Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye,
ametahadharisha kuwa, madhara ya kutosikiliza kero za walimu yatakuwa
makubwa siku za baadaye.
Alisema hayo wakati akizungumza na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama
cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Hanang, mjini hapa, mwishoni mwa
wiki. Alisema wakati akiwa Waziri Mkuu, aliyekuwa Rais wa CWT ambaye sasa
ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Margaret Sitta, alikuwa akifanya naye
vikao kuzungumzia masuala mbalimbali ya walimu ili kuyapatia ufumbuzi.
“Margaret Sitta alikuwa ananipigia simu mara kwa mara kutaka
nikutane na kamati yake kuzungumzia mambo yanayopamba moto kwa walimu,
sikukataa, mara zote nilikuwa nawakaribisha na kukutana hata mara tatu
kwa wiki. Huwezi kukataa kuonana na walimu, hao ndio wanaopigika, sasa
wewe ni nani mpaka unasema huna nafasi, huna nafasi na nani?, unakataa
kuonana na walimu ambao wanatengeneza taifa la kesho?” alihoji.
Akizungumzia suala la elimu, Sumaye alikosoa utaratibu wa kufaulisha wanafunzi wengi kwa kushusha viwango vya elimu. Alisema utaratibu huo ni sawa na kumpitisha ng’ombe kwenye josho
mradi tu awe amelowana, yaani bila kujali iwapo josho hilo lina dawa ya
kuua kupe au la.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment