Mkazi wa Kijitonyama,
Dar es Salaam, Joseph Mumbi ambaye alikamatwa na polisi Kisarawe
akishukiwa kutaka kufanya uhalifu wa kutumia bastola siku ya Ibada ya
Ijumaa Kuu ilipokuwa ikiendelea katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu
Stephano, ameachiwa jana kwa dhamana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei
alisema Mumbi ameachiwa baada ya Polisi kujiridhisha na maelezo ya awali
aliyoyatoa pamoja na kuwasilisha vielelezo vilivyothibitisho uhalali
wa umiliki wa silaha hiyo .
Hata hivyo, Kamanda Matei alisema pamoja na kupata
dhamana, polisi bado wanaendelea na uchunguzi ili kujiridhisha kama
hakuwa na nia mbaya.
Alisema madai kuwa alikuwa hatulii wakati wa misa
pamoja na kitendo chake cha kushika simu yake ya kiganjani mara kwa mara
kama mtu aliyekuwa akitaka kufanya mawasiliano kiasi cha kuwafanya
waumini wamshuku kuwa alitaka kufanya uhalifu, ndiyo yanayowafanya
waendelee kumchunguza.
Kamanda Matei aliongeza kuwa, tayari simu ya
mkononi aliyokua akiitumia kwa mawasiliano siku hiyo imepelekwa Ofisi ya
Kampuni ya Tigo ili wafuatilie mawasiliano yaliyofanyika siku hiyo.
“Tigo wanafuatilia mawasiliano ya simu hiyo halafu
watatutaarifu ili nasisi tukamilishe uchunguzi wetu kuhusiana na jambo
hili,” alisema Kamanda Matei.
Mumbi alishukiwa kuwa huenda akawa ni mhalifu kutokana na muonekano wake uliotia shaka.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment