Social Icons

Pages

Tuesday, March 31, 2015

TUWAANDAE KUWA WAKAKAMAVU WA MWILI AU AKILI?


Lugha inayotawala sasa kwa vijana wengi ni kukosa ajira, kukosa kazi. Na kubwa zaidi Serikali inalaumiwa kwa kuwanyima ajira vijana.
Vijana waliotoka JKT juzi juzi walidiriki kuandamana kuishinikiza Serikali iwaajiri. Maana wana haki ya ziada kuajiriwa na Serikali baada ya kupata mafunzo ya ukakamavu wa mwili jeshini. Pengine inawezekana ni kweli!
Wakati mtazamo wa vijana kulalamikia kukosa ajira ukizidi kukua na kushamiri kwa wengi. orodha ya ajira na nafasi za kazi zinazotangazwa kwenye mitandao ya kijamii, kwenye tovuti za ajira na magazetini ni nyingi.
Wageni na wakakamavu wa akili wanazichangamkia fursa hizo na wanaajiriwa na kuwaacha vijana wanaendelea kulalamika hawana kazi.
Nimewahi kusema huko nyuma kuwa pamoja na kwamba Tanzania yetu Mungu alitujalia rasilimali kama misitu, vipaji mbalimbali kwa watu, wanyama pori na ardhi kubwa na yenye rutuba, bado kuna Watanzania wanasimama kwa ujasiri na kutamka kuwa “hawana kazi”
Tunalalamika hatuna kazi na lazima Serikali ituajiri. Kwa mtazamo wangu ni kosa kubwa. Tunajichelewesha wenyewe kimaendeleo.
Madhara ya mtazamo huu ambao umejengeka kwa kasi nchini kwetu ni kwamba, vijana wengi hawajishughulishi kufikiri, kuthubutu wala kujituma, wanashinda vijiweni wakisubiri ajira za serikalini. Na wachache wanaoajiriwa hawawezi kazi na hawapendi kazi, wengi wanafukuzwa kazi kwa sababu ya uvivu na uzembe.
Vijana sasa wanatamani mafanikio kwa njia ya mkato, ndiyo maana wanajiunga na vikundi vibaya ili kupata utajiri wa muda mfupi. Hawajitumi kufanyakazi wala kubuni fursa za kujiendeleza, wanatumiwa na wanasiasa kuivuruga nchi na kuwaingiza wenye pesa madarakani.
Nguvu kazi ya Taifa maana yake ni vijana walioandaliwa kuijenga nchi. Vijana wakakamavu wa kufikiri, kuchangamkia fursa, kubuni fursa na kufanya kazi kwa bidiii. Vijana wenye uzalendo wa kujenga nchi yao. Vijana wanaojitambua wao ni kina nani wana wajibu gani kwa familia na Taifa lao. Vijana wanaofanya bidii kuzalisha na kuijenga nchi.
Wasiotumiwa na wanasiasa au watu fedhuli kubomoa umoja wa kitaifa na kuingiza wezi madarakani. Hawa ndio vijana wakakamavu. Bahati mbaya, bundi ameingia kwenye umaizi wa vijana. Sasa vijana wengi wanatamani kufanya mazoezi ya viungo ili watumiwe na makundi mabaya.
Hata waliokuwa JKT walidhani wakipata mazoezi ya viungo tayari wana sifa ya kuajiriwa popote wakati wowote. Wakasahau kuwa dunia ya leo ukakamavu wa viungo siyo sifa ya kuwa askari hodari. Hata majeshi yenye mafanikio hayategemei ukakamavu wa viungo vya askari wake. Siku hizi hata ulinzi wa nchi ni sayansi, ni ujuzi, ni maarifa ni teknolojia. Ndiyo maana kuna ndege za kivita na nyingine hazina hata rubani!
Vijana wenzangu elimu unayopata ndiyo ukakamavu muhimu wa kukutoa kimaisha. Vipaji ulivyo navyo ndiyo mtaji wa kukuletea mafanikio haraka. Fursa zinazokuzunguka ndiyo mtaji wa kukuendeleza kwa haraka.
Fursa za utandawazi ni mlango wa kutokea kwenye umaskini. Tukijifanya sisi ni walalamikaji maarufu duniani tutabaki hivyo; na nchi yetu itaporwa na wageni wanaoziona fursa. Tutabaki mateka wa fikra na matendo yetu ya kinyonge. Tutabaki watumwa wa mitazamo hasi na uzandiki wa wanasiasa.
Hata hao wanaotutumia walikuwa vijana na wana fursa nyingi walizotengeneza. Unashindwaje kupiga hatua kama kijana unayejitambua kwa nafasi yako?
Vijana hatuthamini muda japo ‘’muda ni mali’’. Tunapoteza muda mwingi kwa mambo ya ovyo na starehe za ajabu, badala ya kuzalisha. Unakuta vijana wenye nguvu na elimu wanakaa kijiweni au kwenye baa saa tatu hadi tano kwa siku wakipiga porojo na kunywa.
Wengine wanachezea muda hata wakiwa ofisini. Kijana huwezi kuendelea pasipo kujali na kuukomboa muda. Kila dakika iwe na thamani kwako. Inafaa ujiulize umetumiaje saa 12 za mchana wote? Kuna chochote kimefanyika ndani ya siku moja?, ndani ya wiki? ndani ya mwezi? Jaribu kutathimini muda unaotumia kufanya mambo ya ovyo au kustarehe na linganisha na thamani ya muda kwa tukio moja.
Kwa vijana, ukakamavu wa akili kujenga nidhamu ya matumizi ya fedha na rasilimali tulizo nazo. Kila senti itumike kwa tija. Bila kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha na rasilimali tunaweza kuweka bidii kubwa ya kufanya kazi lakini mapato yote yanaishia kwenye ubadhilifu.
Fikiria: kijana anapata mshahara wa Sh 250,000, anatumia kwenye klabu ya pombe Sh 5,000 kila siku, na kununua vifurushi vya kuchati kwenye mitandao. Kwa mwezi, anajikuta pesa yake imemtajirisha mwenye baa na kampuni ya simu. Starehe zinafuja fedha kwa kuwa huambatana na vitu vingi ambayo vinahitaji pia kutumia fedha. Nidhamu ya matumizi ya fedha na rasilimali ni muhimu kama tunahitaji maendeleo ya kweli. Watu wenye maendeleo wana nidhamu kwenye matumizi ya fedha.
Ukakamavu wa akili kwa vijana ni kuchangamkia fursa na kuongeza ujuzi. Katika mafanikio kinachowafanya wengi washindwe ni kukosa ujuzi wa kutosha. Tunaposema ujuzi hatumaanishi kwenda shule na kupata vyeti pekee japokuwa nayo ni hatua ya kupata ujuzi.
Ujuzi ni zaidi ya mtu kuwa na vyeti, ujuzi ni zaidi ya maarifa, ujuzi ni uwezo wa kutenda na kuleta matokeo chanya kama ilivyokusudiwa au zaidi ya kilichotarajiwa. Katika mbio za mafanikio kinachouzika ni ujuzi siyo maarifa ya nadharia wala utaalamu wa kulalamika na kuomba kusaidiwa.
Wapo watu wengi ambao wamesoma na wana vyeti vizuri lakini hawana mafanikio, hakuna uwiano kati ya elimu yake na maisha yake kwa jumla. Mafanikio ni matokeo ya matumizi ya maarifa na ujuzi wa mtu katika shughuli zake na kuchangamkia fursa siyo kulalamika.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: