Social Icons

Pages

Wednesday, January 07, 2015

FEDHA ZA FIFA KUJENGA MADUKA TFF



Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema mgawo wa fedha za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) utatumika kuendeleza soka pamoja na kujenga maduka na hoteli ndogo kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Fifa imetangaza kutoa Dola 1.3 milioni (Sh2.2 bilioni) kwa kila mwanachama wake, ikiwamo TFF pamoja na Dola 300,000 (Sh510 milioni) za kuiandaa timu ya taifa kwa ajili ya Kombe la Dunia mwaka 2018.
Akizungumza na gazeti hili jana, Malinzi alisema TFF imepanga kuzitumia fedha hizo kama walivyopewa maelekezo na Fifa kwa lengo la kuendeleza mchezo wa soka nchini.
Bosi huyo wa TFF aliongeza kuwa wameandaa mpango mkakati maalumu wa kulifanya shirikisho hilo kujitanua kibiashara. “TFF itatumia Dola 750,000 tulizopewa kama gawio la Kombe la Dunia kujenga vitegauchumi mbalimbali vitakavyosimamiwa na shirikisho,” alisema.
“Tumepanga kutumia hizo Dola 700,000 kujenga maduka makubwa kuzunguka eneo la makao makuu ya TFF hapa Karume, pia tutajenga hoteli ndogo katika eneo hili, tumeanza kufanya mawasiliano na mamlaka zinazohusika na utoaji wa vibali vya ujenzi, ikiwemo Manispaa ya Ilala na tayari tumeshawapelekea mchoro wa mradi,” alieleza Malinzi.
Alisema Fifa wameongeza kiasi kinachotolewa kupitia mradi wa Goal Project kutoka Dola 500,000 hadi 600,000 kwa mwaka. Kiasi hicho cha fedha alisema kitatumika kuendeleza soka la wanawake, lile la ufukweni, uendelezaji soka la vijana, kutengeneza miundombinu ya soka na kiasi kingine cha fedha kitatumika katika shughuli mbalimbali za kiutawala kwa shirikisho.”
“Dola 300,000 tulizopewa kwa ajili ya kuiandaa Taifa Stars katika mechi zake za kufuzu kwa Kombe la Dunia 2018 zitasaidia mchakato huo ambao ni mkubwa na mrefu,” alisema Malinzi na kuongeza kuwa fedha hizo zitatumika kuandaa kambi, mechi za kirafiki, posho kwa wachezaji, pia kuendeshea gharama zote zinazohusu Taifa Stars.”
Mapema wiki hii, Katibu Mkuu wa Fifa, Jerome Valcke alisema shirikisho hilo limepanga kuwapa wanachama wake Dola 1,050,000 (Sh1.78 bilioni ) na Dola 250,000 (Sh425 milioni) kwa ajili ya mpango wa kifedha kwa ajili ya maendeleo ya kila mwanachama, Sh850 milioni itakuwa kama bonasi na nyingine, Sh510 milioni kwa ajili ya maandalizi na michezo ya kufuzu kucheza Kombe la Dunia mwaka 2018.
Wakati huo huo; TFF imetangaza kuwa waamuzi 18 nchini wamepata beji ya Fifa baada ya kufanya vizuri kwenye kozi iliyoendeshwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF). Hafla ya kuwakabidhi beji waamuzi hao ilifanyika jana asubuhi kwenye makao makuu ya TFF Karume, Dar es Salaam mgeni rasmi akiwa Malinzi.
Katika hafla hiyo, jumla ya waamuzi 18 walipata beji hizo wakiwamo wanawake saba na wanaume wanane. Miongoni mwao wanawake wa tatu ni waamuzi wa kati na wanne ambao ni wasaidizi. Malinzi aliwataka waamuzi hao kuzingatia sheria zinazoongoza mchezo wa soka huku akiwataka kuepuka kwa nguvu zote masuala ya rushwa na upangaji matokeo.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: