Mfumo huo wa RH yamegawanyika zaidi katika makundi
madogo kama vile kundi A (hasi), kundi A (chanya), kundi B (hasi),
kundi B (chanya), kundi AB (hasi), kundi AB (chanya), kundi O (chanya)
na kundi O (hasi). Binadamu yeyote lazima awe mojawapo ya makundi hayo.
Historia inaonyesha kuwa makundi haya ya damu
yaligundulika kutokana na jitihada za wataalamu wa tiba za kujaribu
kuokoa maisha ya wagonjwa waliokuwa wanapungukiwa damu. Wataalamu hawa walipojaribu kuwaongezea watu damu
za wanyama au za binadamu wengine, mara nyingi walipoteza maisha na hii
ilichochea udadisi ili kujua zaidi kuhusu damu. Tofauti za makundi yetu ya damu zinatokana na urithi wa vinasaba vinavyotofautiana kutoka kwa wazazi wetu.
Kwa mujibu wa J.R. Storry na M.L. Olsson katika
utafiti wao uliochapishwa katika jarida la kisayansi la Immunohematology
toleo la 25 mwaka 2009, vinasaba vya urithi vinaweza kuamua kuwepo kwa
tofauti za makundi ya damu kwa kutengeneza mifumo tata na iliyo tofauti
ya kinga dhidi ya magonjwa katika ukuta wa nje wa chembechembe nyekundu
za damu.
Hata hivyo kila kundi lina faida na hasara zake
pale tunapoyahusisha makundi ya damu na uwezekano wa kuchangia kutokea
kwa magonjwa au kutukinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza na magonjwa
ya kuambukiza. Kwa kipindi cha takribani miaka 20 sasa,
wanasayansi wa maswala ya afya na tiba wamekuwa wakifanya tafiti
mbalimbali kuhusiana na uwezekano wa makundi mbalimbali ya damu
kuchochea au kuzuia utokeaji wa magonjwa kadhaa ambayo binadamu anaweza
kuyapata.
Ushahidi wa tafiti nyingi umeonyesha kuwepo kwa mahusiano ya karibu baina ya makundi ya damu na hali ya afya ya mtu. Katika utafiti wa hivi karibuni ulio ongozwa na
N.A. Zakai wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Vermont nchini Marekani na
kuchapishwa katika jarida la kitabibu lijulikanalo kwa jina la Journal
of Thrombosis and Haemostasis toleo la 12(4) la mwaka huu, ilibainika
kuwa watu wenye kundi la damu la AB wanakabiliwa na uwezekano mkubwa wa
kupata ugonjwa wa kiharusi.
Katika utafiti mwingine wa mwaka 2006 ulioongozwa
na Siripen Kalayanarooj wa Taasisi ya Afya ya Watoto ya Malkia Sirikit
ya nchini Thailand (Queen Sirikit National Institute of Child Health,
Bangkok, Thailand ), pia ilibainika kuwa watu wenye kundi la damu la AB,
wako katika hatari kubwa ya kupata homa ya Dengue kuliko watu wengine. Utafiti huo ulichapishwa kwenye jarida la magonjwa ya kuambukiza (The Journal of Infectious Diseases) toleo la 195(7). Utafiti mwingine uliofanyika nchini Pakistan mnamo mwaka huu nao
ulionyesha kuwa watu wenye ‘kundi A la damu’ wako katika hatari kubwa
ya kupata magonjwa ya moyo. Ushahidi wa kisayansi pia unaonyesha kuwa kundi
hili la damu lina uhusiano wa karibu na ongezeko la lehemu mbaya
mwilini. Aina hii ya lehemu imekuwa ikihusishwa na kuziba kwa mishipa ya
damu na kusababisha magonjwa ya moyo, kiharusi pamoja na kupanda kwa
shinikizo la damu.
Kundi A pia limekuwa likihusishwa na ongezeko la
kutokea kwa saratani mbalimbali ikiwa ni pamoja na ya mishipa ya fahamu,
utumbo, mifuko ya mayai, mfuko wa kizazi na mlango wa kizazi kwa
wanawake. Lakini pia kundi hili limekuwa na uhusiano wa karibu na saratani za kibofu cha mkojo, figo, kongosho na tezi za mate. Utafiti mwingine wa hivi karibuni uliochapishwa
katika jarida la tafiti za afya la Journal of Clinical & Diagnostics
Research, ulibaini pia kuwa watu wenye kundi A la damu wako katika
hatari kubwa ya kupata saratani ya kinywa, tezi za mate na umio. Lakini
pia utafiti huo ulibainisha kuwa watu wenye kundi B wana hatari kubwa ya
kupata saratani ya koo.
Tafiti zingine zinabainisha kuwa watu wenye kundi A
na B, wana uwezo mkubwa wa kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu,
lakini pia watu wenye kundi AB wana uwezo mkubwa zaidi wa kukabiliana na
ugonjwa huo. Katika utafiti wake Dk Ali S.T. Al Ghamdi wa
Kitivo cha Sayansi za Tiba ya Kinywa na Meno katika Chuo Kikuu cha
Mfalme Abdulaziz Jeddah, Saudi Arabia yeye alibaini kuwa watu wenye
kundi B la damu wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata ugonjwa mkali
zaidi wa uvimbe wa fizi.
Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na Chuo Kikuu
cha Pennsylvania chini ya uongozi wa Dk Muredach Reilly uliowahusisha
washiriki 20,000 na ulibaini kuwa watu wenye kundi O la damu wenye
vinasaba ya kijenetiki aina ya Adamts7 hawana hatari kubwa ya kupata
ugonjwa wa shambulio la ghafla la moyo kama ilivyo kwa watu wenye
makundi mengine ya damu.
Hata hivyo baadhi ya watafiti wanaonyesha kuwa
watu wenye kundi la O hawana kinga ya kutosha dhidi ya kipindupindu
lakini wana kiasi fulani cha kinga dhidi ya Kifua Kikuu(TB), Malaria
isiyo kali, saratani za kongosho, tumbo, matiti na mlango wa kizazi. Watafiti wengine wanadai kuwa kundi hili la damu
huchochea kwa kiwango kikubwa kutokea kwa saratani za ngozi na uambukizo
wa bakteria aina ya Helicobacter pylori wanaosababisha vidonda vya
tumbo.
Uhusiano wa makundi ya damu na kutokea kwa aina
mbalimbali za saratani kwa mara ya kwanza ulielezwa na wanasayansi D.E.
Anderson na mwenzake C. Haas katika jarida la maswala ya saratani mwaka
1984. Utafiti mwingine wa hivi karibuni uliofanywa na
timu ya wanasayansi kutoka katika Chuo Kikuu cha Tiba cha Vermont nchini
Marekani nao ulibaini kuwepo kwa uhusiano wa kundi la damu la AB na
kupungua haraka kwa uwezo wa akili katika kufikiri unaowakabili wazee.
“Utafiti wetu ulikuwa unachunguza uhusiano uliopo kati ya
makundi ya damu na kupungua kwa uwezo wa kufikiri lakini tafiti nyingi
zimekwisha onyesha kuwa kuna mambo mengine yanayopunguza uwezo wa
kufikiri kama vile shinikizo la damu, ugonjwa wa kisukari na ongezeko la
lehemu mbaya mwilini” anasema Dk Mary Cushman, mmoja wa wanatimu wa
utafiti huo walioutoa mwaka huu.
Katika utafiti mwingine uliowahusisha wanawake
82,000 wa nchini Ufaransa, watafiti wanadai wamebaini kuwepo kwa hatari
kubwa zaidi kwa wanawake wenye damu kundi B kupata ugonjwa wa kisukari
aina ya pili ikilinganishwa na wengine wenye makundi tofauti ya damu. Utafiti huo ulioongozwa na Guy Fagherazzi, wa
Kituo cha Utafiti wa vyanzo vya Magonjwa katika Jamii (CREP) cha Taasisi
ya Gustave Roussy iliyoko Villejuif Ufaransa, ulibaini kuwepo kwa
ongezeko la asilimia 35 zaidi ya hatari hiyo.
Baadhi ya wasomi wameipokea taarifa ya utafiti huo
iliyochapishwa katika jarida la Diabetologia toleo la Desemba 18 mwaka
huu kwa hisia tofauti. Matatizo mengine ya kiafya ambayo yamekuwa yakihusishwa na makundi ya damu ni kuharibika kwa mimba au watoto kufia tumboni.
Hii inatokana na kutokupatana kwa makundi ya damu ya watoto na wazazi pamoja na uwezo wa kupata mimba kwa baadhi ya wanawake. Baadhi ya watafiti wanadai kuwa wanawake wenye
kundi O la damu wana uwezo mdogo wa kutunga mimba ikilinganishwa na wale
wenye kundi A. Katika utafiti mmoja uliowahusisha wanawake 560
walio katika umri wa kuzaa waliokuwa wanakabiliwa na tatizo la ugumba,
ilibainika kuwa wanawake wenye kundi O la damu walikuwa na uwezekano
mkubwa mara mbili zaidi ya wengine wa kuwa na mayai kidogo tena
yasiyokuwa na afya njema.
Akizungumzia hali hiyo mtafiti Edward Nejat wa
Chuo cha New York’s Albert anasema: “Sababu mahususi ya uhusiano wa
kundi la damu na uwezo mkubwa wa mifuko ya mayai kuwa na mayai ya
kutosha na yenye afya haikuwa bayana. “Kwa wanawake wenye kundi O wanaohitaji kupata
watoto, wanaweza kutumia matokeo ya tafiti hizi kuzaa mapema wakati
ambapo mifuko ya mayai inapozalisha mayai kwa wingi ili kuepuka tatizo
la ugumba linaloweza kujitokeza hapo baadaye.”
Mmoja wa watafiti wa maswala ya uhusiano kati ya
makundi ya damu na magonjwa kutoka katika Kitivo cha Afya ya Jamii cha
Chuo Kikuu cha Harvard, Profesa Lu Qi, anasema: “Ingawa watu hawawezi kubadilisha makundi yao ya
damu, utafiti wetu unaweza kusaidia madaktari kufahamu vizuri zaidi ni
mtu gani yuko kwenye hatari zaidi ya kupata aina ya ugonjwa fulani.” Ni vema kujua kundi lako la damu sawa na ilivyo vema kujua mambo
mengine yanayochangia kuwa na afya njema. Hii itakuza uwezo wako wa
kufahamu hatari zinazo kukabili kutokana na kundi la damu ulilo nalo na
kuepuka hatari hizo kwa kutumia mtindo wa maisha unaofaa.
Magonjwa mengi yanaweza kuepukwa kwa kuzingatia
usafi wa mwili na mazingira, mlo kamili, kufanya mazoezi, kupunguza
uzito na kuepuka matumizi ya tumbaku, pombe pamoja na dawa za kulevya. Uwezo wa kuzaa na kuepuka saratani mbalimbali pia
unaweka kuwa nzuri kama magonjwa yasambazwayo kwa njia ya kujamiiana
kusiko salama na utoaji wa mimba kiholela, vitaepukwa.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment