Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju.
Muswada wa Mahakama ya Kadhi umeondolewa bungeni
na sasa hautajadiliwa katika Mkutano wa 19 wa Bunge unaohitimishwa leo
mjini hapa.Huu ni muswada wa tatu kuondolewa Bungeni baada ya ile miwili ya
sekta ya habari ambayo ni muswada wa Sheria ya kupata Taarifa wa mwaka
2015 na ule wa sheria ya huduma wa Vyombo vya Habari iliyoondelewa
mwishoni mwa wiki iliyopita. Muswada huo ulipangwa kuwasilishwa Bungeni leo, lakini serikali imeamua kuuondoa kutokana na hofu ya kutokea mpasuko nchini.
KASHILILA: HAUTAWASILISHWA
Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, akizungumza na NIPASHE jana
ofisini kwake alisema muswada wa Mahakama ya Kadhi hautakuwapo tena
katika mkutano huo. Dk. Kashilila alisema haijulikani ni lini utawasilishwa bungeni kwa
sababu Mkutano wa Bunge ujao unaotarajia kufanyika Mei, utakuwa mahsusi
kwa ajili ya bajeti.
“Waziri Mkuu alivyosema wataangalia na kushauriana kimsingi, alitoa
maneno ya busara tu au ilikuwa kauli ya mtu mzima, lakini huu muswada
hautakuwapo,” alisema. Dk. Kashilila alisema hali iliyojitokeza Jumapili iliyopita wakati
wa semina ya wabunge haikuwa nzuri kutokana na mvutano mkali miongoni
mwa wabunge.
MASAJU AULIZWE SPIKA
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, alipoulizwa kuhusu
kama muswada huo utawasilishwa bungeni, alisema hakuwa na majibu badala
yake alitaka suala hilo iulizwe ofisi ya Spika. “Suala hili usiniulize, nenda Ofisi ya Spika au muulize huyu
(Magati) ambaye yupo sekretarieti,” alisema huku akiwa na haraka
kuelekea ofisini kwake.
NDUGAI: HAUPO
Naibu Spika, Job Ndugai, akizungumza na NIPASHE nje ya ukumbi wa
Bunge muda mfupi baada ya kuahirisha Bunge, alisema muswada wa Mahakama
ya Kadhi hautawasilishwa bungeni leo. “Huo muswada hauwezi kuletwa bungeni kutokana na hali ilivyo,” alisema Ndugai bila kufafanua zaidi.
MIGIRO ANG’AKA
Naye Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Asha-Rose Migiro, alipoulizwa
kama muswada huo utawasilishwa bungeni alimtaka mwandishi asimuulize
maswali yanayohusiana na muswada wa Mahakama ya Kadhi. “Sitaki kabisa kuulizwa suala la Muswada wa Mahakama ya Kadhi,
kwanza wewe unatoka gazeti gani, “alijibu Dk. Migiro kwa hasira huku
akiingia kantini.
MAASKOFU 4O WAPIGA KAMBI DODOMA
Katika hatua nyingine, juzi jioni maaskofu zaidi ya 40 kutoka mikoa
yote nchini, walikutana na wabunge katika ukumbi wa Kanisa La Kiinjili
la Kilutheli (KKKT) mjini Dodoma kujadiliana suala la muswada wa
Mahakama ya Kadhi. Baadhi ya wabunge waliohudhuria mkutano huo waliiambia NIPASHE kuwa
katika mkutano, maaskofu walitoa azimio kuwa muswada huo usiwasilishwe
bungeni kwa kuwa hatua hiyo inaweza kuhatarisha amani iliyoko nchini.
Maaskofu hao wanaounda Jukwaa la Kikristo Tanzania, waliwasili
mjini Dodoma tangu mwishoni mwa wiki iliyopita pamoja na mambo mengine
kufuatia kama muswada huo utawasilishwa bungeni. Hivi karibuni, Jukwaa la Wakristo Tanzania lilitoa tamko pamoja na mambo mengine kupinga uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi.
“Ikumbukwe Katiba Inayopendekezwa ilipitishwa kwenye Bunge Maalumu
la Katiba kwa ahadi ya Serikali kuipa dini ya Kiislam Mahakama ya Kadhi.
Inashangaza kuwa hata Serikali inatoa rushwa ili kufikia malengo yake.
Kwa hali kama hii, Kanisa haliwezi kuunga mkono kupitishwa kwa Katiba
Inayopendekezwa,” ilisema sehemu ya tamko hilo.
Kuhusu uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi , walisema inakiuka misingi
ya Taifa kuwa Serikali haina dini wala mfumo wa sheria unaobagua raia
wake kwa misingi ya dini. Hii ni mara ya pili muswada wa Mahakama ya Kadhi kuondolewa bungeni
saa ya majeruhi kutokana na upinzani kutoka kwa baadhi ya wabunge.
ULIONDOLEWA FEBRUARI
Februari mwaka huu, muswada huo pia uliondolewa bungeni kwa kile
Mwanasheria Mkuu wa Serikali alicholiambia NIPASHE kwamba ni kwenda
kuonana na viongozi wa dini kuwaelemisha juu ya mahakama hiyo, ili
uwasilishwe tena kwenye mkutano unamalizika leo.
VURUGU SEMINA YA WABUNGE
Mwishoni mwa wiki nusura wabunge wazipige kavu kavu huku
wakirusiana maneno wakati wa semina kuhusu Mahakama ya Kadhi. Kutokana
na joto lilivyopanda, baadhi waliamua kususia semina hiyo na kutoka huku
wengine wakibaki na kurushiana vijembe. Semina hiyo iliandaliwa na
Bunge.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment