Mwenyekiti mstaafu wa Tume ya
Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Amiri Manento amesema jambo kubwa
alilolipitia wakati wa uongozi wake lilikuwa ni kifo cha mwandishi wa
habari, Daudi Mwangosi baada ya kupigwa bomu na polisi, mkoani Iringa
mwaka 2012.
Alisema jambo hilo lilikuwa kubwa kwa wananchi
kuliko lilivyopokelewa na Serikali. Alisisitiza kuwa tume yake ilitoa
taarifa ya kifo hicho ikiwa na mapendekezo na kuikabidhi Serikali. Jambo
la kushangaza, alisema mapendekezo yao hayajatekelezwa mpaka leo. “Hili jambo kwangu lilikuwa kubwa. Tume
tulifuatilia tukio lile na kubaini kuwa Mwangosi alipigwa bomu na
polisi. Tulitoa mapendekezo yetu, lakini mpaka leo hakuna utekelezaji
wake,” alisema Manento ambaye pia ni Jaji Kiongozi mstaafu.
Aliongeza kuwa sasa ni kazi ya Nyanduga kufuatilia
utekelezaji wa maazimio yale ili kuhakikisha haki inatendeka na kujenga
imani ya tume kwa wananchi. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliundwa
kwa mujibu wa Kifungu cha 129 (1)(c) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ya mwaka 1977 na sheria ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
namba saba ya mwaka 2001.
Jukumu kubwa la tume hii ni kulinda, kutetea na
kuhifadhi haki za binadamu nchini. Katika kutekeleza jukumu hilo, tume
imepewa mamlaka ya kupokea malalamiko kutoka sehemu mbalimbali na
kuanzisha uchunguzi wake yenyewe kama itaona kuna ukiukwaji wa haki.
Tume ya Haki za Binadamu ilitoa mapendekezo matano
wakati wa taarifa yake juu ya kifo cha Mwangosi. Baadhi ya mapendekezo
hayo yalikuwa ni: elimu ya vyama vya siasa na sheria ya polisi kuhusu
vyama vya siasa kutolewa kwa askari polisi, ambao wanaonekana
kutozifahamu kabisa. Maoni mengine yalikuwa ni: Jeshi la polisi na
msajili wa vyama vya siasa kuepuka kufanya maamuzi ambayo yatasababisha
hisia za ubaguzi au upendeleo miongoni mwa jamii wakati wanatekeleza
majukumu yao.
Kamati za ulinzi na usalama za mikoa na wilaya,
zilitakiwa kuwa makini na vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu na
ukiukwaji wa misingi ya utawala bora vinavyofanywa na mamlaka mbalimbali
kwenye maeneo yao. Pia, tume ilipendekeza kuheshimiwa na kulindwa kwa misingi ya demokrasia ya vyama vingi nchini.
Awali, Rais Kikwete alimwapisha Msajili wa
Mahakama ya Rufani, Katarina Revocati ambaye aliahidi kuendeleza nguvu
iliyoanzishwa ya kuleta mabadiliko katika mhimili wa Mahakama na
kuufanya utende kazi zake kwa ufanisi. “Baada ya mabadiliko ya sheria, ofisi ya msajili
imebaki na kazi ya kushughulikia mashauri tu. Kuanzia mwaka jana majaji
walianza kuzunguka mikoani kusikiliza kesi za muda mrefu. Nina tumaini
nitasaidia kuongeza nguvu katika mpango huo,” alisema.
Alitaja changamoto kubwa iliyo mbele yake kuwa ni mlundikano wa kesi nchi nzima bila kusikilizwa. Alisema hatua zimeshachukuliwa kukabiliana na tatizo hilo na kuwa majaji walianza na mikoa ya Tabora na Dar es Salaam. Naye mwenyekiti mpya wa tume hiyo, Bahame Nyanduga
alisema tume itashirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na
asasi za kiraia katika kusimamia haki za binadamu hasa mwaka huu wa
uchaguzi mkuu.
Nyanduga aliyasema hayo jana baada ya kuapishwa na
Rais Jakaya Kikwete, Ikulu jijini Dar es Salaam kushika wadhifa huo.
Sambamba naye, pia aliapishwa Makamu Mwenyekiti, Iddi Mapuri na
makamishna wanne ambao ni Mohamed Hamad, Kelvin Mandopi, Rehema Ntimizi
na Salma Hassan. “Katika uongozi wangu, nitashirikiana na wadau
mbalimbali wa haki za binadamu na utawala bora ili kujenga jamii ya
Watanzania katika msingi wa haki na usawa.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment