Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon
Makubaliano ya kudhibiti biashara ya silaha duniani yanaanza kutekelezwa
leo, huku wanaharakati wakiapa kuwa watahakikisha
makubaliano hayo yanatekelezwa ipasavyo.
Makubaliano hayo ya kihistoria ya kudhibiti biashara ya silaha, ATT,
yameweka sheria katika sekta ya viwanda vya kutengeneza silaha yenye
thamani ya Euro bilioni 70 na yanataka kuziondoa silaha mikononi mwa
wahalifu na watu wanaokiuka haki za binaadamu.
Wanaharakati wanaounga mkono makubaliano hayo wamefurahishwa na
maendeleo hayo, wakisema wameyasubiri kwa muda mrefu. Mkurugenzi wa
shirika lisilo la kiserikali la muungano wa asasi za kudhibiti silaha,
Anna Macdonald, amesema kwa muda mrefu silaha zimekuwa zikiuzwa, lakini
maswali bado yanabaki kwa wale wanaoathirika na silaha hizo.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, nchi zilizotia saini zinalazimika
kuunda vitengo vya kitaifa vya kukagua bishara ya silaha zinazouzwa nje
ya nchi.
Nchi hizo zinapaswa pia kufanya tathmini kuangalia kama silaha
zinazouzwa nje zinaweza kukwepa vikwazo vya kimataifa, kutumiwa katika
mauaji ya halaiki au katika uhalifu wa kivita, au kama zinaweza
kuangukia mikononi mwa makundi ya ugaidi au ya kihalifu.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon amesema makubaliano hayo
yanaonesha dhamira ya mataifa mbalimbali, mashirika ya kimataifa na
asasi za kiraia kuachana na biashara ya silaha. Ban amesema anaendelea
kuyahimiza mataifa yote, hasa yanayouza silaha kwa wingi kusaini
makubaliano hayo. Pia ameyataka mataifa yote yaliyoridhia makubaliano
hayo kuanza kuyatekeleza mara moja bila ya kuchelewa.
Kamishna wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa azungumza
Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa
Mataifa, Zeid Ra'ad Al Hussein, ameyapongeza makubaliano hayo kama mfumo
wa kukomesha kutiririka kwa silaha ambazo zinaweza kutumika kufanya
mauwaji, uhalifu na ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu.
Wanaharakati wanasema kutekelezwa kwa makubaliano hayo kutasaidia
kuifanya biashara ya silaha kuwa ngumu zaidi kuingizwa kwenye maeneo
yenye mizozo duniani kama vile Syria, Sudan Kusini na maeneo mengine ya
Mashariki ya Kati pamoja na Afrika. Mkutano wa kwanza wa mataifa
yaliyosaini makubaliano hayo utafanyika mwezi Septemba, mwaka ujao. Tangu yalipoidhinishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa miaka miwili
iliyopita, makubaliano hayo yamesainiwa na nchi 130, lakini yameridhiwa
na nchi 60 tu, zikiwemo Ujerumani, Ufaransa, Italia, Uhispania na
Uingereza pamoja na Israel ambayo imeridhia mwezi huu. Marekani ambayo ndiyo mtengenezaji mkubwa na msafirishaji wa silaha
duniani, imesaini makubaliano hayo lakini bado inasubiri ridhaa ya
Baraza la Seneti. Mataifa mengine yanayotengeneza silaha kwa wingi kama
vile China, Urusi, India na Pakistan bado hayajasaini makubaliano hayo.
CHANZO: DW KISWAHILI
No comments:
Post a Comment