Meneja wa Maabara ya Buni Hub Jacquline Dismas akieleza namna
printa ya 3D inavyofanya kazi hivi karibuni. Huenda isiwe inafahamika na Watanzania wengi,
lakini mashine ya kwanza ya kuchapa vifaa vya maumbo mbalimbali, imeanza
kutengenezwa nchini.
Kwa mara ya kwanza Afrika Mashariki na Kati,
Printa inayochapa kitu katika pande tatu maarufu kwa kiingereza kama ‘3D
Printer’, imetengenezwa jijini Dar es Salaam katika kituo cha kukuza
ubunifu na ujasiriamali cha Buni Hub.
Printa hiyo, yenye uwezo wa kutengeneza vifaa
mbalimbali vya plastiki kutokana na usanifu wake, ilitengenezwa na timu
ya wataalamu wa elektroniki na teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(Tehama) baada ya kupatiwa ujuzi na mtaalamu kutoka Uingereza, Mathew
Rogge.
Kwa wengi waliozoea printa za kuchapa karatasi
watashangazwa na uwezo mkubwa wa printa hiyo inavyoweza kuuchapa mchoro
uliopo kwenye kompyuta hadi kuwa kifaa pasina kukosea.
Baada ya wiki tatu za kuitengeneza, printa hiyo
imeshatengeneza vifaa kadhaa vya plastiki vinavyoweza kutumika kama
vipuri kutengenezea mashine nyingine ya namna hiyo.
“Mashine hii tulioitengeneza kwa kutumia mabaki ya
vifaa vya elektroniki, inaweza kutengeneza vitu unavyoweza kuvishika na
kuvitumia katika kazi mbalimbali kama vikombe, midori, sampuli za
nyumba, viatu na vinginevyo,” anasema Meneja wa maabara ya Buni Hub,
Jacqueline Dismas. “Tunajaribu kwa hali na mali kuhakikisha mazingira
yetu ni safi kwa kupunguza taka ambazo zinaweza ama kutumika tena au
kutengenezwa upya.”
Ili kupata vifaa vya kuundia mashine hiyo, anasema
iliwahitaji kuzunguka kwenye vituo vya kukusanya taka za kielektroniki
kama printa, kompyuta na televisheni vilivyopo jijini hapa.
Matumizi ya taka hizo, zinazosaidia kupatikana kwa
mota, chanzo cha nishati ya umeme (power supply) na reli za kujengea
printa, yanasaidia kupunguza tatizo la taka ngumu na kujenga tabia ya
kutunza mazingira.
Tofauti na printa zinazochapa karatasi ambazo
hutumia wino kuchapa, printa za 3D zinatumia malighafi za plastiki,
chuma, udongo, na nyinginezo ziitwazo ‘filament’ kuzalisha bidhaa
tofauti kutokana na mahitaji.
Kuingia kwa teknolojia ya uundaji printa za 3D
hasa kwa kutumia taka za kielektroniki, kutapunguza gharama za ununuzi
wa mashine hizo zilizoanza kupata umaarufu ulimwenguni kwa kurahisisha
kazi lukuki ambazo awali zilifanyika kiwandani.
Matumizi shuleni
Kauli ya COSTECH
CHANZO: MWANANCHI
Kwa mujibu wa Jacqueline, baada ya kupata taaluma ya kuunda
mashine hizo wana mipango mbalimbali ya kutengeneza bidhaa muhimu kwa
jamii ambazo zimekuwa vigumu kupatikana sokoni. “Moja ya miradi tunayotarajia kupitia printa za 3D ni kuanza kutengeneza vifaa vya kufundishia katika shule zote Tanzania.
“Hivi sasa shule zote za kata za sekondari zina
maabara lakini zinakabiliwa na vifaa vidogo vidogo vya mazoezi kama gia
katika somo la Fizikia ambavyo vinaweza kuzalishwa na mashine hizo,”
anasema.
Anabainisha kuwa vifaa kama moyo au ubongo wa
binadamu unaotumika kufundishia somo la Bailojia pia vinaweza
kutengenezwa kirahisi.
Wastani wa bei ya Printa moja ya 3D ya kiwango cha chini ni takriban Sh2.5 milioni iwapo utaiagiza nje ya nchi. Hata hivyo, kiongozi wa timu iliyotengeneza
mashine hiyo Stanley Mwalembe, anasema gharama za jumla ya uundaji
mashine waliyointengeneza zinafikia kati ya Sh150, 000 hadi 200,000.
Licha ya kwamba kwa sasa hawajaanza kuzalisha kwa ajili ya biashara, anaeleza kuwa bei ya reja reja inaweza isizidi Sh350, 000. Mafanikio ya uingizaji wa teknolojia hiyo unafungua ukurasa mpya wa kuimarisha mfumo wa uchumi wa kibunifu na viwanda.
‘’Iwapo printa hizo mpya zikizalishwa kwa wingi
zitatoa fursa lukuki kwa wajasiriamali wadogo kutengeneza bidhaa zao
majumbani,’’ anabainisha Mwalembe.
Baada ya kupata teknolojia hiyo, Mwalembe ambaye
pia ni mhadhiri wa Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam, (DIT) anasema
wataanza kuzalisha printa za 3D kwa ajili ya kuuza reja reja kuwasaidia
wajasiriamali. “Mradi wa kwanza tunaoufikiri ni kuanzisha
uzalishaji wa chupa ndogo za plastiki kwa kutumia mashine hizi hali
kadhalika kuandaa malighafi (filament) inayotumika katika uzalishaji wa
chupa hizo,” anaongeza. Kwa sasa, anasema wanaweza kutengeneza printa hizo
kwa oda maalumu na karakana yao ya nje ya kituo cha Buni ina uwezo wa
kuzalisha hadi printa 500 za 3D kwa mwaka.
Kauli ya COSTECH
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia
(COSTECH), DK Hassan Mshinda anatoa hofu kwamba nia yao ni kuzitengeneza
printa hizo na kuzigawa katika vyuo mbalimbali ili wanafunzi nao
wajifunze kuzitengeneza. “Sisi tunatazamia zaidi kuzalisha vitu vingine
kama ‘drone’,” Drone ni ndege ndogo zisizo na rubani zinazotumika
kufanya kazi tofauti ikiwemo kubeba mizigo, kupiga picha, ulinzi, na
kazi nyinginezo,’’ anaeleza.
Kwa sasa, anabainisha kuwa wanataka kusambaza
elimu ya teknolojia hiyo kwa wananchi waielewe, ili iwe rahisi kutumia
fursa za mashine hizo kufanya ujasiriamali. “Tunaamini vijana wengi watajifunza na hatuwezi
kuepuka teknolojia hii kwa sababu ulimwengu wa viwanda unaelekea katika
uzalishaji kwa kutumia printa za 3D,” anabainisha huku akisema zama za
viwanda vinavyotoa moshi zimepitwa na wakati.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment