Social Icons

Pages

Wednesday, April 01, 2015

MAJAMBAZI YAUA TENA POLISI

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
Matukio ya majambazi kuua polisi yameendelea kulitikisa Jeshi la Polisi, baada ya askari wawili kuuawa na mmoja kujeruhiwa.
Askari hao wa Mkoa wa Kipolisi  Temeke, waliuawa na watu wanaodaiwa kuwa majambazi na mmoja kujeruhiwa kwa risasi. Tukio hilo lilitokea juzi usiku katika kizuizi cha polisi kilichopo kijiji cha Kipara Mpakani (ambacho ni kijiji cha kwanza cha wilaya Mkuranga), kata ya Vikindu, mkoani Pwani.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, jana alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa, linaonyesha chembe za ugaidi na kwamba upelelezi wa kina unafanyika ili kuona ukweli wa tukio hilo kama lina sura ya ujambazi au ugaidi.
Wakati Jeshi la Polisi likidai kuwa katika eneo la tukio kulikuwa na mashambulizi makali ya kujibizana kwa risasi kati ya askari na majambazi waliokuwa wanane hadi 10 wakitumia mapanga kuwashambulia askari watatu waliokuwa kwenye kizuizi hicho, mashuhuda wa tukio hilo wanaeleza kuwa walikuwa majambazi wawili na walitokea kwenye msitu wa hifadhi ya jamii wa Vikindu.
Kamanda Kova aliwataja askari waliopoteza maisha kuwa ni D. 2865 Sajenti Fransis na Koplo E.177 Michael ambaye ni askari wa kikosi cha usalama barabarani ambao walifariki dunia papo hapo. Alisema katika tukio hilo askari mmoja Sajenti 5573 Ally Mapuzi, ambaye alijeruhiwa kwa risasi kwenye paja la mguu wa kushoto na amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Temeke kwa matibabu.
“Majambazi hao waliwashambulia kwa ghafla askari kisha kupora silaha aina ya SMG ikiwa na risasi 30 ndani ya magazine na kutokomea kusikojulikana…askari aliyejeruhiwa alipambana vikali na majambazi hayo kwa kutumia bunduki aliyokuwa nayo ambayo walishindwa kuipora hivyo kutokomea pori la Vikindu,” alisema.

OPERESHENI KABAMBE KUFANYIKA
Kova alisema jeshi hilo linaendesha opereshini kali ya aina yake ya kuwasaka watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, waliovamia na kuwaua askari hao na kujeruhi. Alisema nguvu na mbinu zote za kipolisi zitatumika na kwamba vikosi vya Kanda Maalum Dar es Salaam na mkoa wa Pwani vimeshaanza ili kuhakikisha majambazi hao wanapatikana haraka iwezekanavyo.
“Pamoja na operesheni hiyo, Jeshi la Polisi linachunguza ili kubaini kama tukio hili linaashiria vitendo vya ugaidi au ni ujambazi wa kutumia silaha…natoa wito kwa wananchi wa mikoa hii kupitia dhana ya polisi jamii kushirikiana nasi kwa hali na mali kwa kutoa taarifa sahihi,” alisema.
 
MASHUHUDA WAZUNGUMZA
 Wakizungumza na NIPASHE katika eneo la tukio jana, baadhi ya mashuhuda walisema, watu wawili wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wakiwa na bunduki moja walitokea kwenye msitu wa hifadhi ya jamii ya Kipara mpakani na kuwavamia askari hao ghafla waliokuwa kwenye kizuizi hicho na kuwashambulia kwa risasi na kuwapora silaha na kutokomea msituni.
Mmiliki wa duka la kuuza vinywaji, Mohamed Ally, ambaye mmoja wa askari alifariki akiwa kwenye kibaraza cha duka lake, alisema tukio hilo lilitokea wakati akiwa dukani hapo akiendelea na shughuli zake. Alisema ilitokea majira ya saa 2:00 usiku wakati polisi hao watatu wakiwa kwenye eneo hilo, mara ghafla walitokea watu wawili ambao walikuwa na bunduki moja na kuanza kuwashambulia askari hao.
“Baada ya kumpiga risasi askari aliyekuwa amekaa kwenye kiti alinyanyuka na kutaka kujiokoa, lakini walimfuata hadi nje ya kibaraza cha duka langu na kummiminia risasi nyingine na kufariki papo hapo mwingine aliyekuwa amesimama aliuawa papo hapo na mmoja alijeruhiwa alikimbia, walirusha risasi nyingi hewani na kuwa kama uwanja wa mapambano ya vita na kusababisha taharuki kubwa kwa wananchi,” alisema na kuongeza:
“Nikiwa hapa usiku wakati haya maduka yote yamefungwa, watu wasiyofahamika wawili waliwasili katika eneo la tukio wakiwa hawana usafiri wowote na walianza kuwarushia risasi askari na mara baada ya kuona hali ni mbaya na mimi nilikimbia kujiokoa.”
Ally ambaye dukani kwake ni hatua chache kutoka eneo la tukio, alisema inavyoonyesha majambazi hao walikuwa na lengo mahususi la kupora silaha na kuua na siyo kuiba mali yoyote kwani baada ya kupora silaha waliondoka kurudi kwenye pori walilotokea.
Jirani wa eneo la kizuzi hicho, Rehema Yusuph, alisema majira ya saa 2:00 usiku akiwa na wanawe alisikia milio mingi ya risasi na walilazimika kulala chini ili kujiokoa. “Nakumbuka ilikuwa muda wa swala ya Ishah, tunasubiri kupata mlo wa usiku, tulisikia milio mingi ya risasi, nilikumbatia wanangu tukalala chini tukisubiri lolote litakalotokea hatukuwa na jinsi,” alisema.
Alisema kizuizi hicho kiliwekwa na polisi baada ya tukio la kuuawa polisi wa Ikwiriri na kwamba hakina miezi miwili au mitatu na kwamba wamekuwa wakipeana zamu. “Baada ya hali kutulia tulitoka na kukuta askari mmoja kalala kwenye kibaraza cha duka, mwingine chini ya mti waliokuwepo walitueleza kuwa ni majambazi wawili walivamia na kuwapora silaha na kumjeruhi mmoja na kuua wawili…tumeogopa sana kwa kuwa hii ni mara ya pili eneo letu linavamiwa kwa kuwa miaka miwili iliyopita walivamia kituo cha mafuta cha Lake Oil na kupora fedha,” alisema.
Mkazi wa eneo hilo, Tatu Bakari, alisema akiwa nyumbani kwake alisikia milio ya risasi kwa muda wa nusu saa na alipotoka alikuta polisi wamejaa eneo la tukio. Jana NIPASHE lilikuta magari ya polisi wanane yakiwa na askari waliokuwa wamevalia sare na wengine kiraia.
 
ASKARI ALIYEJERUHIWA AZUNGUMZA 
Askari aliyejeruhiwa katika tukio hilo, Sajenti Ally na kulazwa wodi namba tano, alisema akiwa kwenye lindo na wenzake alishangaa kuona watu wasiofahamika wakitokea porini wakiwa na silaha kama bunduki na silaha za jadi kama panga na kwamba walianza kuwashambulia kwa kuwapiga risasi.
“Mmoja kati yetu alipigwa kwa panga shingoni na risasi sehemu mbalimbali za mwili, baada ya kuona hivyo nilikimbia kujiokoa, lakini nilipigwa risasi ya kwenye paja ambayo haikugusa mfupa na iliingia kwenye nyama na kutokea upande wa pili, hali ilivyozidi kuwa mbaya nilikimbia kujificha, nilikaa huko hadi nilipojiridhisha kuwa hali imetulia,” alisema.
Alisema walijitokeza watu mbalimbali kuwasaidia na alipelekwa Zahanati ya Kongowe kwa huduma ya kwanza na baadaye alihamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Temeke.
 
JESHI LA POLISI KUSHUGHULIKIA MAZISHI
Kamanda Kova alisema Jeshi la Polisi litagharamia mazishi ya askari hao kama ilivyo utaratibu wa ndani ya jeshi kuwasaidia askari wake.
 
MATUKIO POLISI KUUAWA
Matukio ya polisi kuuawa yamekuwa yakitokea katika kipindi kifupi ndani ya mwaka mmoja katika siku za hivi karibuni. Septemba, mwaka jana, tukio kama hilo lilitokea katika kituo kikuu cha polisi kilichoko wilaya ya Bukombe, mkoani Geita, ambako askari wawili waliripotiwa kuuawa, wengine watatu kujeruhiwa na bunduki 10 aina ya SMG, pamoja na risasi na mabomu ya kutupa kwa mkono, ambayo idadi yake haikujulikana, yaliporwa na majambazi.
Juni 11, mwaka huo, majambazi walivamia kituo kidogo cha polisi Mkamba kilichoko katika wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani na kuua askari polisi mmoja na mgambo mmoja na kujeruhi askari polisi mwingine mmoja. Katika tukio hilo iliripotiwa kuwa, mjambazi hao yalipora bunduki mbili aina ya SMG, tatu aina ya shotgun na magazini 30 zilizokuwa kwenye ghala kuu la silaha.
Pia tukio kama hilo, lilitokea Januari 21, mwaka huu, katika kituo cha polisi Ikwiriri, kilichopo katika tarafa ya Ikwiriri, wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani, ambako iliripotiwa askari wawili kuuawa na majambazi 10 waliovamia kituo hicho na kupora silaha saba na kisha kulipua bomu kituoni hapo. 
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: