Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe.
Mpango maalum wa kuboresha huduma za majisafi na majitaka jijini Dar es Salaam utagharimu Sh. trilioni 1.088, Bunge limeelezwa.
Hayo yalielezwa bungeni jana na Waziri wa Maji, Prof. Jumanne
Maghembe, alipokuwa akitoa kauli ya serikali kuhusu
utekelezaji wa mpango huo. Alisema mpango huo ambao ulianza Februari 2011, umelenga kupanua
mtambo wa maji wa Ruvu chini kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa maji
kutoka lita milioni 180 kwa siku hadi lita milioni 270 kwa siku.
Alisema kazi inayofanyika sasa ni ulazaji wa bomba kubwa la maji
kutoka Ruvu chini hadi jijini Dar es Salaam kazi ambayo imeshafanyika
kwa asilimia 93 na serikali pia inakarabati matenki ya kuhifadhia maji
yaliyopo Chuo Kikuu cha Ardhi.
Alisema mpango huo pia umelenga kupanua mtambo wa Ruvu juu ili
kuongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 82 kwa siku hadi lita
milioni 196 kwa siku, akieleza kuwa upanuzi huo utaenda sambamba na
ulazaji wa bomba kubwa kutoka Mlandizi hadi Kimara na ujenzi wa tenki la
kuhifadhia maji Kibamba.
Alisema serikali imechimba visima 20 Kimbiji na Mpera vitakavyoweza
kuzalisha lita milioni 260 za maji kwa siku na kwamba hadi wiki
iliyopita, mkandarasi alikwishachimba visima vitatu. Alisema kazi nyingine ni ujenzi wa bwawa la Kidunda litakalohifadhi
maji ili kuhakikisha maji ya mto Ruvu yanakuwapo kipindi chote cha
mwaka.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment