Wafaransa wanyamaa kimya kwa dakika moja kuwakumbuka wahanga wa shambulio la Charlie Hebdo. Kengele zimepigwa katika kanisa katoliki la Notre Dame mjini Paris,
wakati raia wa Ufaransa walipowakumbuka wahanga wa shambulizi la kigaidi
katika ofisi ya jarida la Charlie Hebdo.
Raia hao wamekusanyika katika makao makuu ya ofisi ya jarida la tashtiti
la Charlie Hebdo, kuweka maua na kutoa heshima zao mahali kulikotokea
shambulizi la kigaidi hapo jana. Bendera nchini humo zilipepea nusu mlingoti, ishara ya kuomboleza vifo
vya watu 12 waliouwawa hapo jana. Watu hao ni pamoja na waandishi wanane
wa habari, maafisa wawili wa polisi, mfanyakazi mmoja na mgeni
aliyetembelea ofisi hiyo.
Raia waliokuwa katika eneo hilo
waliweka kalamu, kuwasha mishuma na hata vijikaratasi vilivyokuwa na
ujumbe wa huzuni na kulaani kitendo hicho. Mwanamke mmoja alisema kwa
sauti “Mshikamano na Uhuru” huku akibubujikwa na machozi. Na ilipofika
saa sita juu ya alama hivi ndivyo hali ilivyokuwa nchini Ufaransa.
Wafaransa walinyamaa kwa dakika moja kuwakumbuka wahanga wa shambulio
hilo la kigaidi. Baadaye raia hao waliimba wimbo wa taifa, huku wakilia,
wengi wakiwa na kalamu na penseli ishara ya wachora vibonzo waliolengwa
katika shambulio hilo. Wakati huo huo Rais wa Ufaransa Francois Hollande amewataka wananchi
kuungana dhidi ya ugaidi na kutovumiliana. Rais Hollande pia ameongoza
mkutano wa dharura uliohudhuriwa na Rais wa zamani Nicholas Sarkozy,
Waziri Mkuu Manuell Valls, Viongozi wakuu wa Usalama pamoja na viongozi
wengine wa juu serikalini. Naye Pierre Desirat, mkaazi wa Paris aliye na miaka 48,
amesema amesikitishwa na tukio la jana na amejitokeza kuonesha
mshikamano kwa raia wenzake wa Ufaransa. "Nimekuja hapa kuwa pamoja na wenzangu kuonesha mshikamanokwa jarida
hili, waandishi habari, na polisi na Ufaransa yote kwa Ujumlana
ilioumizwa kutokana na tukio la jana. Nimekuja tu kama raia wa kawaida,"
alisema Pierre Desirat.
Bado hali niya wasiwasi nchini Ufaransa.
Huku hali ya wasiwasi ikiendelea kutanda nchini humo, polisi wanaendelea
kuwatafuta ndugu wawili wanaoaminika kujihami kwa silaha wanaohofiwa
huenda wakatekeleza shambulizi jengine la kigaidi. Wanaume hao Cherif Kouachi,aliye na miaka 32 na kakaake Said Kouachi
aliye na miaka 34 wanaaminika kutekeleza shambulizi dhidi ya jarida la
Charlie Hebdo kutokana na gazeti hilo kuwahi kuchora kibonzo
kilichomkejeli au kumtashtiti mtume wa dini ya kiislamu, mtume Mohammed. Wakati hayo yakiarifiwa Serikali ya Uingereza imesema
imeimarisha zaidi usalama katika mipaka yake ikiwemo katika bandari na
vituo vya ukaguzi maeneo wanayofanyia kazi nchini Ufaransa, kutokana na
shambulio la kigaidi, naye kiongozi wa kanisa katoliki Papa Francis,
ameongoza ibada ya misa ya kuwakumbuka wahanga wa shambulio hilo huku
akikemea ukatili dhidi ya binaadamu. Aidha hii leo kumekuwa pia na taarifa za mashambulizi mengine dhidi ya
polisi kusini mwa Ufaransa, ambako watu waliokuwa kwenye gari wamewapiga
risasi polisi wawili na kumuua mmoja wa kike. Waendesha mashtaka nchini
humo wamesema wanalichunguza tukio hilo kama tukio la kigaidi.
CHANZO: DW KISWAHILI
No comments:
Post a Comment