Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, akisaidiwa
kusukumwa katika baiskeli ya miguu mitatu alipowasili katika Kituo cha
Polisi cha Oysterbay, jijini Dar es Salaam jana baada ya kutoka hospitali
alikokuwa amelazwa ili kumalizia mahojiano na Jeshi la Polisi.Askofu wa Kanisa la Ufunuo na Uzima, Josephat
Gwajima, ametolewa hospitali na Jeshi la Polisi kumwachia bila
masharti yoyote. Askofu Gwajima, ambaye alilazwa katika Hospitali ya TMJ kwa siku
nne baada ya kuugua ghafla wakati akihojiwa na polisi, alitolewa katika
hospitali hiyo jana saa 6:15 mchana na maofisa wa jeshi hilo waliovalia
nguo za kiraia.
Maofisa hao waliofika saa 6:15 mchana wakiwa kwenye magari mawili na kuingia moja kwa moja hadi chumba alichokuwa amelazwa muda mfupi baadaye, walitoka wakiwa na Askofu Gwajima aliyekuwa amebebwa kwenye machela akisaidiwa na wafuasi wake kuisukuma.
Askofu Gwajima aliingizwa katika moja ya magari ya polisi lililofika katika hospitali hiyo kumchukua. Dakika chache baadaye, alipakiwa kwenye gari hilo na kuondoka hadi
katika kituo cha polisi cha Oysterbay, ambako waliwasili saa 6: 50
mchana.
Alipofikishwa katika kituo hicho, aliingizwa katika Kitengo cha
Upelelezi Mkoa wa Kinondoni akiwa kwenye machela, huku akifuatana na
Wakili wake, John Mallya, na kuruhusiwa huku akielezwa kuripoti kesho
katika Kituo cha Polisi cha Kati.
Hata hivyo, ilichukua muda wa takriban saa moja na nusu kukamilisha
taratibu huku waandishi wa habari na wafuasi wake wakiwa nje
wakimsubiri. Baada ya kuruhusiwa akiwa ndani ya gari lake akizongwa na umati wa watu, alisema afya yake imeimarika.
Alisema wachungaji wanapaswa kuheshimiwa kutokana na kauli wanazozitoa. Askofu Gwajima alisema kwa sasa anaenda kupumzika, hivyo akalitaka jeshi hilo kutotumia nguvu katika kupata mwafaka. Nje ya kituo cha polisi Oysterbay, mamia ya waumini wa Askofu
Gwajima walifurika wakisubiri kujua hatima ya kiongozi wao.Wafuasi hao
waliokuwa wamevalia mavazi ya kiuchungaji, walionekana wakirandaranda
nje ya viwanja vya kituo hicho.
Baada ya kuruhusiwa, wafuasi hao waliruka ruka kwa furaha, huku
wakiimba nyimbo za kumtukuza Yesu Kristo na kulisukuma gari lililombeba. Baadhi ya waumini waliamua kutembea kwa miguu kutoka kituo hicho
hadi kanisani kwenye viwanja vya Tanganyika Pakers, huku wakiwa wanaimba
na kushikilia matawi ya mti.
Katika kituo kikuu cha polisi, waumini hao walipiga kambi na
walianza kumiminika saa 3.00 asubuhi na kusababisha eneo hilo kufurika
watu. Ulinzi ulikuwa umeimarishwa katika eneo hilo na baadhi yao
waliondolewa, hivyo kulazimika kusambaa maeneo yaliyo karibu na kituo
hicho, huku wachache wakiruhusiwa kuingia eneo la kituo.
Kumiminika kwa wafuasi hao katika kituo hicho kulitokana na taarifa
zilizoeleza kwamba Askofu Gwajima angefikishwa katika kituo hicho kwa
ajili ya hatua nyingine za kipolisi. Majira ya saa 6:35 mchana, walipata taarifa kwamba anapelekwa
Oysterbay, hali iliyoulazimisha umati wa waumini hao kukodi magari
kuelekea huko. Awali, maaskofu wa makanisa ya Kipentekoste walikuwa wamepanga
kwenda kuonana na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu,
kuzungumzia suala la Askofu Gwajima.
Hata hivyo, walishindwa kumuona IGP, huku baadhi yao wakianzia
katika ofisi ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova, ambaye hata hivyo hawakufanikiwa kumuona kutokana na kuwa
nje ya ofisi. Wakili wake, Mallya, alisema aliruhusiwa bila masharti.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment