Social Icons

Pages

Tuesday, March 31, 2015

UJENZI RELI YA KATI UTATUKOMBOA KIUCHUMI


Kama kuna mradi hapa nchini ambao umezungumzwa kwa muda mrefu pasipo kutekelezwa, basi mradi huo ni ujenzi wa Reli ya Kati. Kwa zaidi ya miongo miwili sasa, viongozi wamekuwa wakitoa ahadi za ujenzi wa reli hiyo na kutoa matumaini kwa wananchi kwamba kero ya usafiri wa abiria na mizigo katika reli hiyo itamalizika muda siyo mrefu.
Ahadi hiyo ilianza kutolewa wakati wa Serikali ya Awamu ya Pili, ikaendelea katika awamu ya tatu na ikawa hivyo pia katika awamu hii ya nne iliyopo madarakani hivi sasa.
Ilifika wakati ahadi hizo zikachukuliwa na wananchi kama simulizi na ngonjera zisizokwisha. Kuanzia wakuu wote wa nchi katika awamu hizo tatu hadi mawaziri wao wakuu na mawaziri walioiongoza wizara husika, kila mmoja aliahidi Serikali yake ingejenga reli hiyo. Mara ya mwisho kutolewa kwa ahadi hiyo ilikuwa Julai, mwaka jana wakati Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiwa ziarani Uingereza, aliwaambia Watanzania wanaoishi nchini humo kwamba Serikali sasa ilikuwa imedhamiria kuwekeza katika mradi mkubwa wa ujenzi wa Reli ya Kati ambao ungegharimu Sh11.4 trilioni na kukamilika baada ya miaka minne.
Alisema uzinduzi wa mradi huo ungefanyika Desemba, mwaka jana na kwamba reli hiyo ingejengwa upya badala ya kubanduabandua mataruma ya reli hapa na pale.
Sasa inaonekana dhahiri kwamba ndoto ya Serikali ya muda mrefu iko mbioni kutimia. Tunaweza kusema ‘hayawi hayawi sasa yamekuwa’, kutokana na Serikali juzi kutangaza mpango kabambe wa ujenzi wa mradi mkubwa wa reli mpya ya kati itakayogharimu Sh14 trilioni. Pamoja na kutoweka wazi sababu za kuchelewa kuanza ujenzi wa reli hiyo, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta alisema jiwe la msingi la ujenzi wa reli hiyo itakayokuwa na urefu wa kilomita 2,561 litawekwa na Rais Jakaya Kikwete, Juni 30, mwaka huu.
Hata hivyo, imekuwa ikihofiwa kwamba kukwama kwa ujenzi huo kulitokana na ukosefu wa fedha. Waziri Sitta sasa anasema mradi huo mkubwa kuliko yote tangu Uhuru utagharimiwa na mabenki yapatayo 100 na kwamba Serikali haitatoa hata senti moja kutoka Hazina. Reli hiyo itatoka Dar es Salaam kwenda Mwanza kupitia mikoa ya kati kuelekea Isaka hadi Burundi.
Pengine wakati tukifurahia ujio wa mradi huo na kuzungumzia maendeleo yatakayotokana na reli hiyo, ingekuwa vyema tukasisitiza kwamba kuna umuhimu kwa Serikali kujipanga vyema na kuweka mipango thabiti ya usimamizi wa mradi huo na kuhakikisha utekelezaji wake unakamilika katika muda uliopangwa. Mradi huo ni ukombozi mkubwa wa nchi yetu kiuchumi, mbali na ukweli kwamba utatoa ajira kwa wananchi wengi wakati wa ujenzi na baada ya kukamilika.
Tunaipongeza Serikali kwa kufanya uamuzi huo ambao utamaliza uharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara zetu uliokuwa ukisababishwa na malori ya mizigo. Uamuzi huo umezingatia masilahi ya Taifa, kwani zimekuwapo hisia kwamba ucheleweshaji wa mradi huo huenda ulisababishwa na baadhi ya viongozi na wafanyabiashara ambao waliona usafiri wa Tazara na Reli ya Kati kama tishio kwa biashara yao ya usafirishaji wa abiria na mizigo.
Ni matarajio yetu kwamba Serikali itahakikisha kwamba reli hiyo inajengwa, huku ikitambua kwamba wapo watu watakaofanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba mradi huo kamwe haufanikiwi.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: