Eneo la kizuizi cha magari Mbagala Kongowe nje kidogo ya jiji la Dar es
Salaam lilipotokea tukio la kuvamiwa kwa askari na kusababisha wawili
kuuawa kwa kupigwa risasi, juzi usiku.
Askari polisi wawili
wameuawa na mmoja kujeruhiwa baada ya kuvamiwa na watu wanaodhaniwa
kuwa na viashiria vya ama ugaidi au ujambazi katika kizuizi cha barabara
ya Kilwa, Kipara Mpakani, Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani.
Tukio hilo ambalo tayari limelaaniwa na Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe na Tume ya Utawala Bora na Haki
za Binadamu, limekuja katika kipindi ambacho Mkuu wa Jeshi la Polisi
(IGP), Ernest Mangu amepangua makamanda na maofisa wa polisi 160 nchini
kote.
Wakati Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam
ikisema inachunguza chanzo cha vifo vya askari hao ambao ni wa kanda
hiyo, Chikawe alisema tukio hilo linawezekana kuwa la kigaidi au
ujambazi lenye lengo la kuchukua silaha kwenda kufanyia matuko
mbalimbali. Askari waliouawa ni D.2865 SGT Francis na E.177 CPL Michael wakati aliyejeruhiwa ni D 5573 D/SGT Ally.
Mashuhuda
Walioshuhudia tukio hilo walisema lilitokea juzi
saa mbili usiku na kudumu kwa dakika 10 na kufanya eneo hilo kuwa kama
uwanja wa vita kutokana na milio ya risasi.
Mkazi wa eneo hilo, Mohamed Ali alisema aliwaona
watu watano wakitokea katika Pori la Kipara Mpakani, mmoja akiwa
ameshika bunduki na mwingine panga. “Niliwaona wakiwafuata askari karibu na kizuizi,
mmoja alimpiga polisi risasi kifuani na mwingine akamkata polisi kwa
panga shingoni,” alisema na kuongeza kuwa aliwaona askari hao wakiwa
wamelala chini baada ya kuuawa. “Baada ya tukio hilo, watu wote
waliokuwa karibu na eneo hili walikimbia kujificha wakihofia usalama
wao.”
Shuhuda mwingine, Shiraz Abdul alisema alimwona
mmoja wa askari mwingine akikimbia pamoja na wananchi baada ya tafrani
hiyo... “Niliwaona askari watatu wakiwa wamelala chini, mmoja akiwa
analia kuomba msaada,” aliongeza.
Shuhuda, Rehema Yusuph ambaye anaishi karibu na
barabara kilipo kizuizi hicho alisema, walianza kusikia watu wakipiga
kelele na kuhisi kwamba ilikuwa ajali.
“Mara nyingi huwa ajali zinatokea hapo barabarani,
kwa hiyo sisi tulidhani kwamba ilikuwa ajali. Lakini baada ya sekunde
chache tulianza kusikia milio ya risasi. Mara nikaona watu wanakimbilia
kwenye veranda yangu, baada ya kuuliza wakasema kuna watu wamevamia
hicho kituo na wameua na kujeruhi askari.”
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova alisema jeshi hilo linachunguza kama waliofanya mauaji
hayo ni magaidi au majambazi.
“Kwa jinsi walivyofanya uvamizi wa kushtukiza, kuna viashiria
vya ugaidi, Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi wa kina ili kubaini,”
alisema. Alisema askari hao walivamiwa na kundi la watu wanaokadiriwa kuwa kati ya wanane hadi kumi wakiwa na mapanga na silaha nyingine.
“Ghafla waliwavamia askari watatu waliokuwa kazini
katika kizuizi hicho kisha kupora bunduki aina ya SMG ikiwa na risasi
30 ndani ya magazine na kutokomea kusikojulikana,” alisema.
Alisema polisi mwenye namba D.5573 D/SGT Ally
alipambana na wauaji hao kwa kutumia bunduki aliyokuwa nayo ya SMG
lakini alizidiwa na kujeruhiwa kwenye paja la mguu wa kushoto na
amelazwa katika hospitali ya Temeke.
Majeruhi azungumza
Akizungumza kwa tabu katika Wodi namba 5 kwenye hospitali hiyo, Ally alisema walivamiwa na kundi la watu wenye mapanga. Alisema alipambana nao lakini kutokana na wingi wao walipora silaha ya askari mwenzake na kuondoka nayo.
Ahadi ya Chikawe
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe
alisema Serikali imesikitishwa na mauaji ya askari hao na kwamba
itahakikisha wahalifu hao watapatikana na kuchukuliwa hatua kali.
“Hii hali haiwezi kuhimilika, askari wangu wawili
wameuawa tena wakiwa kazini na hii si mara ya kwanza ni lazima hatua
zichukuliwe kama ambavyo tulishafanyia kazi matukio ya awali. Ningekuwa
na uwezo ningesimama mwenyewe na kuwa wakili katika kesi za wahalifu hao
mara watakapopatikana.”
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, nayo imeeleza kusikitishwa na kulaani vikali mauaji ya askari hao wakiwa kazini.
Tamko hilo lililosainiwa na Mwenyekiti wa Tume
hiyo, Bahame Nyanduga imesema mbali na tukio hilo, imelaani kujeruhiwa
vibaya kwa wafuasi 25 wa Chama cha Wananchi (CUF) lililotokea Machi 25
Makunduchi, Zanzibar. “Tume inawataka wananchi kuheshimu haki za binadamu na kuwa
wavumilivu katika kipindi hiki ambacho nchi inakabiliwa na matukio
makubwa ya kuipigia kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa na Uchaguzi
Mkuu Oktoba,” lilisema tamko hilo.
Mabadiliko polisi
Wakati hayo yakitokea, IGP Mangu amefanya mabadiliko makubwa ambayo yanagusa vigogo 160 wa jeshi hilo nchi nzima. Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na
jeshi hilo, zimeeleza kuwa mabadiliko hayo yamegusa pia safu ya juu ya
uongozi wa jeshi hilo, ikiwa ni mabadiliko makubwa tangu ashike wadhifa
huo.
Katika mabadiliko hayo, baadhi ya makamanda wa
mikoa wamehamishwa kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine huku baadhi ya
wasaidizi wao wakipandishwa vyeo.
“Uhamisho huu utekelezwe mara moja na mishahara
yao ihamishiwe vituo vyao vipya,” inaeleza taarifa hiyo iliyolewa juzi
na kusambazwa kwa makamanda wa mikoa nchini na kusainiwa na Naibu
Kamishna wa Polisi (DCP), G.A. Semiono. Katika mabadiliko hayo, DCP Ally Mlege aliyekuwa
Kanda ya Dar es Salaam, anakwenda kuwa mkuu wa kitengo cha kuzuia
uhalifu makao makuu.
DCP Daniel Nyambabe aliyekuwa idara ya uhusiano wa
kimataifa, anakwenda kuwa mkuu wa operesheni wa jeshi hilo. Kadhalika,
DCP Valentino Mlowola aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza
anakwenda kuwa Mkurugenzi wa kitengo cha intelijensia.
DCP Robert Mikomangwa anatoka Makao Makuu ya
Polisi kwenda kuwa mkuu wa kitengo cha upelelezi cha kukabiliana na
changamoto ya ongezeko la uhalifu. Mabadiliko hayo pia yamemgusa DCP Maria Nzuki aliyekuwa RPC Ilala ambaye sasa anakuwa mkuu wa kitengo cha Polisi Jamii. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Geofrey Kamwela amerudishwa makao makuu ya polisi kitengo cha upelelezi.
Maofisa wengine waliohamishwa ni SACP Lucas
Mkondya anayetoka CO Vehicle Management kwenda kuwa RPC Ilala wakati RPC
Pwani, Ulrich Matei akihamishiwa Kanda ya Dar es Salaam. SACP Fulgence Ngonyani anatoka kuwa RPC Njombe na kwenda kuwa
RPC Kilimanjaro na SACP Ferdinand Mtui anatoka Idara ya Operesheni
kwenda kuwa RPC Kigoma.
RPC Tanga, Frasser Kashai anatoka Tanga na kuwa Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU). ACP Franco Kibona anatoka RCO Njombe na kupanda
cheo kuwa RPC Njombe, ACP Zuberi Mwombeji ambaye ni RCO Iringa naye
anakuwa RPC Tanga.
Uhamisho huo pia umemgusa ACP Gemini Mushi
aliyekuwa Ofisa Mnadhimu mkoa wa Manyara anayekwenda kuwa RPC Mkoa wa
Simiyu. Uhamisho huo umegusa Ma-RCO, wakuu wa polisi wa wilaya (OCD),
wakuu wa upelelezi wa wilaya (OC-CID), wakuu wa vituo (OCS) na maofisa
wanadhimu.
Mabadiliko hayo yamekuja wakati jeshi hilo
likitikiswa na vitendo vya uhalifu likiwamo wimbi jipya la kuvamiwa na
kuuawa kwa polisi na kuporwa bunduki za kivita.
IGP Mangu alithibitishwa kuwapo kwa mabadiliko hayo na kuthibitishwa pia na msemaji wa jeshi hilo, Advera Bulimba.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment