Mwenyekiti wa Ukawa Profesa Ibrahim Lipumba(katikati) akiwa na
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia(kushoto) na Katibu Mkuu wa
Chadema, Wilbrod Slaa(kulia).
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umelitaka Bunge kuiwajibisha serikali ikiwa Rais Jakaya Kikwete atashindwa kutekeleza maazimio ya Bunge ikiwemo kumng’oa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo. Akizungumza jana, Mwenyekiti wa Ukawa Profesa Ibrahim Lipumba akiwa na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na Katibu Mkuu wa Chadema, Wilbrod Slaa, alisema Kikwete anasita kumuondoa Muhongo wakati Bunge lililishatoa maazimio ya kutaka aondolewe.
Profesa Lipumba alisema Bunge linalowakilisha
wananchi zaidi ya milioni 45 liliazimia uteuzi wa Muhongo utenguliwe
lakini rais anasema bado anachunguza. Profesa Lipumba alisema kama Rais Kikwete
atashindwa kumwajibisha Muhongo atakuwa ameshindwa kutekeleza moja ya
maazimio ya Bunge na kwamba Ukawa litaliomba Bunge kuiwajibisha
serikali. Alisema moja ya njia ya kuiwajibisha serikali ni pamoja na wabunge kupiga kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu.
Profesa Lipumba alisema “ hivi rais anachunguza
nini haliamini bunge, kama anavyoteua mawaziri pia ana madaraka ya
kutengua nafasi zao, sasa anasita nini wakati ni azimio la bunge
limemwelekeza, ikumbukwe kuwa bunge kwa niaba ya wananchi ndilo lenye
jukumu la kuisimamia serikali,” alisema Lipumba.
Alisema hotuba aliyoitoa Jumatatu wakati
akiwahutubia wazee wa mkoa wa Dar es Salaam, haijakidhi matarajio ya
wengi kwani kuna maazimio hayajatekelezwa. Azimio ambalo halijatekelezwa na rais Kikwete ni lile linalotaka kutaifishwa kwa mitambo ya IPTL na kutengua uteuzi wa Muhongo.
Mwenyekiti huyo alisema rais amekataa kutekeleza
azimio la kutaka mitambo ya IPTL itaifishwe na kutoa sababu ambazo
hazina maana. “Tangu mitambo ya IPTL imefungwa taifa limepata
hasara kubwa kwa sababu umeme unaouzwa na ni wa gharama kubwa kuliko
mitambo yoyote ya umeme inayotumika katika bara la Afrika taifa
limeingia hasara kubwa, rais aitaifishe,” alisema Profesa Lipumba. Alisema katika hotuba hiyo rais alionyesha
kuipendelea IPTL na kuikandamiza Tanesco wakati akielezea kuwa fedha za
Escrow zilikuwa mali ya IPTL.
Hatua za kuchukua
Lipumba alisema kama rais atashindwa kutekeleza baadhi ya
maazimio, Ukawa wataitisha maandamano nchi nzima ili kulaani ufisadi wa
Tegeta Escrow na kushinikiza utekelezaji wa maazimio ambayo yatakuwa
hayajatekelezwa. Alisema hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya
wote waliohusika na ufisadi wa akaunti ya Tegeta Escrow na wengine
walionufaika nazo. Sheria ya maadili itungwe upya ili iweke uwazi wa mtu yoyote kuona taarifa ya mali za viongozi. Vyama vya siasa vya Ukawa kwa kushirikiana na wabunge vitaendelea kuelimisha umma kuhusu ufisadi wa Akaunti ya Tegeta Escrow.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment