Social Icons

Pages

Friday, January 09, 2015

SASA KAZI NI MOJA TU, KUDAI TUME HURU


Padre Baptiste Mapunda (M.Afr)
Tunapouanza mwaka 2015 tujue kwamba huu ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu kwa wabunge, madiwani pamoja na rais.
Kisiasa ni mwaka wa kihistoria kwa sababu Katiba Inayopendekezwa inapaswa kupigiwa kura ya “Ndiyo” au “Hapana” mwezi Aprili 2015 kama Serikali haitabadili mwelekeo wake. Mimi ni kama nilivoandika kwamba kura yangu kwa Katiba hiyo ninayoiita ya CCM ni “hapana, hapana, hapana”.
Nitapiga kura ya “Hapana” na kuwashawishi Watanzania wanaopenda mabadiliko na maendeleo kuungana nami kwa sababu katiba hii iliyopendekezwa kwa mabavu ya bunduki na mabomu ya dola, haina masilahi kwa wananchi wa kawaida. Katiba hii inayopendekezwa, ina kazi moja tu; kulinda ufisadi na mali za kikundi cha watu wa chache ndani ya Serikali ya CCM.
Wewe mwananchi wa kawaida ambaye huna manufaa nayo, utaipigia kura ya kuipitisha ili iweje?
Maoni ya Tume ya Marekebisho ya Katiba iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba yalipendekeza kuwapo kwa “TUME HURU YA UCHAGUZI” ambayo inakidhi mahitaji ya siasa za vyama vingi na sio chama tawala tu cha CCM.
Swali langu ni je, Serikali ya CCM itakubali kuunda Tume Huru ya Uchaguzi, wakati ikijua kwamba ushindi wake katika chaguzi unategemea sana tume hii ya sasa ya CCM chini ya mamlaka ya Rais ambaye ni mwenyekiti wa CCM?
Nathubutu kuandika kwamba, sasa Watanzania wenzangu kazi ni moja tu, yaani kudai kuundwa kwa TUME HURU YA UCHAGUZI” kama ilivyokusudiwa na wananchi kwenye Rasimu ya Katiba. Chombo hiki ni cha kitaifa si cha chama kimoja. Kwa hivyo wananchi wote bila kujali chama, dini, kabila, cheo, ukanda unakotoka wala rangi, tuungane kudai ili iundwe haraka na kushughulikia masuala yote ya uchaguzi kwa haki, uhuru, uwazi na usawa kwa vyama vyote na kuondokana na malalamiko ya miaka mingi.
Tume hii huru itaratibu sheria na kanuni za uchaguzi, kusimamia uchaguzi wenyewe, kushughulikia kesi na kero pamoja na kuwatangaza washindi wa kweli mwisho wa uchaguzi.
Tume hiyo itashughulika na uboreshwaji wa daftari la wapiga kura nchini Tanzania.Masuala haya mawili yaani Tume Huru ya Uchaguzi na uandikishwaji majina ya wananchi kwenye darftari la Wapigakura ni mambo muhumu sana katika ukuaji, ukomavu wa demokrasia na utawala bora nchini. Wapinzani mkirogwa kuingia kichwa kichwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu bila ya TUME HURU YA UCHAGUZI, basi mjue itakuwa “imekula kwenu”.
Ushindi wa CCM unategemea tume ya sasa ambayo mimi binafsi naiona kuwa ni poliCCM ambayo imejaa rushwa, fitina, wizi wa kura, uchakachuaji, upendeleo na vurugu. Mimi kama mchezaji mpira wa miguu katika jamii hasa nikiwa katika shule na vyuo mbalimbali, mara nyingi tulikuwa tunakataa timu yetu kushiriki katika mchezo ambao kanuni zilikuwa za upendeleo. Ni mtu mjinga pekee, tena mwenye ‘umaskini wa akili’ ndiyo atakubali kushiriki katika shughuli ya pamoja ambayo inaendeshwa bila sheria na kanuni na pengine hata upendeleo mkubwa.
Wapinzani chondechonde nawasihi anzeni kudai uundaji wa katiba mpya mwanzoni mwa mwaka huu, kuishinikiza Serikali kwani hilo ni la msingi kuliko hata kufanya kampeni za uchaguzi.
Usalama wa kura zenu na ushindi upo mikononi mwa “TUME HURU YA UCHAGUZI” na siyo tume ya sasa ambayo ipo chini ya mamlaka ya Rais ambaye ni mwenyekiti wa CCM la hasha. Madai ya TUME HURU YA UCHAGUZI siyo ya wapinzani tu bali ya Watanzania wote wenye kupenda haki, uhuru katika chaguzi zetu pamoja na maendeleo ya demokrasia na utawala bora. Viongozi wa madhehebu ya dini yote na waumini wao ni wadau wa demokrasia inayostawisha amani na uhuru wa kuabudu, hivyo ni vyema washiriki kikamilifu katika madai hayo ya msingi wa demokrasia.
Wanaharakati, vyama vya wafanyakazi, wakulima na wafugaji nao pia ni waathirika wa tume hii ya sasa. Wanafunzi wa vyuo vikuu pamoja na vijana wote ambao wanapaswa kujiandikisha na kupigia kura, basi nao washiriki harakati za kudai TUME HURU YA UCHAGUZI badala ya kungoja kuhongwa ili kuwavusha wanasiasa wanaotumia “umaskini wa akili’ kuwahadaa kwa ahadi hewa mfano uundwaji wa baraza la vijana.
Jinsi uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa uliofanyika Desemba mwaka jana na kuvurugwa kwa makusudi; ulivyojaa mizengwe, fitina, chuki, vitisho, majeruhi, utekaji, mauaji, wizi wa kura na maovu mengine ni alama tosha kwamba “ sasa TUME HURU YA UCHAGUZI” haiepukiki ni muda mwafaka iundwe hata kama ni kesho.
Kama CCM wana ujasiri wa kubadilisha matokeo, kuongeza kura na vituko vingine vikafanyika mbele ya hadhara, itakuwaje kama kura zitahesabiwa na kujumlishwa na Tume ya sasa chini ya mamlaka ya Rais?
Maana yake ni kwamba wananchi wataendelea kupigia kura lakini mabadiliko hawatayaona na hii ndiyo sababu ya kule Kenya mwaka 2007 hawakuwa na njia nyingine isipokuwa akina Raila Odinga kukataa kata kata kuyatambua matokeo na ushindi wa Kibaki na hatimaye vurugu zukatokea na kuzaa maafa ya zaidi ya watu elfu moja. Usipotenda haki, usitegemee kupata amani, labda amani ya bunduki kama hii inayohubiriwa na Serikali ya CCM hapa nchini. La mgambo limepigwa enyi Watanzania amkeni tuungane pamoja bila kujali tofauti zetu. Tudai uundwaji wa TUME HURU YA UCHAGUZI kwa maendeleo ya demokrasia na utawala bora nchini. Ndiyo kwa maana nathubutu kuandika kwa uwazi na uhuru kwamba “ sasa kazi ni moja tu; kudai TUME HURU YA UCHAGUZI”.
hakuna kulala mpaka kieleweke.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: