumbani kwake.
Njia ya kuelekea kanisani anakotoa huduma askofu  huyo, Kawe jijini Dar es Salaam, kulikuwa na makundi ya watu wakiimba nyimbo za kusifu, wengine wakiwa wamebeba matawi ya miti, wakitoka katikati ya Jiji  ambao walijiunga na wenzao waliokuwa polisi na kuanza safari kuelekea Kawe.
Wakili wa Gwajima, John Mallya alisema mteja wake ameachiwa kwa dhamana bila masharti yoyote na kutakiwa kufika kituo Kikuu cha Polisi kesho.
Alisema wachungaji 15 waliokamatwa kwa tuhuma za kutaka kumtorosha Askofu huyo wameachiwa pia, ingawa itawalazimu kuhoji kushikiliwa kwao zaidi na kuwekwa ndani zaidi ya saa 24.
Baadhi ya wachungaji hao walisema kuwa licha ya kukaa ndani siku tatu hawafahamu walikamatwa kwa sababu gani.
Mchungaji Yekonia Biyagaze alisema, hafahamu hadi leo alikamatwa kwa sababu gani, kwani hakufanya fujo, kutukana, kupiga kelele bali kumuhudumia mgonjwa. Mchungaji Fredrick Fussi alisema kama wana hatia wapelekwe mahakamani na wapo tayari kujibu tuhuma dhidi yao.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: