Mkazi wa Mbondole, Kata ya Msongola, Dar es Salaam Uwesu Mansuri (28)
akiwa kwenye kibanda alichotengenezewa na wazazi wake huku akiwa
amefungwa mnyororo mguuni, jana.
Unakumbuka
masaibu ya mtoto, hayati Nasra Mvungi aliyeishi kwenye boksi miaka
mitatu? Mkazi wa Mbondole, Wilaya ya Ilala, Uwesu Mansuri (28) naye
ameishi kwa kufungwa mnyororo mguuni na wazazi wake kwa miaka mitatu kwa
madai ya kulinda usalama wake.
Kijana huyo ambaye anapata huduma zote za
kibinadamu chini ya kibanda kidogo kilichopo chini ya mwembe nyumbani
kwao, ameonekana kudhoofika na kutoa harufu mbaya kutokana na
kutoogeshwa kwa muda mrefu. Taarifa za kufungwa kwa kijana huyo zilisikika
kutoka kwa wakazi wa eneo hilo na mwandishi wetu alifika eneo hilo na
kushuhudia jinsi alivyofungwa na kuishi katika mazingira machafu.
Kijana huyo anakula na kujisaidia hapohapo, jambo
ambalo limeelezwa na baadhi ya wakazi wa eneo hilo kuwa ni la
unyanyasaji na hatari kwa afya yake.
Wakizungumza jana, wakazi wa eneo hilo walisema
kijana huyo alifungwa mnyororo huo kwa zaidi ya miaka mitatu huku akiwa
analala kwenye kibanda kidogo ambacho si salama kwake. Mmoja wa wakazi
hao, Imelda Saburi alisema wanaona uchungu kwa kitendo cha wazazi hao
kumfunga mnyororo kijana huyo huku akipata maumivu makali yanayomfanya
awe analia kwa sauti kila siku usiku.
Alisema walijaribu kuwashauri wazazi hao wamfungue
mnyororo huo na wampeleke hospitalini kupata huduma za afya lakini
walikataa. “Tulimfuata baba wa mtoto huyo na kumshauri amfungue hiyo
minyororo lakini alikataa ushauri wetu,” alisema Saburi.
Mkazi mwingine, Hassan Abdul alisema,
wanashangazwa na wazazi hao kutojali huku wakimtenga na kumlaza nje
akinyeshewa na mvua na kupigwa na jua.
Wazazi wajitetea
Mama mzazi wa kijana huyo, Zuena Ngarima alisema
walilazimika kumfunga mnyororo mguuni kwa kuwa amekuwa akifanya fujo na
kuharibu vitu mbalimbali vya wakazi wa eneo hilo. Alisema mwaka 2009, kijana huyo alianza
kuchanganyikiwa na walimpeleka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MHN)
na alilazwa kwa siku 19, alipopata nafuu aliruhusiwa kurudi nyumbani.
Ngarima alisema wakati kijana huyo akipata ugonjwa
huo, baba yake mzazi alikataa kumpeleka hospitalini akidai atapona,
ndipo alipoamua kuwafuata ndugu zake na kumlazimisha amchukue ili
akapatiwe matibabu. “Mwanangu amelazwa Muhimbili mara tatu lakini baba
yake haonekani na huwa hachangii na kuniachia peke yangu nikimuuguza.”
Alisema kutokana na kukosa mtu wa kumsaidia
kumhudumia kijana huyo, analazimika kutombadilisha nguo zilizochafuka
kwa haja ndogo na kubwa jambo ambalo limemfanya awe anatoa harufu kali.
CHANZO: MWANANCHI
Alisema yeye na baba wa mtoto huyo waliachana kutokana na
matatizo ya kijana huyo, hivyo inampa wakati mgumu kumhudumia kijana
huyo kutokana na kukosa fedha.
“Nina wakati mgumu sana. Kijana wangu hana mtu wa
kumhudumia, hivyo ninalazimika kutoa hela siku mojamoja aweze kunyolewa
nywele na kubadilishwa nguo,” alisema. Baba wa mtoto huyo, Mansuri Mchoi
alidai kwamba mtoto huyo alianza kuchanganyikiwa baada ya kuvuta bangi,
hivyo walimshauri asitumie kilevi hicho lakini alikuwa anaendelea.
Alisema baada ya kumtibu bila mafanikio,
walikubaliana yeye na mama wa mtoto huyo wamfunge mnyororo huo ili asiwe
mbali na wazazi kwa kuhofia kuharibu vitu vya watu. “Tuhuma ninazopelekewa kuwa simtibii si za kweli.
Huyu ni mtoto wangu ninamhangaikia sana aweze kupona, kama kuna mtu
atajitokeza kumponyesha nipo tayari,” alisema.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbondole, Thomas Nyanduli
alisema ofisi yake imewaita wazazi hao ili kuchukua maelezo yao na
baadaye hatua za kisheria zichukuliwe. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Merry Nzuki
alisema hajapata taarifa juu ya tukio hilo na kuahidi kutuma askari wake
kulifuatilia.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment