Waziri Mkuu Mizengo Pinda akifurahi na wananchi wa Halmashauri ya
Nsimbo, Wilaya ya Mlele baada ya kuwasili kwenye viwanja vya halmashauri
hiyo kuhutubia mkutano wa hadhara akiwa kwenye ziara katika jimbo lake
la uchaguzi.
Katavi. Waziri Mkuu Mizengo Pinda amezitaka
ngazi mbalimbali za uteuzi wa wagombea wa CCM kuwapa wananchi nafasi
kuchagua watu wanaowataka ili kuepuka kupoteza viti katika uchaguzi. Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo juzi jioni wakati
akiwahutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika
kwenye Uwanja wa Mikutano wa Kashaulili, Mpanda mkoani hapa.
Pia alitumia mkutano huo kuaga jimboni humo
akisema muda wa kuendelea kuwa Mbunge wa Katavi umetosha na sasa
anatafuta kitu kingine cha kufanya. Kwa mara ya kwanza, Pinda alichaguliwa kuwa Mbunge
wa Mpanda Mashariki (sasa Katavi) mwaka 2000 na ameongoza jimbo hilo
kwa mihula mitatu.
Kuhusu uteuzi
Akizungumzia uteuzi wa wagombea mbalimbali, Pinda
aliwaasa viongozi wa CCM kuwateua watu wanaofaa kugombea uongozi kwenye
nafasi mbalimbali wale ambao wanakubalika na wananchi na wawape nafasi
wananchi kuchagua mtu wanayemtaka.
Alisema haifai CCM kuwalazimisha kwa kuwachagulia
wananchi kiongozi wasiyemtaka... “Kumekuwa na tabia ya kuteua watu ambao
hawakubaliki kwa wananchi na matokeo yake watu hao wamekuwa wakishindwa
kwenye uchaguzi... acheni chuki, msiteue watu kuwania uongozi kwa ajili
ya kupewa pesa na urafiki,” alisema. Pinda aliyetangaza ni ya kuwania urais kimyakimya,
aliwataka Watanzania kutowachagua watu wanaotaka kiti hicho na vile vya
ubunge na udiwani kwa kutanguliza fedha.
“Watu hao wanaotafuta uongozi kwa kutoa rushwa kwa
wananchi ni hatari, kuweni makini kwa kuchagua viongozi waadilifu
watakaoongoza kwa kutanguliza mbele utaifa kuliko masilahi yao binafsi.
“Wako watu wanaotaka uongozi kwa kuhonga
wapigakura, watu wa namna hiyo hawafai kuwa wagombea wa urais, ubunge na
udiwani kwa kuwa si waadilifu na wakishapata uongozi kamwe hawezi
kuwajali wananchi kwanza watataka kurudisha fedha walizotoa. “Hakikisheni mnachagua viongozi ambao wanaweza
kuwaongoza kwenye maeneo yenu na siyo vinginevyo, achaneni na watu
wanaowapa pesa hao hawatawapeleka kokote badala yake watakuwa viongozi
wabinafsi kwa kutanguliza masilahi yao mbele na kuwasahau wananchi
waliowaweka madarakani,” alisema Pinda. Alisema: “Watu wanaotaka uongozi kwa fedha,
wanapowaletea hizo pesa kuleni lakini mhakikishe wakati wa uchaguzi
hamwapigii kura.”
Huku akishangiliwa na wananchi hao kwa makofi na vigelegele,
alisisitiza: “Ukitaka kumchagua mtu mwenye sifa za kuwa rais wa nchi
hii, chagueni mtu ambaye hatoi rushwa kwa wananchi, mwadilifu,
mnyenyekevu na mchapakazi. Hata watu wanaotaka ubunge na udiwani
hakikisheni hamwachagui wanaotaka uongozi kwa rushwa, chagueni viongozi
watakaowaongoza vizuri kwenye maeneo yenu.”
Viongozi wa dini
Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa dini kuachana na
masuala ya kuhubiri siasa wanapokuwa kwenye nyumba za ibada na badala
yake wafanye kazi wanayotakiwa kufanya ya kuhubiria neno la Mungu. “Kumeanza kusikika maneno kuwa viongozi wa dini
wanaendeleza chuki kwa kuhubiri siasa kwenye nyumba za ibada badala ya
kutenda kazi zao za kuwapa neno la Mungu waumini wao.
“Viongozi hawa wajibu wao ni kufanya kazi ya
kuwaongoza waumini kwa kuwahubiria neno la Mungu kuliko kutumia nyumba
za ibada kuhubiri siasa, kufanya hivyo ni kukiuka maadili ya kazi zao. “Kama wanataka kufanya siasa waje hapa majukwaani
tupambane sawasawa... kama mtu anaweza aje apambane hapa,” alisema
Waziri Mkuu. Alisema viongozi wa dini washirikiane na Serikali na chama hasa tawala (CCM), katika kuhubiri upendo na amani lakini si siasa.
“Ninaogopa kuona kiongozi wa dini anakwenda
kanisani kisha anasema chagueni Chama cha Mapinduzi, ni hatari. Nafasi
walizonazo ni za kidini na zinatakiwa kuheshimiwa,” alisema na kuongeza
kuwa kuacha hayo yakiendelea ni hatari kwa Taifa kwani na kunaweza
kuleta mgogoro katika jamii. Waziri Mkuu leo anakamilisha ziara yake mkoani
Katavi kwa kufanya mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi
Ifukutwa, Mpanda.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment