Rais Joachim Gauck wa Ujerumani amewataka raia wa nchi hiyo kuonesha
huruma, ukarimu na upole kwa wakimbizi, ikiwa ni sehemu ya ujumbe wake
wa Krismasi kwa taifa.
Rais Gauck amewataka wananchi wa Ujerumani wawe tayari kusaidia badala
ya kujifungia ndani ya mipaka yao na kujitenga na wengine. Bwana Gauck
ameitaka Ujerumani iwe jamii ya uwazi.
Amesema pale ambapo Ujerumani inaweza kutoa mchango katika kudumisha
amani na kusaidia katika juhudi za kupunguza dhiki , itapasa kufanya
kila linalolazimu.
Juu ya kuwa tayari kuonyesha huruma kwa wakimbizi Rais wa Ujerumani
amesema Wajerumani watakuwa na furaha na faraja ikiwa watawashirikisha
wengine katika kile ambacho wao wenyewe wanatumai kukipata.
Rais wa shirikisho la Ujerumani amewapongeza wananchi wake kwa
kujitokeza kwa wingi kupinga tabia ya kujifungia ndani ya mipaka yao na
kujitenga na wengine.Gauck amesema kuwa mtazamo huo umempa moyo. Katika ujumbe wake wa Krismasi ,Gauck pia amewaambia wananchi
wa Ujerumani kwamba hawana haja ya kuwa na hofu juu ya dunia
inayowazunguka. Badala yake amewashauri wananchi wake wajaribu kuzielewa
changamoto zinazoikaili jamii yao na pia wayazingatie maadili yao.
Bwana Gauck aliekuwa mchungaji wa Kiprotestanti na mtetezi wa haki za
kiraia katika iliyokuwa Ujerumani Mashariki, ametilia maanani katika
hotuba yake kwamba watu wengi wana wasi wasi kutokana na vita na vitendo
vya ugaidi ambavyo amesema vinafanyika kwa kulitumia jina la dini.
Mwaka wa migogoro na vita
Rais wa Ujerumani ameeleza kwamba wakati mwaka huu unapoagwa inapasa
kukumbuka yaliyotokea katika mwaka huo. Amesema mwaka huu ulikuwa wa
migogoro, vita ,mauaji na ugaidi uliofanywa kwa kulitumia jina la
dini.Amesema Kila siku watu wanauliwa. Katika ujumbe wake wa Krismasi Rais wa Ujerurmani pia
amewapongeza Wajerumani wanaoshiriki katika harakati za kupambana na
maradhi ya Ebola katika nchi za Afrika magharibi. Pia amewapongeza
askari wa Ujerumani wanaoshiriki katika juhudi za kuleta amani katika
sehemu mbalimbali za dunia. Bwana Gauck ameelezea matumaini kwamba masuluhisho yanaweza kupatikana.
Amesema japo siyo rahisi kuyaleta masuluhisho hayo,litakuwa jambo la
kukatisha tamaa ikiwa watu watakuwa na hofu. Bila ya kutumia kauli ya uwazi Rais Gauck amezungumzia juu ya jumuiya ya
watu wanaojiita " Pegida." katika miezi ya hivi karibuni Ujerumani
imeshuhudia kuibuka wimbi la maalfu ya watu wanaoandamana kuupinga
Uislamu katika miji kadhaa .
Wazalendo wanaoupinga Uislamu barani Ulaya
Watu hao wanajiita wazalendo waopinga kusilimishwa kwa magharibi, Watu
hao wanafanya maandamano kila wiki. Jumatatu iliyopita watu 17,500
walishiriki katika maandamano kama hayo.Lakini wakati huo huo wananchi
wengine wa Ujerumani pia wamekuwa wanajitokeza kuwapinga watu hao.
CHANZO: DW KISWAHILI
No comments:
Post a Comment