Social Icons

Pages

Tuesday, March 31, 2015

UJENZI WA VYUO VYA VETA KILA WILAYA UMEYEYUKA?


Unapoangalia idadi ya wanafunzi wanaotoka elimu ya msingi kwenda madaraja ya juu, hukosi kugundua kuwapo kwa tofauti kubwa ya kiidadi.
Ilivyo ni kuwa, kadri wanafunzi wanavyozidi kupanda madaraja ya elimu ndivyo idadi yao inavyopungua. Tuangalie mfano ufuatao.
Mwaka 2009 wanafunzi waliomaliza elimu ya msingi walikuwa 999,070 miaka minne baadaye waliohitimu kidato cha nne  walikuwa 404,083 
Hii ndiyo hali halisi nchini. Hata hivyo,  katika jamii kuna fursa nyingi ambazo wale wanaoshindwa kujiendeleza kielimu wanaweza kuzitumia zikawasaidia kimaisha, lakini pia zikawa chachu ya baadaye kuendelea katika taaluma hadi madaraja ya juu.
Fursa hizi zipo katika sekta kama kilimo, madini, uvuvi, ufugaji, biashara na aina mbalimbali za ufundi. Sekta hizi zinaweza kuwa mkombozi  kwa  vijana wa Kitanzania wanaokosa fursa  kujiendeleza kwenye  masomo ya kitaaluma.
Kwa Tanzania ili wanafunzi hawa waweze kunufaika na fursa hizi ni kwa kuitumia nafasi za mafunzo ya ufundi kupitia vyuo vinavyosimamiwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta).  Mafunzo haya yana faida kubwa kwa wanafunzi hawa
Kwa mfano, mwishoni mwa 2013, Veta ilifanya utafiti na kubaini ajira kwa wanafunzi waliosomea mafunzo ya ujasiriamali katika vyuo hivyo ziliongezeka kutoka asilimia 66.1 hadi 77 mwaka 2014.
Vyuo vya ufundi kila wilaya
Kutokana na kukua kwa mahitaji ya mafunzo ya ufundi, Veta ilizindua mpango mkakati wa miaka mitano, kuanzia mwaka 2012/13 mpaka 2016/17 uliozimia kujenga vyuo vya ufundi katika kila wilaya nchini (sawa na vyuo 127 kwa wakati huo) ili kuokoa vijana waliokosa nafasi ya kuendelea na masomo ya sekondari.
Hata hivyo, kukiwa kumebaki miaka mitatu sasa, Meneja Uhusiano wa Mamlaka hiyo, Sitta Peter anasema mpango umeshafanikisha ujenzi wa chuo kimoja tu kilichopo wilayani Makete.
Anasema sababu za kuwa na kasi ndogo ya utekelezaji wake, ni kutokana na bajeti ndogo inayotengwa na Serikali. Hata hivyo, anaongeza kusema kuwa baadhi ya vyuo viko katika hatua ya ujenzi. Vyuo hivyo vipo katika wilaya za Namtumbo, Ludewa, Chunya, Karagwe, Korogwe na Kilindi.
Sitta anasema Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato nchini(TRA), inatakiwa kuongeza kiwango cha cha tozo kwa waajiri (SDL), kinacholipwa kwenye mfuko wa mafunzo ya ufundi stadi kutoka asilimia tano ili kisaidie kufanikisha lengo hilo.
“Lakini hata kama hatutafanikiwa kutekeleza ndani ya muda tuliopanga, bado ujenzi utaendelea kufanyika. Kinachotakiwa ni fedha na ardhi ya kujenga vyuo hivyo,” anaeleza.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi kutoka TRA, Richard Kayombo anasema mamlaka hiyo kazi yake ni kukusanya mapato tu na siyo kufuatilia utekelezaji wa matumizi ya fedha hizo.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiah Oluoch anasema kama Serikali ingekuwa na nia ya dhati kujenga vyuo kila wilaya, hatua hiyo ingeweza kutekelezwa kwa bajeti ya mwaka mmoja tu. Anasema pamoja na kuvunja sheria ya matumizi ya fedha hizo, bado ingeweza kujenga vyuo vya Veta katika wilaya zote za Tanzania bara.
“ Kwa mujibu wa sheria, Veta ilitakiwa kiwango hicho cha fedha kipelekwe kwenye matumizi ya kuinua vyuo vya ufundi tu, lakini kwa sasa hivi wanakata mishahara ya watumishi wa vyuo vikuu ikiwa ni kinyume cha sheria ya kodi,” anasema na kuongeza:
“Lakini pamoja na mgawanyo huo, vyuo 300 vingeweza kujengwa kwa gharama ya Sh2 bilioni kila wilaya ili kuwafikia vijana waliokosa elimu ya taaluma na kunufaika na fursa za mazingira yanayowazunguka.”
Oluoch anasema kwa sasa kuna wastani wa vijana zaidi ya 300,000 , wanaokosa nafasi ya kujiunga na Veta, kwa sababu ya gharama zinazotozwa pamoja na kukosekana kwa vyuo hivyo katika wilaya zao.
“Kwa hivyo napendekeza kuongeza Veta hizo ili kuwafikia hao vijana lakini wabadilishe ratiba ya kuanza msimu wa masomo yao kwa sasa. Pia waondoe mitihani kwa wanafunzi wanaohitaji kujiunga na badala yake waunganishwe moja kwa moja wale wanaopenda kujaza kwenye fomu za mitihani ya kuendelea na masomo kidato cha tano.”
Mbunge wa jimbo la Nzenga, Dk Khamis Kigwangalla anasema katika jimbo lake hakuna Veta hata moja jambo ambalo linatishia ukuaji na ustawi wa jamii kwa jamii hiyo. Anasema mpaka sasa kuna fursa nyingi zinazopatikana katika jimbo lake, lakini kwa kukosekana kwa chuo hicho kumesababisha vijana wengi kukosa mbadala wa ajira za kujiajili.
“Veta inahitajika kwa kiwango kikubwa ukilinganisha na huduma nyingine katika upanuaji wa fursa na ukuzaji wa soko la ajira kwa vijana, kwa hivyo juhudi zinahitaji zaidi.”

Mkakati wa Serikali
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa kupitia hotuba ya bajeti ya mwaka 2014/15, alisema juhudi za ujenzi wa vyuo unaendelea na kuwa mpaka wakati huo, ujenzi wa chuo kipya cha Wilaya ya Makete ulikuwa umekamilika kwa asilimia 98, huku udahili wa wanafunzi ukiongezeka kutoka 53,233 mwaka 2005/2006 hadi kufikia 112,447 mwaka 2011/2012.
Naye Naibu wake, Anne Kilango anasema bado Serikali ina mpango wa kuendelea na ujenzi wa vyuo vya ufundi kwa kila Wilaya. Hata hivyo, anakiri kuwa umekuwa ukisuasua kutokana na ujenzi wake kuwa wa gharama kubwa.
Kilango alitoa kauli hiyo Bungeni Machi 19 alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Chakechake, Masoud Abdallah Salim aliyetaka kujua utekelezaji wa ahadi ya Serikali kujenga chuo cha Veta kila Wilaya.
Wakati huohuo hivi karibuni, Serikali imezindua Sera mpya ya elimu inayoelekeza kwamba, Serikali itaweka utaratibu utakaowezesha kuwaendeleza kimafunzo wanafunzi wenye vipaji na vipawa mbalimbali
Aidha, Serikali imeahidi kuweka utaratibu na kuimarisha utambuzi wa maarifa, ujuzi na stadi nje ya mfumo wa shule ili kupanua fursa za kujiendeleza kielimu.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: