Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika
Wakati leo Serikali
ikiwasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao wa mwaka
2015, wadau wanaotumia mitandao nchini wameupinga kwa madai kuwa
hawakushirikishwa na muswada huo unalenga kudhibiti mawasiliano ya
wananchi wenyewe kwa wenyewe.
Wamesema makosa yaliyoainishwa katika muswada huo
ambao kama utapitishwa leo na kuwa sheria, yanaweza kuwabana watu ambao
hawahusiki. Baadhi ya makosa yaliyoanishwa katika sheria hiyo
ni pamoja na kutuma taarifa bila ridhaa ya mtu, kusambaza picha za ngono
na za utupu, udanganyifu unaohusiana na kompyuta, makosa yanayohusiana
na utambuzi, kughushi kunakohusiana na masuala ya kompyuta na kusambaza
picha za utupu za watoto.
Mengine ni unyanyasaji kwa kutumia mtandao,
kuchapisha taarifa yoyote ambayo itasababisha mauaji ya kimbari, uongo
na matusi ya kibaguzi, huku adhabu kali ikiwa ni faini ya Sh50 milioni
au kifungo kisichopungua miaka saba, kwa mtu atakayebainika kusambaza
picha za ngono mtandaoni.
Malalamiko kama hayo yaliwahi pia kutolewa na
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika aliyeitaka Serikali ikusanye
maoni ya wadau kabla ya kuwasilisha muswada huo kwa hati ya dharua
kutokana na umuhimu wake kwa jamii. Kupitia tamko lao lililotolewa na Taasisi ya
Sikika, wadua hao wamesema muswada huo una mapungufu kama utapitishwa na
kuwa sheria.
Wamedai kuwa unaweza kuifanya Tanzania ikawa ni
kati ya nchi adui wa matumizi ya mtandao wa Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (Tehama). “Sheria hii itamuathiri mtu yeyote anayeweza
kutumia mtandao wa intaneti kwa kutumia kifaa chochote iwe kompyuta
kubwa au vifaa vyenye uwezo wa kufanya kazi kama kompyuta kama simu za
kiganjani, televisheni na vifaa vingine vinavyoendana na hivyo,”
limeainisha tamko hilo.
Wakibainisha kasoro za muswada huo, walisema,
“Ibara ya 7 (1-3) haibainisha ni aina gani ya data ambazo haziruhusiwi
kuguswa, kufutwa au zikiguswa, kufutwa ni kosa la jinai.”
Pia, wamedai kuwa muswada huo haujaweka bayana
adhabu itakayotolewa iwapo nyaraka za siri zinaweza kuwekwa wazi katika
mtandao kama zina maslahi ya nchi au wananchi kutolea mfano matumizi
mabovu ya pesa za umma. “Neno pornografia (picha za utupu) halijapewa
maana na hivyo jambo lolote lenye mwonekano wa kiasherati (sexually
vulgar) linaweza kutafsiriwa kama pornografia na kumuingiza muhusika
matatizoni,” limeainisha tamko hilo.
Imefafanua kuwa Ponografia ya mtandao isikatazwe kabisa ila
inatakiwa kuweka ulinzi thabiti wa kuhakikisha watoto hawawezi kufungua
mitandao ya aina hiyo, “Ponografia zote ni chafu, lakini sio chafu zote
ni ponografia.”
Linasema kuwa suala la kujifanya mtu mwingine kwenye mtandao, linaweza kuleta utata.
Wameiomba Serikali iuondoa ili kuepusha nchi kuwa na sheria kandamizi.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment