Social Icons

Pages

Wednesday, April 01, 2015

NDUGAI AIBUKA SAKATA LA MGOMO WA WAFANYABIASHARA


Naibu Spika, Job Ndugai ambaye alipotea bungeni wakati wa mjadala moto wa sakata la akaunti ya Tegeta Escrow na kuzua maswali mengi, jana ameibukia katika sakata la wafanyabiashara baada ya wabunge kuwasha moto kutaka Serikali isikilize madai yao na kumwachia mwenyekiti wa jumuiya yao, Johnson Minja aliyenyimwa dhamana.
Ndugai alipotea katikati ya mkutano wa kumi na sita na kumi na saba wa Bunge uliojadili Escrow na jana aliibuka na kuongoza kikao cha Bunge kilichokuwa na mjadala mkali wa mgomo wa wafanyabiashara baada ya wabunge bila kujali itikadi zao kuibana Serikali wakiitaka ifanye kila njia kumwachia kwa dhamana Mwenyekiti wa Wafanyabiashara nchini, Johnson Minja kwa maelezo kuwa ikifanya hivyo itatuliza migomo hiyo. Kutokana na hali hiyo, Ndugai alilazimika kuiomba Kamati ya Uongozi ikutane, kujadili suala hilo na kutoa ushauri kwa Serikali.
Kabla ya kuahirisha Bunge jana mchana, Ndugai aliwaeleza wabunge kuwa kamati hiyo imeitaka Serikali kuharakisha mazungumzo yake na wafanyabiashara ili kumaliza malalamiko yao ambayo ni; ongezeko la kodi kwa asilimia 100, matumizi ya mashine za kielektroniki (EFD’s) na Minja kuachiwa kwa dhamana.
Mjadala mkali uliibuka baada ya kipindi cha maswali na majibu, baada ya wabunge 10 kusimama na kutaka kuomba mwongozo wa Spika wakishinikiza mgomo huo ujadiliwe kwa dharura kwa maelezo kuwa, unasababisha Serikali kukosa mapato na kuwatesa wananchi wanaohitaji kupata huduma.
Mbunge wa kwanza kupewa ruhusa ya kuzungumza alikuwa ni Deo Sanga (Njombe Kaskazini-CCM),  aliyetaka kujua sababu za Serikali kutotoa majibu ya uhakika wakati ikijua wazi kuwa mikoa ya Mbeya, Arusha, Dodoma na Tabora kulikuwa na migomo ya kimya kimya.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Ismail Aden Rage akisema kuwa Tabora mjini maduka yamefungwa tangu juzi na wananchi wanahangaika kwa kukosa huduma.
Alipopewa nafasi Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee alitaka Bunge lijadili mgomo huo kwa dharura kwa kuwa hali ni mbaya nchini.
Akitoa ufafanuzi wa Serikali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenister Mhagama alieleza kuwa Serikali inafanya mazungumzo na wafanyabiasha na yapo katika hatua nzuri, kuhusu ongezeko la kodi na matumizi ya mashine za EFD’s.
Kauli hiyo iliungwa mkono na wabunge wa CCM, akiwemo Rage na Sanga waliotaka wabunge wenzao wakubaliane na kauli ya Serikali na kuipa muda lakini wabunge wa upinzani walipinga.
Pia maelezo hayo ya Serikali yalipingwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, Luaga Mpina akisema kuwa tangu tume ya maridhiano kuundwa Julai mwaka jana, Serikali haijaitisha kikao na wafanyabiashara hao.
 Alisema baada ya kamati hiyo kushinikiza hatimaye Serikali ilikubali kufanya hivyo kukutana na wafanyabiashara hao Ijumaa iliyopita, kwamba kati ya makubaliano hayo ni pamoja na Minja kuachiwa huru.
“Inashangaza kuona kwamba pamoja na mazungumzo ya kina, Serikali imeshindwa kusimamia na kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa,” alisema.
Mvutano huo ulimuinua Mwanasheria Mkuu wa Serikali(AG), George Masaju na kuwataka wabunge waende mahakamani kwa ajili ya kutoa hoja za kumtoa Minja kwa dhamana na si bungeni kauli ambayo ilimfanya azomewe na baadhi ya wabunge.
“Minja aliachiwa kwa dhamana lakini alikiuka masharti ya dhamana kwa kuitisha vikao na migomo. Hapo ndipo Serikali ilipoieleza mahakama ambayo ilimfutia dhamana,” alisema Masaju.
Kauli hiyo ya Masaju iliwakera wabunge wengi huku Mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema), David Silinde  akishangazwa na Serikali kuendelea kumshikilia kiongozi huyo wakati hajatenda kosa la kufanya anyimwe dhamana.
Baada ya hali ya hewa kuchafuka zaidi, Ndugai ndipo alipotoa agizo la Kamati ya Uongozi kukutana ili kupata majibu ya uhakika.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: