Mgombea wa urais nchini Nigeria, Muhammadu Buhari akapiga kura.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, wananchi wa Nigeria
walipiga kura kumchagua Rais katika uchaguzi wenye ushindani mkali kati
ya Rais wa sasa, Goodluck Jonathan na mpinzani wake Jenerali Muhammadu
Buhari.
Katika makala haya, mtangazaji na mwandaaji wa vipindi katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Salimu Kikeke anazungumzia uzoefu alioupata katika mchakato wa uchaguzi huo, kama alivyohojiwa na mwandishi wetu.
Katika makala haya, mtangazaji na mwandaaji wa vipindi katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Salimu Kikeke anazungumzia uzoefu alioupata katika mchakato wa uchaguzi huo, kama alivyohojiwa na mwandishi wetu.
Swali: Tueleze uzoefu wako kuhusu matumizi ya
mfumo wa kielektroniki wa kuandikisha wapigakura na pengine changamoto
zake ulizozibaini nchini Nigeria?
Jibu: Nadhani dunia inaelekea katika mfumo wa
kidijitali na itafika wakati pengine kila nchi duniani itakuwa ikitumia
mfumo wa kielektroniki, katika uchaguzi, lakini pia katika mambo mengine
mbalimbali.
Kwa kuwa bado ni mfumo mpya, watu wengi hawajaweza
kuelewa hasa unafanyaje kazi. Nadhani uzuri wa mfumo huu, ni kwamba una
uwazi zaidi na matokeo yake yanaweza kuaminiwa na wapiga kura kwa kuwa
ni mashine ambazo hufanya kazi na hilo pia hupunguza uwezekano wa makosa
ambayo huweza kufanywa na binadamu. Vifaa vya kusomea kadi (card readers) vina betri
yenye uwezo wa kufanya kazi kwa saa 14, na husoma kadi moja kwa chini ya
sekunde 60 na ni vigumu ‘kuchakachua’ labda mtu aghushi ‘VIN,’ yaani
namba maalumu ya mpigakura.
Kwa hiyo mfumo huu una ufanisi mkubwa, lakini kama
teknolojia nyingine zozote mpya, zina changamoto zake siku za mwanzo,
na zinapozoeleka hali inakuwa tofauti.
Swali: Kipi kimekukosha na kukusononesha kuhusu mchakato mzima wa uandikishaji na uendeshwaji wa kampeni nchini Nigeria?
Jibu: Hii ni moja ya nchi zinazoelezwa kuwa na
demokrasia kubwa barani Afrika. Pia kwa mara ya kwanza katika kipindi
cha miaka mingi, uchaguzi huu una ushindani mkali kati ya wagombea urais
ambao ni Goodluck Jonathan wa chama tawala PDP na Jenerali Muhhamadu
Buhari wa chama cha upinzani APC, wanavutana vikali kabisa.
Kitu ambacho kimenivutia hasa ninapozungumza na
wananchi wa hapa, ni kutaja suala la amani. Licha ya vuta nikuvute
iliyopo, wengi wanasema cha msingi ni kufanya uchaguzi huu kwa amani.
Kumekuwa na vijembe vya hapa na pale, na wakati mwingine ghadhabu ambazo
unaweza kudhani zitavuka mipaka na kuleta tafrani, lakini hilo
halijajitokeza kwa kiwango kikubwa cha kutisha- ukiacha matukio ya
Desemba mwaka jana, ambapo kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya haki za
Binadamu watu takriban 58 waliuawa katika ghasia zinazihusiana na
uchaguzi katika sehemu mbalimbali.
Pamoja na kuwa masuala makuu kama usalama, ufisadi
na uchumi ni mambo yanayozungumzwa zaidi kwenye vyombo vya habari,
wananchi wengi wa kawaida wanataka mambo ya kila siku maishani kama vile
umeme na maji, lakini kubwa kuliko yote wanataka amani.
Kampeni kwa jumla zimekuwa salama na kwa kuwa kuna
ushindani mkali katika urais, wagombea wamekuwa wakijinadi kwa kusema
kinagaubaga jinsi watakavyokabiliana na changamoto za taifa hili. Jambo
zuri pengine ni kuwa wote wamewahi kuongoza taifa hili.
Swali: Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC), imekuwa ikilalamikiwa
kwa kutokuwa chombo huru, hali ikoje Nigeria kuhusu chombo
kinachosimamia masuala ya uchaguzi?
Jibu: Hii ni changamoto kubwa kwa Mwenyekiti wa
Tume huru ya Uchaguzi ya Taifa ya Nigeria (INEC). Profesa Attahiru
Muhammadu Jega aliteuliwa na Rais Goodluck Jonathan kuongoza taasisi hii
muhimu Juni 8 mwaka 2010, baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa mwenyekiti
Profesa Maurice .
Kuteuliwa kwake kuliidhinishwa na mkutano wa
vigogo uliohudhuriwa na viongozi wa zamani wanaoheshimika kama vile
Yakubu Gowon, Muhammadu Buhari (Mgombea wa upinzani wa sasa), Ibrahim
Babangida, Abdulsalami Abubakar, Ernest Shonekan, Olusegun Obasanjo na
Shehu Shagari.
Wengi kutoka vyama vya kiraia na hata wanasiasa
waliupokea vyema uteuzi huo na wananchi wana imani kuwa Profesa Jega
ataweza kazi hii na ataifanya kwa uhuru na uwazi.
Nigeria ikitajwa kuwa na demokrasia kubwa Afrika
haitotaka kuharibu jina lake, hasa kwa kutazama nchi jirani ya Ghana
ambayo Mwenyekiti wake, Kwadwo Afari-Gyan ameshikiliwa wadhifa huo tangu
mwaka 1993. Wadadisi wanasema Jega naye anaweza kufanya hivyo kama
atapatiwa nafasi.
Swali: Ukiwa Mtanzania unafahamu fika taratibu za
mfumo wa uchaguzi uliopo nyumbani, Je, mfumo huu una tofauti yoyote na
unaotumika Nigeria?
Jibu: Mifumo inafanana kwenye uchaguzi wa urais na
wabunge. Kuna wagombea urais 14, lakini wawili ndio wanachuana zaidi
ambao ni Goodluck Jonathan na Muhammadu Buhari. Kura ni ya siri kama
Tanzania na rais anapigiwa kura na wananchi, na anayepata kura nyingi
zaidi ndio anakuwa mshindi. Tofauti na Tanzania huku kuna mfumo wa
magavana ambao uchaguzi wao unatarajiwa kufanyika baadaye mwezi huu.
Swali: Unautazamaje ushiriki wa vyombo vya habari
katika mchakato wa uchaguzi huko, Je, kuna mazingira mwafaka na huru kwa
vyombo kufuatilia uchaguzi?
Jibu: Kihistoria ukitazama, Nigeria imekuwa na uhuru mkubwa wa habari pengine kuliko nchi yeyote ile barani Afrika.
Pamoja na kuwa katika miaka ya nyuma wamepitia
changamoto kubwa hasa katika enzi za utawala wa kijeshi, lakini vyombo
vya habari, hasa magazeti yameweza kukabiliana vilivyo na changamoto
hizo.
Katika uchaguzi huu, ambao una mvutano mkali
katika nafasi ya urais, wananchi wanapata nafasi ya kusoma yote; mabaya
na mazuri ya wagombea na hivyo kuwapa wapiga kura taswira ya kile
wanachotaka inapofika siku ya upigaji kura.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment