Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya NCCR-Mageuzi,
Hemed Msabaha, ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) Mkoa wa Kilimanjaro, kuingilia kati madai ya wakazi wa
Kijiji cha Kilototoni Wilaya ya Moshi ya kuhujumiwa ahadi yao ya
kupatiwa umeme iliyotolewa na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal.
Rai hiyo ya Msabaha inafuatia malalamiko ya wakazi hao ambao pamoja na
kuiomba Takukuru kufanya hivyo, pia wameelekeza kilio chao kwa Mkuu wa
mkoa huo, Leonidas Gama, wakimtaka kuunda kamati maalum ya kuchunguza
madai ya kupotoshwa Makamu wa Rais kuhusu utekelezaji wa mradi wa wakala
wa nishati vijijini (Rea) katika mji mdogo wa Himo.“Kwa kuwa wananchi hawa, wanaona wamehujumiwa kutokana na ahadi ya Dk. Bilal, ni vizuri Takukuru wasijiweke kando, waingilie kati kutafuta kiini cha mgogoro huu. Siamini jambo hili litachukuliwa kisiasa, isipokuwa ni jambo ambalo kutimiza tu madai ya haki,”alisema Msabaha.
Wakazi hao wanadai Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), walimdanganya Makamu wa Rais kuwa miongoni mwa vijiji vitakavyonufaika na mradi huo ni pamoja na Kilototoni lakini kwa sababu zisizoeleweka, imechepusha mradi huo na kuutekeleza katika kijiji jirani cha Ghona kilichopo Kata ya Kahe Mashariki.
Kwa mujibu wa wakazi hao, Dk. Bilal alitoa ahadi hiyo kwa wananchi wa Kilototoni Oktoba 7, mwaka 2013 akiwa katika kata ya Makuyuni wakati akizindua miradi ya ukarabati wa vituo vya kupooza umeme na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme katika mkoa wa Kilimanjaro.
Wakizungumzia madai hayo, Alli Mfinanga alisema Dk. Bilal aliyekuwa ameongoza na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter, alitangaza kijiji hicho kimepata mradi wa umeme wa Rea na kwamba baada ya Makamu wa Rais kuondoka, waliambiwa wajiandae kuingiziwa umeme kwenye nyumba ao lakini cha kushangaza ulipelekwa Ghona.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho, Robert Mosha, alisema mradi huo umetekelezwa nje ya matarajio yao licha ya ramani kuonyesha kijiji chao ndicho kilichopitiwa na umeme.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment