Social Icons

Pages

Wednesday, April 08, 2015

MAWAZIRI MEMBE NA MWANDOSYA WAMZUNGUMZIA KARUME

Rais wa ‪Zanzibar‬, Dk Ali Mohamed Shein (wa pili kulia mbele) pamoja na viongozi wengine wakiomba dua iliyoongozwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kabi (kulia) katika kaburi la Marehemu Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Mzee Abeid Amani ‪Karume‬. Shughuli hiyo ya kisomo cha hitma ilifanyika jana katika Ukumbi wa Ofisi ya CCM Kisiwandui mjini Unguja.
Makada wa Chama cha Mapimduzi(CCM) wanaotajwa kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu ujao,  wamesema yapo mambo mengi ya kujifunza kutoka kwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, marehemu Sheikh Abeid Amani Karume aliyoyafanya katika miaka minane ya uongozi wake.
Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti mjini Zanzibar katika hitima ya kumkumbuka iliyofanyika Makao Makuu ya CCM Kisiwanduwi na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa akiwamo Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, walisema bado kuna safari ndefu ya kuyafikia mambo aliyoyafanya kiongozi huyo wakati wa uhai wake.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema kazi aliyoifanya Karume ya kuwasogezea maendeleo wananchi wake jirani bado inaendelea kuonekana na ni ya mfano katika Bara la Afrika. Alisema Karume aliwapenda wananchi wake ndiyo maana aliweza kufanya mambo makubwa ya maendeleo katika kipindi kifupi cha uongozi wake.
“Karume alitumia rasilimali za nchi kujenga nchi, hakuwa mbadhirifu ndiyo maana wananchi wanaendelea kumkumbuka kwa kuthamini kazi yake hiyo,” alisema Membe.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya alisema Karume ataendelea kukumbukwa na vizazi vingi kutokana na miradi mingi ya maendeleo aliyokuwa amefanya wakati wa uhai wake ikiwamo ya kuwapatia wananchi wake huduma za jamii bure pamoja na kufanikiwa kuondosha matabaka na kujenga umoja wa kitaifa visiwani humo.
“Ni kiongozi aliyekuwa na uwezo mkubwa katika kusimamia Serikali, ubadhirifu kwake ulikuwa mwiko katika Serikali yake,” alisema Profesa Mwandosya.
Mtoto wa marehemu Karume, Balozi mstaafu, Ali Abeid Karume alisema watu waliomuua baba yake walikuwa na mawazo kuwa kifo chake kingekuwa ndiyo mwisho wa Mapinduzi ya Zanzibar na Sultani kupata nafasi ya kurudi tena kutawala visiwani Zanzibar.
Mke wa Rais huyo wa Kwanza wa Zanzibar, Mama Fatma Karume alisema katika kumuenzi Karume, ni muhimu kwa wananchi na viongozi kuendelea kuimarisha misingi ya Muungano walioachiwa na waasisi hao akiwamo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Alisema yeye binafsi yuko tayari kugombana na mtu yeyote anayetaka kuuvunja Muungano kwa sababu umefanikiwa kuleta faida nyingi kwa wananchi ikiwamo kuimarisha ulinzi na usalama pamoja na kuimarisha umoja wa kitaifa.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: