Social Icons

Pages

Friday, January 09, 2015

VICHOZI MENO VIZURI ILA NA HATARI KWA FIZI, MENO


Matumizi ya vijiti vya kuchokoa meno maarufu kama ‘toothpick’ ni namna nyepesi zaidi ya kuondoa mabaki ya nyama, mboga za majani au matunda yaliyonasa katika meno badala ya kufanya hivyo kwa kidole ama kitu kingine.
Wapo wengine ambao hata kama wamekwishaondoa mabaki ya vyakula kwenye meno huona raha kutembea huku wakikitafuna kijiti hicho.
Unaifahamu hatari ya kutumia vijiti hivi ambavyo pengine ni biashara kubwa ya watu wengi hapa nchini?
Hatari ya vijiti hivi inayotajwa na Daktari bingwa wa meno kutoka Kliniki ya Meno ya SD, Israel Kombole ni kupanua fizi kunakochangia jino kushambuliwa kirahisi na magonjwa na hata kung’oka kwa meno.
Tabia ya kuchokoa meno inaelezwa na Dk Kombole kuwa inasababisha kutanuka kwa fizi ambako huweza kuwa hifadhi ya mabaki ya chakula ambayo yakioza huwa ndicho chanzo cha kuharibika kwa meno. “Meno yanaathirika kwa urahisi zaidi halafu vijiti hivi husababisha hata mtu akaharibu umbile la meno kwa sababu atakapozoea basi nafasi ya jino na jino huongezeka,” anasema
Mbadala wa vijiti hivi unatajwa na Dk Kombole kuwa ni uzi mwembamba maalumu kwa kuondolea uchafu kwenye meno. Sambamba na kutengeneza mashimo kwenye fizi, pia vijiti hivi vinaelezwa kuwa husababisha mdomo kuwa na vidonda mara kwa mara.
“Mtu anayetumia toothpick mara kwa mara hupata vidonda mdomoni kutokana na kukwaruzwa na mara nyingi, mtumiaji anaweza asihisi kama amepata jeraha. Baadaye anaweza kubaini kuwa amepata vidonda na kumbe vidonda vimesababishwa na toothpick,” anasema.
Vidonda hivi, Dk Kombole anasema huweza kuwa vikubwa hasa pale bakteria wanapoingia kupitia uchafu ule ule ulio katika meno. Anaeleza madhara mengine ni kupata tatizo la kuvuja damu mara kwa mara kutokana na tabia ya kuchokoa kila baada ya kula. “Kama ‘toothpick’ itakandamizwa kwa nguvu mdomoni, inaweza kuleta kidonda ama mchubuko hivyo mara nyingine kufanya kidonda, pia kama wapenzi watapigana busu muda huo huo baada ya kujichokoa, uwezekano wa maambukizi ya magonjwa ni mkubwa,” anasema Dk Kombole. Anafafanua: “Siyo maambukizi ya magonjwa tu, bali pia watumiaji wa vijiti hivi wanaweza kuvimeza kwa bahati mbaya na inapotokea hivyo, huweza kusababisha kushindwa kufanya kazi kwa ogani au kuharibiwa kwa utumbo.” Hoteli ya Macdonald Portal Golf and Spa ya Uingereza iliondoa huduma ya toothsticks katika meza za wateja ili kuondoa madhara yanayoweza kuwapata baada ya kutumia vijiti hivyo.
Jarida la Offspring Health la nchini China linaweka kielelezo cha mwanamke mmoja ambaye aliugua tumbo kwa muda mrefu kiasi cha kumshtua daktari wake. Mwanamke huyo baadaye alianza kupata homa, kutapika, mapigo ya moyo kwenda kwa kasi, kushindwa kupumua na ilionekana kuwa amekula chakula chenye sumu. Madaktari walipompima kwa kutumia ‘ultra sound’ walibaini uwepo wa vitu kama miba miba vimejikusanya katika tishu zake za mwili. Hata hivyo, wakati huo kipimo hicho kilibaini kuwa ini lake limeathirika. Wataalamu wa afya walipomfanyia upasuaji mkubwa ili kuondoa taka zilizofanana na miba katika tishu walishangazwa kuona vipande vya ‘toothpick’. Kadhalika, Jarida la Register Guard linaeleza kuwa kutafuna vijiti vya kuchokoa meno, husababisha kubaki kwa vipande vidogo vidogo ambavyo huweza kumezwa kwa bahati mbaya na iwapo vitaingia katika ogani yoyote mwilini huweza kusababisha kifo au pengine maumivu makali. Vijiti vya kuchokoa meno pia vinaweza kuwa chanzo cha magonjwa kwani wengi tunavikuta katika mazingira tusiyoyafahamu hasa katika migahawa. Ni rahisi kupata maambukizi ya magonjwa kwa njia hiyo. Kuhusu vijiti hivyo kugusa uchafu, Dk Mainess Nzingu wa kliniki ya meno katika Hospitali ya Amana anasema kwa vina ncha kali, huweza kusababisha jeraha kwenye fizi au mdomoni na iwapo kilikuwa katika mazingira machafu basi bakteria wataingia moja kwa moja.

Historia ya vijiti vya meno
Usafishaji wa meno unaanzia mbali na unahusisha mataifa mengi wakiwamo Waafrika. Matumizi ya miti kama kifaa cha kusafisha meno yalianza kutumiwa na babu zetu. Ilikuwa ni rahisi na salama kwa sababu mti ule kwanza ulilainishwa kwa mate na kutafunwa tafunwa kabla ya kutumika.
Hata hivyo, baadaye 1869, raia wa Uingereza, Charles Foster alivumbua mfanano wa mswaki, yaani kifaa cha kusafisha meno kilicho katika muundo wa kisasa zaidi ambacho ni toothpick. Mpaka sasa karibu kila mgahawa na hata kwa mamalishe, hukosi kuona kibakuli kilichosheheni vijiti vya kuchokoa meno.
Hata hivyo, watumiaji wengi licha ya kukubali kuwa matumizi ya vijiti hivyo yanawaweka katika hatari, lakini waliona hakuna mbadala wa vijiti hivyo kwani ni gharama kutembea na uzi wa kisasa wa kusafisha meno.
Kwa upande wake, Cecilia Kasembe anasema vijiti vya kuchokoa meno ni rahisi kutumia kuliko uzi huo na kuwa vinapatikana bure katika migahawa. “Ni kitu rahisi kusafisha meno kwa sababu unapoacha uchafu kwenye fizi unakusumbua,” anasema. Kadhalika, Rashda Muganda mkazi wa Mbezi Samaki anasema ‘toothstick’ imekuwa mazoea kwa wengi kwa sababu imeboreshwa kwa kuchongwa vizuri na kuwekwa katika chombo maalumu. Hata hivyo, Wataalamu wa afya wanaeleza wazi kuwa vijiti hivi hutumiwa vibaya na wengi hasa ile tabia ya kutembea na kijiti kila mahala huku akikitafuna.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: