Dar es Salaam. Kamati Kuu ya CCM, itakuwa na
vikao vizito kuanzia Jumatatu kujadili masuala mbalimbali yanayokikabili
chama hicho.
Mambo makubwa yanayotarajiwa kuchukua nafasi
katika vikao hivyo vitakavyoanza saa 72 zijazo ni kuwajadili wanachama
wake ambao baadhi ni mawaziri waliokumbwa na kashfa ya Akaunti ya Tegeta
Escrow na tathmini ya wanachama wake sita walio katika adhabu ya mwaka
mmoja baada ya kutiwa hatiani kwa kudaiwa kufanya kampeni za urais kabla
ya muda.
Pia kamati hiyo, inatarajia kutumia vikao hivyo
kuangalia namna ya kupata wagombea watakaokubalika na wananchi kuelekea
kwenye kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa rais, wabunge na madiwani. Akiwa katika ziara ya kuwashukuru wananchi kwa
kuipa CCM ushindi kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa mkoani Tanga hivi
karibuni, Katibu Mkuu wa CCM, Abdurahman Kinana alisema chama hicho
kitaanza rasmi vikao vyake vya ngazi ya Taifa kupitia masuala mbalimbali
yanayokihusu.
Alipoulizwa kuhusu agenda hizo katika vikao hivyo
jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikuja juu na
kusema hakuna kitu kama hicho. “Hata mkiiandika vibaya CCM, itashinda
tu,” na kisha kukata simu. Hata hivyo, habari zilizopatikana jana jioni
kutoka ndani ya CCM, zinasema kuwa sekretarieti ya chama hicho,
inakutana leo mjini Dodoma kuandaa ajenda za kikao hicho kitakachoanza
Jumatatu ijayo.
Mawaziri waliokumbwa na kashfa ya Escrow ni Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ambaye
ni pia Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM. Profesa Tibaijuka tayari ameondolewa kwenye nafasi
yake ya uwaziri baada ya kukiri kupewa Sh1.6 bilioni na Mkurugenzi wa
VIP Engineering, James Rugemalila. Wengine waliotajwa kupewa mgawo na Rugemalila ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge na Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba, William Ngeleja. Pia Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo yupo katika uchunguzi kuhusiana na kashfa hiyo.
Mbali na wahusika wa Akaunti ya Escrow, kikao
hicho cha Kamati Kuu ya CCM kitachunguza maadili ya viongozi wakiwamo
waliokumbwa na zuio la kujihusisha na kampeni kwa miezi 12, huku
mienendo yao ya kisiasa ikifuatiliwa. Watakaojadiliwa ni Naibu Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi, Teknolojia, January Makamba, Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na
Uratibu), Steven Wasira na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini
ambaye ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja. Kinana akiwa Tanga alikaririwa akisema: “Wiki ijayo tunaanza
kukaa vikao vya kupimana sisi viongozi juu ya uadilifu wetu ndani ya
Serikali, tunataka kuwa na viongozi wenye kujua Watanzania wanataka nini
na uadilifu wao usiwe hata na chembe ya shaka.”
Msingi wa hukumu
Alisema salamu za CCM kwa Watanzania kwa mwaka
2015 ni ahadi ya kuweka mkazo katika maadili kwa viongozi wake na kwamba
itafanya tathmini kwa lengo la kujipanga kwa uchaguzi mkuu ujao. “Watanzania wanataka viongozi wasiokuwa na urasimu
umangimeza, wenye mlolongo wa itifaki na wanaoweza kushuka chini,”
alisema Kinana.
Msingi wa hukumu
Kikao cha tathmini cha wiki ijayo ni mfululizo wa
baada ya kikao cha mwisho cha Agosti mwaka jana kilichokutana chini ya
Mwenyekiti wake, Philip Mangula kupitia taarifa za utekelezaji wa adhabu
kwa makada sita wa chama hicho wanaodaiwa kuanza kampeni kuwania urais
kabla ya wakati.
Kufanyika kwa kikao hicho kulitokana na agizo la
Mangula ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM, alilolitoa Februari 8,
mwaka jana akizitaka ofisi zote za ngazi ya mikoa na wilaya kufungua
mafaili kupitia mienendo ya wagombea walioanza kampeni za uchaguzi wa
kuteuliwa kugombea urais kabla ya wakati. Makada hao waliozuiwa
kujihusisha na kampeni kwa miezi 12 na adhabu zao zinamalizika Februari
18.
Hatua ya kufanyia tathmini hiyo ni kutokana na
kuelezwa kuwa pamoja na adhabu hiyo, baadhi yao walikuwa wakikiuka na
kuendelea na mikakati ya kampeni kwa kukusanya watu wa kupanga nini cha
kufanya tayari kwa uchaguzi wa mwaka huu.
Katika kikao hicho cha Kamati Ndogo ya Maadili na
Nidhamu, ilielezwa kuwa katika kipindi cha miezi kadhaa, timu za maofisa
usalama wa chama zilisambazwa mikoa yote na kukusanya taarifa za makada
hao.
Kikao kama hicho cha Kamati Kuu kilikutana Julai
16, mwaka jana na kupokea taarifa za harakati za baadhi ya wanachama wa
CCM walioonyesha nia ya kuomba ridhaa ya chama kuwania urais. Kutokana na hali hiyo, Kamati Kuu iliitaka Kamati
ya Maadili kufanya marejeo na kuangalia utekelezaji wa adhabu kwa makada
hao sita.
Siku moja baadaye, Julai 17, mwaka jana, Nape
alisema endapo Kamati ya Usalama na Maadili itabaini kama makada hao
walikiuka mwenendo wa utekelezaji wa adhabu waliyopewa, watapoteza
sifa. “Baada ya kutafakari kwa kina, Kamati Kuu inapenda kuwakumbusha
kuwa ili wasipoteze nia ya kugombea ni muhimu wakazingatia katiba,
kanuni na taratibu za chama zinazosimamia masuala hayo.”
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment