Basi la Majinjah baada ya kuangukiwa na lori wilayani Mufindi, Iringa lilipokuwa likitokea Mbeya kwenda Dar es Salaam.
Ajali za vyombo
vya usafiri wa majini na barabarani huenda zikaendelea kutokea nchini na
kuchukua uhai wa watu wengi zaidi kila kukicha kutokana Serikali
kuwaadhibu madereva tu na kuwaacha maofisa waliohusika na miundombinu
mibovu na wanaoshindwa kukagua ipasavyo vyombo hivyo.
Kila zikitokea ajali za barabarani, Jeshi la
Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani hukimbilia kuwakamata madereva na
kuwafungulia mashtaka na wakati mwingine wamiliki wa vyombo hivyo,
lakini siyo maofisa waliosababisha barabara kujengwa chini ya kiwango,
nyembamba au kuacha mashimo bila kuyafukia wala maofisa wanaoacha
kukagua magari.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi, kwa muda mrefu
sasa, unaonyesha kwamba, Serikali imekuwa ikishituka tu wakati wa vifo
na viongozi wakihudhuria mazishi ambako hutoa makaripio na ahadi ya
kuwachukulia hatua madereva wanaodaiwa kuwa wazembe na kuwawajibisha
watendaji wote ambao hawafanyi lolote kuzuia majanga ya ajali. Lakini
huwa hakuna ufuatiliaji, hata kesi zikitupwa, Serikali huishia kuahidi
kukata rufaa bila utekelezaji.
Kwa ajali za barabarani, Jeshi la Polisi kitengo
cha Usalama Barabarani hukimbilia kuwakamata madereva na kuwafungulia
mashtaka, lakini wanaosababisha vifo katika matukio kama ya milipuko ya
mabomu au kuacha nyaya za umeme zikiwa zimelala barabarani hadi
kusababisha ajali hawachukuliwi hatua ambayo ni sawa na waliosimamia
ujenzi wa barabara nyembamba.
Takwimu za vifo
Wakati dawa ya kudhibiti ajali haijapatikana,
takwimu za Usalama Barabarani zinaonyesha kuwa mwaka 2012 kulikuwa na
ajali 11,438 zilizosababisha vifo vya watu 4,919; mwaka 2013 idadi ajali
ilikuwa 11,311 zilizosababisha vifo vya abiria 1,739 na mwaka jana
ajali zilikuwa 8,405 na vifo vilikuwa 1,743.
Kila vinapotokea vifo vya watu kutokana na ama
kulipuliwa na mabomu, ajali ya vyombo vya usafiri wa majini, barabarani
au kukanyaga umeme, Serikali hutoa kauli nzito na kuahidi kumchukulia
hatua kali mtu yeyote atakayebainika kuhusika kuonyesha kuwa
haitavumilia uzembe wa aina yoyote lakini baada ya muda, hali hubaki
ileile bila ufuatiliaji.
Nani alaumiwe?
Mkurugenzi mstaafu wa Mamlaka ya Udhibiti wa
Usafiri wa Nchi Kavu na Majini(Sumatra), Ahmed Kilima anasema ajali za
barabarani zinasababishwa na mazingira makubwa matatu ambayo ni makosa
ya kibinadamu, ubovu wa miundombinu na ubovu wa magari.
Kilima anataja makosa ya kibinadamu kuwa ni
mazingira ya uzembe wa dereva, ulevi, utoaji wa leseni kwa madereva
wasiokuwa na ujuzi wa kutosha, ukaguzi mdogo wa mabasi na malori
yanayosafiri mikoani, abiria kushabikia mwendo kasi na udhaifu wa
wamiliki wa mabasi na malori kuajiri madereva wasio na uwezo.
“Kwa hiyo, siwezi kusema nani alaumiwe lakini
mazingira yanaonyesha madereva na wamiliki wanahusika zaidi kwa upande
wao kabla ya kuangalia makosa mengine yanayotokana na mamlaka husika,”
alisema Kilima.
Katibu Mkuu wa Chama cha Kutetea Abiria Tanzania
(Chakua), Godwin Ntongeji anasema ili kupunguza au kuondoa kabisa tatizo
la ajali nchini, ni lazima ukaguzi wa mabasi na madereva ufanyike mara
kwa mara.
Majanga
“Hakuna ukaguzi na watu wanaendelea kufa njiani, ajali nyingine
siyo makosa ya dereva ila ni ubovu wa mabasi yenyewe. Jeshi la Polisi
lina wajibu wa kukagua kuanzia leseni za madereva mpaka uchakavu wa
mabasi, hivyo, haliwezi kukwepa lawama kwa namna yoyote juu ya vifo vya
Watanzania,” anasema.
Msemaji wa Sumatra, David Mziray anasema jukumu la
mamlaka hiyo ni kutoa leseni za biashara tu kwa wamiliki wa mabasi na
malori na kwamba hakuna basi au lori linalokabidhiwa leseni bila kuwa na
utambulisho wa dereva mwenye sifa zote.
“Sisi hatuwezi kuhoji ubora wa magari au dereva
kwa sababu anakuwa amekuja na vyeti vinavyoonyesha amethibitishwa na
Jeshi la Polisi kwamba ana sifa zote, kwa hiyo, tunatoa leseni kwa ajili
ya biashara ya kubeba abiria au mizigo,” anasema Mziray.
Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Malori
Tanzania, Clement Masanja anasema Serikali imeshindwa kusikiliza vyanzo
vya ndani vya ajali hizo kutoka kwa madereva wa malori. Anasema kuwa
jumla ya mabasi yanayotoka na kuingia kila siku katika Kituo cha Mabasi
Ubungo ni wastani wa 300 huku takriban asilimia 50 yakiwa mabovu.
Masanja anasema lazima Serikali ikubali kuhusika
na ajali za barabarani kutokana na ubovu wa miundombinu na kushindwa
kufanya ukaguzi wa mabasi mabovu. Kuna wakati Serikali iliwataka
wamiliki wa mabasi kufunga vidhibiti mwendo lakini viliondolewa na kuna
wakati Jeshi la Polisi lilipewa kamera kwa ajili ya kupima mwendo kasi,
lakini havitumiki ipasavyo.
Mnadhimu Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani,
Kamishna Msaidizi wa Polisi, Johanes Kahatano anasema licha ya madereva
kupinga, msimamo wa Serikali utabakia kuwa mwendokasi wa kilomita 80 kwa
saa.
“Pamoja na changamoto ya miundombinu ,lakini
kupunguza mwendokasi kutasaidia sana, hatuwezi kuendelea kuona ajali
zikitokea kwa mazingira ya mwendokasi,” anasema.
Kuhusu ukaguzi wa mabasi na leseni za madereva,
Kahatano anakiri kuwa ni changamoto kwa Serikali kutokana na ukosefu wa
vifaa vya kisasa kwani wamekuwa wakikagua mabasi hayo kwa macho tu bila
kujihakikishia undani wa basi kama ni bovu au la. “Lakini kwa ukaguzi wa
leseni tunajitahidi sasa kwani hatuwezi kuitoa leseni mpaka dereva
afanyiwe majaribio. Kuhusu mazingira ya rushwa katika leseni siwezi kuwa
na ushahidi kwa sababu hatujashuhudia tukio la rushwa katika utoaji wa
leseni,” alisema Kahatano.
Majanga
Mei 21, 1996 ilitokea ajali mbaya ya kuzama meli
ya mv Bukoba usiku ikiwa abiria kati ya 750 na 800 pamoja na wafanyakazi
37.Kati ya hao, 114 waliokolewa, maiti 391 ziliopolewa na kuzikwa
katika makaburi ya Igoma, nje kidogo ya Jiji la Mwanza. Miili mingine
ilichukuliwa na jamaa kuzikwa kwao. Miili 332 haikupatikana.
Serikali ilifungua kesi dhidi ya aliyekuwa nahodha
wa mv Bukoba, Jumanne Rume-Mwiru (sasa marehemu); Mkaguzi wa Mamlaka ya
Bandari, Gilbert Mokiwa; aliyekuwa Meneja wa Bandari ya Bukoba,
Alphonce Sambo na aliyekuwa Maneja wa Bandari ya Kemondo, Prosper
Lugumila. Kesi hiyo Na. 22 ya 1998, ilianza kusikilizwa Mei 14, 2001.
Wakati wa usikilizaji wa kesi hiyo iligundulika
kwamba meli hiyo iliyojengwa na kampuni ya Kibelgiji, siku ya uzinduzi
Julai 27, 1979 ilibainika haikuwa thabiti na ilikosa uwiano. Hukumu ya
kesi ilitolewa Novemba 29, 2002 na washitakiwa wote walishinda. Serikali
iliahidi kukata rufaa, lakini hadi leo haijafanya hivyo.
Mwaka 1998, basi la No Challenge la mkoani Tanga lilipata ajali
iliyosababisha vifo vya abiria wapatao 70 kutokana na kile aliyekuwa
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Simon Sirro kudai ni mwendo kasi na uzembe wa
dereva wa basi hilo. Baadaye basi hilo lilibadilishwa jina na kuitwa
Tashrif lakini nalo lilisababisha vifo vya watu 27 katika ajali
iliyotokea Korogwe.
Halafu ukaja mfululizo wa matukio ya mabasi
kugongana na treni pia magari moshi hayo kugongana yenyewe. Kwa mfano,
Juni 24, 2002 ilitokea ajali mbaya ya treni kuwahi kutokea barani Afrika
mkoani Dodoma. Treni iliyobeba abiria 1,200 ilirudi kinyumenyume katika
kilima kidogo na kugongana na treni ndogo ya mizigo na kusababisha vifo
vya watu 281. Ajali hiyo ilisababishwa na kushindwa kwa breki za treni
hiyo iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam, lakini hakuna aliyewajibishwa.
Machi 11, mwaka huu ilitokea ajali mbaya ya
barabarani katika Kijiji cha Changarawe wilayani Mufindi katika Mkoa wa
Iringa baada ya basi la Majinjah lililokuwa likitokea Mbeya kwenda Dar
es Salaam kugongana na lori la mizigo. Watu 50 walikufa na wengine 37
kujeruhiwa. Sababu za ajali hiyo imeelezwa kwamba nikuwapo kwa shimo la
muda mrefu katika eneo hilo la barabara.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment